![]() |
Yanga SC |
Na Mahmoud Zubeiry
YANGA SC
inatarajiwa kuondoka leo saa nane mchana kwa njia ya basi kwenda Morogoro,
tayari kwa mchezo wa kesho wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, dhidi ya
wenyeji Mtibwa Sugar, kwenye Uwanja wa Jamhuri, Morogoro.
Huo utakuwa
mchezo wa pili kwa Yanga katika ligi hiyo, baada ya awali kulazimishwa sare ya
bila kufungana na Prisons kwenye Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya Jumamosi.
Kocha Mkuu
wa Yanga, Mbelgiji Tom Saintfiet jana aliwaomba radhi mashabiki wa Yanga kwa sare
ya Jumamosi kwenye Uwanja wa Sokoine na akawatupia lawama viongozi wa klabu
hiyo, kwa maandalizi mabovu.
Lakini Mbelgiji
huyo amesema leo anapeleka wachezaji 18 Morogoro kwa ajili ya mechi ya pili ya
Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara dhidi ya Mtibwa Sugar, akiwa ana matumaini
makubwa ya ushindi.
Saintfiet alilalamikia
kulala kwenye hoteli mbaya, yenye vitanda vichache na vidogo, vilivyosababisha
watu wakalala mzungu wa nne, na chakula kibaya na kwa ujumla alisema hawakuwa
vizuri kabla ya mechi hiyo. Alisema yeye
alilala kitanda kimoja na Louis Sendeu na Mbuyu Twite alibanana na Didier
Kavumbangu na hoteli haikuwa na mabomba vyooni wala bafuni, hivyo kulazimika kuingia
na ndoo na kuogea kata.
Alisema pia
hoteli hiyo ilikuwa katikati ya mji na karibu na stendi ya mabasi, kila
alfajiri kelele nyingi na kwa ujumla timu iliingia uwanjani ikiwa haiku vizuri.
“Mimi kwa
mfano sijaoga siku mbili, kwa kweli tulikuwa katika mazingira magumu na
wapinzani wetu walicheza soka ya kuudhi tangu mwanzo, kupoteza muda, na marefa
hawakuchukua hatua, tulipoteza nafasi kupitia kwa Kiiza (Hamisi) na Msuva
(Simon), siwezi kulaumu mchezaji wangu yeyote, lakini hiyo ndiyo hali
halisi,”alisema Saintfiet.
Baada ya mazoezi
ya asubuhi kwenye Uwanja wa sekondari ya Loyola, Mabibo, Dar es Salaam na saa 8:00
mchana watasafiri kwa njia ya barabaraba kwenda Morogoro ambako wakifika
watatafuta hoteli nzuri mapema.
Alisema
anajua hata Uwanja wa huko, Jamhuri si mzuri na mechi itakuwa ngumu kwa sababu
Mtibwa Sugar nao walitoka sare ya bila kufungana na Polisi katika mchezo wao wa
kwanza Jumamosi na anaiheshimu timu hiyo kama moja ya timu tano kubwa Tanzania,
pamoja na Simba, Azam na Coastal Union.
“Lakini
pamoja na kwamba Simba wamependelewa kupangiwa ratiba ya kuanza kucheza
nyumbani mechi tano mfululiuzo, nakuambia Mei mwaka 2013 Yanga ndio itavishwa
taji la ubingwa wa Ligi Kuu, acha wafurahie sasa hivi, watalia mwisho,”alisema
Mtakatifu Tom.
Kuhusu
wachezaji 18 anaokwenda nao Morogoro, Mtakatifu Tom alisema atawataja baada ya
mazoezi ya leo na hiyo inaonekana ni kwa sababu ya kufuatilia hali za wachezaji
ambao kwa sasa hawako vizuri, akiwemo kiungo Haruna Niyonzima.
Wachezaji
aliokwenda nao Mbeya walikuwa ni makipa; Yaw Berko, Ally Mustafa ‘Barthez’,
mabeki Shadrack Nsajigwa, Juma abdul, Godfrey Taita, Mbuyu Twite, Kevin
Yondan, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, David
Luhende, Oscar Joshua na Stefano Mwasyika.
Aliwataja
viungo ni Athumani Iddi ‘Chuji’, Haruna Niyonzima, Frank Domayo, Rashid Gumbo,
Nizar khalfan, Shamte Ally na Simon Msuva, wakati washambuliaji ni Jerry
Tegete, Didier Kavumbangu, Said Bahanuzi na Hamisi Kiiza, wakati waliobaki
walikuwa ni kipa Said Mohamed, mabeki Ladislaus
Mbogo, Job Ibrahim, viungo Juma Seif ‘Kijiko’, Salum Telela, Omega Seme, Nurdin
Bakari, Idrisa Assega na Issa Ngao wa Yanga B, anayekomazwa kikosi cha kwanza.
0 comments:
Post a Comment