• HABARI MPYA

    Friday, September 14, 2012

    YANGA SAA 14 MBEYA, WANAIONJA SOKOINE LEO

    Yanga SC

    Na Princess Asia
    KOCHA Mkuu wa Yanga, Mbelgiji Tom Saintfiet anatarajiwa kuiongoza timu yake katika mazoezi ya kwanza kwenye Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya leo, ili kuuonja klabla ya mechi ya kesho ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara dhidi ya Prisons.
    “Baada ya safari ya saa 14 na dakika 30, tumefika Mbeya salama,”alisema Mtakatifu Tom alipozungumza kwa simu na BIN ZUBEIRY jana, saa 4:00 usiku.
    Tayari Mtakatifu Tom amesema kwamba mechi hiyo itakuwa ngumu kwa sababu anaamini wapinzani wao watakamia na watasaidiwa na kucheza nyumbani.
    Lakini pia, Saintfiet alisema Prisons haina presha ya kufungwa na Yanga kwa sababu ni timu kubwa, hivyo watacheza kwa utulivu, wakipata sare ni safi, wakifungwa hakuna tatizo na wakishinda kwao itakuwa ‘sikukuu’.
    Kwa sababu hizo, Mtaalamu huyo wa Kibelgiji anaamini mechi hiyo itakuwa ngumu kwao na timu yake inaondoka leo Dar es Salaam kwenda Mbeya ikilijua hilo.   
    Mtakatifu Tom ametaua wachezaji 22 kwa ajili ya mechi hiyo na amesema ameteua wachezaji hao kulingana na mazingira ya mechi yenyewe na kwamba wachezaji wengine wote waliobaki ni wazuri pia.
    Aliwataja wachezaji aliowateua kuwa ni makipa; Yaw Berko, Ally Mustafa ‘Barthez’, mabeki Shadrack Nsajigwa, Juma abdul, Godfrey Taita, Mbuyu Twite, Kevin Yondan,  Nadir Haroub ‘Cannavaro’, David Luhende, Oscar Joshua na Stefano Mwasyika.
    Aliwataja viungo ni Athumani Iddi ‘Chuji’, Haruna Niyonzima, Frank Domayo, Rashid Gumbo, Nizar khalfan, Shamte Ally na Simon Msuva, wakati washambuliaji ni Jerry Tegete, Didier Kavumbangu, Said Bahanuzi na Hamisi Kiiza.
    Aliwataja wachezaji wa kikosi cha kwanza ambao hawatasafiri kwa ajili ya mechi hiyo kuwa ni kipa Said Mohamed, Ladislaus Mbogo, Job Ibrahim, Juma Seif ‘Kijiko’, Salum Telela, Omega Seme, Nurdin Bakari, Idrisa Assega na Issa Ngao wa Yanga B, ambaye anakomazwa kikosi cha kwanza.
    Jumamosi Yanga ilicheza mechi ya mwisho ya kujipima nguvu kabla ya kuanza kwa Ligi Kuu na kushinda mabao 4-0 dhidi ya Moro united, Mrundi Didier Kavumbangu akifunga mawili, mengine beki Juma Abdul na kiungo Shamte Ally. 
    “Kavumbangu aliwahi kufunga pia tulipocheza na Sinza Stars, ninafurahia hilo, ni muhimu kwa klabu kubwa, lakini pia wachezaji wengine wanaweza kufunga, Stefano Mwasyika, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Juma Abdul…tumecheza mechi 14 kabla ya ligi, zikiwemo dhidi ya Sinza Stars na Kijitonyama Stars, tumefunga mabao 42 na tumefungwa sita tu,”alisema Mtakatifu Tom.
    Saintfiet alitaka mechi moja dhidi ya timu inayocheza kama wapinzani wao wa kwanza katika Ligi Kuu, Prisons na pia katika Uwanja mbaya kama ambao atachezea mechi ya kwanza ya ligi hiyo, Sokoine mjini Mbeya na ndiyo maana timu hiyo ikacheza na Moro United juzi kwenye Uwanja wa Shule ya Msingi Kijitonyama.
    Saintfiet ameridhika na kiwango cha timu na sasa anasema timu iko tayari kwa Ligi Kuu, akianza na Prisons iliyorejea Ligi Kuu msimu huu kwenye Uwanja wa Sokoine, Septemba 15.
    Hiyo ilikuwa mechi ya 11, Saintfiet anashinda Yanga katika mechi 12 tangu ajiunge nayo miezi miwili iliyopita, mbali ya ziwe za mazoezini dhidi ya Sinza Stars na Kijitonyama Stars.
    Ndani ya mechi hizo kuna mechi sita za Klabu Bingwa ya soka Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame, ambalo aliiwezesha Yanga kutwaa ubingwa wa tano wa michuano hiyo, ikipoteza mechi moja tu ya kwanza dhidi ya Atletico ya Burundi, kwa kufungwa 2-0, mabao yote ya Kavumbangu, ambaye baadaye ikamsajili. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: YANGA SAA 14 MBEYA, WANAIONJA SOKOINE LEO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top