• HABARI MPYA

    Sunday, March 10, 2013

    KINESI AOKOA JAHAZI, SIMBA YARUHUSIWA KUTOKA HOTELINI, SASA IPO NJIANI YAELEKEA TAIFA KUPAMBANA NA WAGOSI WA KAYA

    Kikosi cha Simba SC; Charuhusiwa kutoka hotelini

    Na Mahmoud Zubeiry
    KAIMU Mwenyekiti wa Simba SC, Joseph Itangare ‘Kinesi’ amefanikiwa kuushawishi uongozi wa hoteli ya Sapphire Court, Kariakoo, Dar es Salaam uiruhusu timu kutoka katika hoteli hiyo iende Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kumenyana na Coastal Union ya Tanga katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara. 
    Wachezaji wa Simba SC walifungiwa katika hoteli ya Sapphire Court na kuzuiwa kutoka kwenda Uwanja wa Taifa, kumenyana na Coastal Union leo kutokana na ukubwa wa deni.
    Kwa mujibu wa Mhudumu mmoja wa hoteli hiyo, baada ya hapo, ndipo viongozi wa Simba wakiongozwa na Kinesi wakafika na kuzungumza na Menejimenti ya hoteli hiyo.
    “Mzee Kinesi ameomba, amekubaliwa kwa makubaliano maalum juu ya ulipwaji wa deni na timu imeruhusiwa kuondoka sasa,”alisema Mhudumu wa hoteli hiyo alipozungumza na BIN ZUBEIRY mida hii.
    Hamkani si shwari sasa ndani ya Simba SC, kufuatia viongozi wawili wa Kamati ya Utendaji, aliyekuwa Makamu Mwenyekiti, Geoffrey Nyange ‘Kaburu’ na Mjumbe wa Kamati ya Utendaji, Zacharia Hans Poppe kujiuzulu wiki hii.
    Wakati huo huo, Mwenyekiti wa Simba SC, Alhaj Ismail Aden Rage yuko India kwa matibabu na Kinesi aliyeteuliwa kukaimu Umakamu Mwenyekiti, sasa ndiye anakaimu Uenyekiti wa klabu.
    Aidha, Baraza la Wazee kwa pamoja na Baraza la Wadhamini, wameunda Kamati Maalum ya kusimamia timu kuhakikisha inafanya vizuri katika wakati huu mgumu, chini ya Mwenyekiti, Rahma Al Kharoos, maarufu kama Malkia wa Nyuki.
    Leo ndio unatarajiwa kuwa mtihani wa kwanza kwa Malkia wa Nyuki tangu akabidhiwe timu, wakati itakapomenyana na Coastal Union ya Tanga katika mchezo wa Ligi Kuu jioni hii Uwanja wa Taifa.
    Simba SC kwa sasa haifanyi vizuri katika Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara na tayari imekwishatolewa katika Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kufungwa jumla ya mabao 5-0 na Recreativo de Libolo ya Angola katika raundi ya kwanza tu.     
    Ubingwa wa Ligi Kuu ni kama umekwishaota mbawa, kwani hadi sasa Wekundu hao wa Msimbazi wanashika nafasi ya tatu wakiwa na pointi 31, sawa na Coastal Union ya Tanga na Mtibwa Sugar ya Morogoro, nyuma ya Azam FC yenye pointi 37 na Yanga inayoongoza kwa pointi zake 45, zote za Dar es Salaam.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: KINESI AOKOA JAHAZI, SIMBA YARUHUSIWA KUTOKA HOTELINI, SASA IPO NJIANI YAELEKEA TAIFA KUPAMBANA NA WAGOSI WA KAYA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top