Ally Mustafa 'Barthez' akiteremka kwenye basi Uwanja wa Jamhuri, Morogoro juzi. |
Na Mahmoud Zubeiry
KAMBI
inahama. Yanga waliingia kambini jana, makao makuu ya klabu yao, makutano ya
mitaa ya Twiga na Jangwani, lakini leo hawatalala hapo tena.
Habari
kutoka ndani ya Yanga zimesema kwamba kambi inahama kwa sababu mazingira ya
hosteli hiyo ya klabu kwa ujumla si mazuri- na zaidi kuwaepushia wachezaji
usumbufu kutoka kwa baadhi ya wanachama wenye desturi mbaya.
Hatua ya
Yanga kuingia kambini inafuatia
kuambulia pointi moja katika mechi mbili za Ligi Kuu, ikitoa sare na Prisons
0-0 mjini Mbeya Jumamosi na kufungwa 3-0 na Mtibwa Sugar mjini Morogoro jana.
Meneja wa
Yanga, Hafidh Saleh aliwataja wachezaji 30 walioingia kambini hiyo jana
kujiandaa na mchezo wa Jumamosi dhidi ya JKT Ruvu, Uwanja wa Taifa, Dar es
Salaam kuwa ni Nizar Khalfan, Athumani Iddi ‘Chuji’, Shamte Ally Kilalile, Said
Rashid Bahanuzi, Haruna Niyonzima Fadhili, Didier Kavumbagu Fortine, Juma Seif
Dion ‘Kijiko’, Nadir Haroub Ally ‘Cannavaro’, Nurdin Bakari Hamad, Said Mohamed,
Rashid Omary Gumbo, Juma Jaffar Abdul, Omega Sunday Seme na Kevin Yondan
Patrick.
Wengine ni Jerson
John Tegete, Idrisa Rashid Abdallah, Godfrey Taita Magina, Oscar Joshua Nkulula,
David Charles Luhende, Ibrahim Job Isaac, Ladislaus Mbogo Mahendeka, Ally Mustafa
Mtinge ‘Barthez’, Shadrack Joel Nsajigwa, Hamisi Friday Kiiza, Yaw Koffi Berko,
Stephano Asangalwisye Mwasyika, Mbuyu Twite Banza, Simon Msuva, Frank Domayo na
Issa Ngao.
Wakati Yanga
wanakumbuka kambi baada ya kupoteza pointi tano katika mbio za ubingwa wa Ligi
Kuu, tangu wamerejea kutoka Arusha wiki wiki mbili zilizopita, wapinzani wao wa
jadi, Simba SC wamekuwa kambini hoteli ya Sapphire, Kariakoo, Dar es Salaam.
Kuanza
vibaya kwa Yanga katika Ligi Kuu kumeibua maswali na maoni mengi, kocha akisema
wachezaji wamevimba vichwa na hawajitumi tena, jambo ambalo limeungwa mkono na
uongozi ambao sasa unawaweka chini ya uangalizi maalum wachezaji hao.
Saintfiet alisema
kwamba wachezaji wake wamelewa sifa baada ya mwanzo mzuri wa msimu na kila
mmoja sasa anajiona ‘staa’ kiasi cha kutocheza kwa kujituma, hali ambayo
imechangia timu yake kuanza vibaya katika Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.
Akizungumza
na BIN
ZUBEIRY jana, Mtakatifu Tom alisema kwamba wachezaji wanatakiwa
kubadilika haraka, vinginevyo mabadiliko yatahitajika katika timu.
“Nimesononeshwa
mno tena, na ninaomba radhi kwa mashabiki, wanastahili ushindi, tuna mashabiki
wazuri, katika mechi (ya juzi) tulipata nafasi nane nzuri asilimia 100, mita
tano kutoka langoni kwa wapinzani, tulipoteza hadi penalti. Si kawaida,”.
“Mtibwa
Sugar si timu mbaya, walipata nafasi nne na wakafunga mabao matatu, mashuti
mawili ya kiwango cha dunia. Kama tusingetengeneza nafasi, ingekuwa rahisi
kwangu kama kocha kulaumiwa, lakini sasa sisi makocha hatuwezi kupiga mpira
kupeleka nyavuni, na wachezaji ndio wanatakiwa kufanya hivyo,”.
“Hii inauma,
kufanya vizuri Kombe la Kagame na kuanza vibaya katika ligi, wachezaji fulani
si wachezaji tena, wanajiona mastaa, hivyo wanatakiwa kuzinduka haraka,
vinginevyo mabadiliko yanahitajika,”alisema Mtakatifu Tom.
Mechi ya juzi
ilikuwa ya pili kwa Yanga kufungwa chini ya Saintfiet tangu aanze kazi Julai
mwaka huu, akirithi mikoba ya Mserbia, Kostadin Bozidar Papic aliyetupiwa
virago, katika mechi 14 alizoiongoza timu hiyo hadi sasa, ambazo ndani yake
zipo sita za Kombe la Kagame, aliloiwezesha timu hiyo kutwaa.
Yanga
iliyoanza ligi kwa sare ya bila kufungana na Prisons mjini Mbeya, juzi
ilifungwa 3-0 na Mtibwa Sugar katika mchezo wake wa pili, kwenye Uwanja wa
Jamhuri, Morogoro.
0 comments:
Post a Comment