• HABARI MPYA

    Thursday, March 07, 2013

    KABURU NAYE ABWAGA MANYANGA SIMBA SC KWA BARUA PEPE

    Kaburu; Amejiuzulu Simba SC?

    Na Mahmoud Zubeiry
    MAKAMU Mwenyekiti wa Simba SC, Geoffrey Nyange ‘Kaburu’ inadaiwa amemuandikia barua pepe, Mwenyekiti wa klabu hiyo, Alhaj Ismail Aden Rage kumtaarifu kujiuzulu wadhifa huo. 
    Habari ambazo BIN ZUBEIRY imezipata jioni hii zimedai kuwa, Kaburu amemuandikia barua pepe Rage, ambaye kwa sasa yupo India kwa matibabu ya mgongo kumjulisha uamuzi wake huo.
    Juhudi za kumpata Kaburu mwenyewe kuzungumzia habari hizo, hazikufanikiwa kutokana na simu zake zote kutopatikana.
    Kaburu anakuwa kiongozi wa pili wa Kamati ya Utendaji ya Simba kujiuzulu leo, baada ya awali mchana, Zacharia Hans Poppe aliyekuwa Mjumbe kujiuzulu pia.   
    Hans Poppe, aliyekuwa pia Mjumbe wa Kamati ya Utendaji, alisema kwamba ameamua kujiuzulu nyadhifa zote hizo kwa sababu kuna mgawanyiko ndani ya uongozi unaokwamisha maendeleo.
    Akizungumza na BIN ZUBEIRY ofisini kwake jioni ya leo Mbezi Beach, Dar es Salaam, Hans Poppe alisema kwamba kwa kuona hawapati mafanikio wanayoyatarajia, ameamua kung’atuka kuwapisha wengine.
    “Kwa muda wa takriban miaka mitatu sasa nimekuwa nikishikilia nyadhifa ndani ya Simba. Nimejitahidi kutekeleza majukumu yangu kadiri ya uwezo wangu, lakini naona hatupati mafanikio tunayoyatarajia, ”alisema.
    “Ni wazi kuwa kwenye uongozi tumekuwa hatufanyi kazi kwa umoja na mgawanyiko huu unatukwaza na hatuwezi kupata maendeleo,”alisema Hans Poppe.
    “Baada ya kutafakari, nimeona ni bora nijiuzulu nyadhifa hizo kupisha wengine ambao wanaweza wakawa na mawazo mapya ya kuendeleza klabu, nami nitabakia kuwa mwanachama mwaminifu daima,”alisema Hans Poppe.
    Poppe amewasilisha barua ya kujiuzulu Simba SC leo na wazi kujiuzulu kwa Kapteni huyo wa zamani wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) ni pigo kwa klabu hiyo, kwani alikuwa akiisaidia mno kwa hali na mali.
    Aidha, kujiuzulu kwa Hans Poppe wazi kutachochea zaidi mgogoro ndani ya klabu hiyo na kuongeza shinikizo la viongozi wa klabu hiyo kujiuzulu pia.
    Simba SC kwa sasa haifanyi vizuri katika Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara na tayari imekwishatolewa katika Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kufungwa jumla ya mabao 5-0 na Recreativo de Libolo ya Angola katika raundi ya kwanza tu.     
    Ubingwa wa Ligi Kuu ni kama umekwishaota mbawa, kwani hadi sasa Wekundu hao wa Msimbazi wanashika nafasi ya tatu wakiwa na pointi 31, sawa na Coastal Union ya Tanga na Mtibwa Sugar ya Morogoro, nyuma ya Azam FC yenye pointi 36 na Yanga inayoongoza kwa pointi zake 42, zote za Dar es Salaam.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: KABURU NAYE ABWAGA MANYANGA SIMBA SC KWA BARUA PEPE Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top