• HABARI MPYA

    Thursday, March 07, 2013

    HII NDIYO SABABU HASWA KWA NINI HANS POPPE AMEACHIA NGAZI SIMBA SC

    Hans Poppe

    Na Mahmoud Zubeiry
    ALIYEKUWA Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba SC na Mjumbe wa Kamati ya Utendaji, Zacharia Hans Poppe, amesema kwamba ameamua kujiuzulu nyadhifa zote hizo kwa sababu kuna mgawanyiko ndani ya uongozi unaokwamisha maendeleo.
    Akizungumza na BIN ZUBEIRY ofisini kwake jioni hii Mbezi Beach, Dar es Salaam, Hans Poppe amesema kwamba kwa kuona hawapati mafanikio wanayoyatarajia, ameamua kung’atuka kuwapisha wengine.
    “Kwa muda wa takriban miaka mitatu sasa nimekuwa nikishikilia nyadhifa ndani ya Simba. Nimejitahidi kutekeleza majukumu yangu kadiri ya uwezo wangu, lakini naona hatupati mafanikio tunayoyatarajia, ”alisema.
    “Ni wazi kuwa kwenye uongozi tumekuwa hatufanyi kazi kwa umoja na mgawanyiko huu unatukwaza na hatuwezi kupata maendeleo,”alisema Hans Poppe.
    “Baada ya kutafakari, nimeona ni bora nijiuzulu nyadhifa hizo kupisha wengine ambao wanaweza wakawa na mawazo mapya ya kuendeleza klabu, nami nitabakia kuwa mwanachama mwaminifu daima,”alisema Hans Poppe.
    Poppe amewasilisha barua ya kujiuzulu Simba SC leo na wazi kujiuzulu kwa Kapteni huyo wa zamani wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) ni pigo kwa klabu hiyo, kwani alikuwa akiisaidia mno kwa hali na mali.
    Aidha, kujiuzulu kwa Hans Poppe wazi kutachochea zaidi mgogoro ndani ya klabu hiyo na kuongeza shinikizo la viongozi wa klabu hiyo kujiuzulu pia.
    Simba SC kwa sasa haifanyi vizuri katika Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara na tayari imekwishatolewa katika Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kufungwa jumla ya mabao 5-0 na Recreativo de Libolo ya Angola katika raundi ya kwanza tu.     
    Ubingwa wa Ligi Kuu ni kama umekwishaota mbawa, kwani hadi sasa Wekundu hao wa Msimbazi wanashika nafasi ya tatu wakiwa na pointi 31, sawa na Coastal Union ya Tanga na Mtibwa Sugar ya Morogoro, nyuma ya Azam FC yenye pointi 36 na Yanga inayoongoza kwa pointi zake 42, zote za Dar es Salaam.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: HII NDIYO SABABU HASWA KWA NINI HANS POPPE AMEACHIA NGAZI SIMBA SC Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top