![]() |
Na Bin Zubeiry |
KATIKA mechi ya tatu mfululizo, Jumamosi washambuliaji wa Yanga walitoka uwanjani bila kufunga bao, wakimenyana na Toto Africans ya Mwanza katika Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Yanga ilishinda 1-0, bao pekee la kiungo Nizar Khalfan aliyeingia kipindi cha pili uwanjani kuchukua nafasi ya Jerry Tegete.
Mechi mbili zilizotangulia pia Yanga ilipata ushindi mwembamba wa 1-0, dhidi ya Azam FC ya Dar es Salaam na baadaye Kagera Sugar ya Bukoba, zote mabao akifunga kiungo Haruna Niyonzima.
Washambuliaji wa Yanga wana bahati kucheza wamezungukwa na viungo hodari ambao wamekuwa wakiwatengenezea nafasi nzuri. Nasema nafasi nzuri, kwa sababu ni nafasi za kukutana na mipira kwenye njia kuunganisha tu nyavuni, lakini wanakosea.
Mipira inawapita wanapiga hewa, ama wanapiga nje au wanawadakisha makipa.
Ukiifuatilia sana Yanga chini ya kocha Mholanzi, Ernie Brandts imekuwa ikifunga mabao mengi katika mechi nyepesi mno na uwezo wa kufunga wa washambuliaji wote, Hamisi Kiiza, Jerry Tegete, Didier Kavumbangu na Said Bahanuzi umeshuka kwa kiasi kikubwa.
Uwezo wa kushambulia bado wanao, tena mkubwa sana- lakini kutumbukiza mpira nyavuni, hadi kwa penalti pia shaka. Kama unavyojua magazeti ya nyumbani, wakati mwingine yanaibuka na habari kichekesho, zikaibuka habari za wachezaji kulogana.
Mimi siamini juu ya hilo na vyombo vya habari vinapaswa kuwa mstari wa mbele kukemea hayo mambo ni si kuyashabikia.
Kwa nini washambuliaji wa Yanga hawafungi? Kwa sasa, Yanga inaongoza Ligi Kuu na timu inashinda kwa mbinde, hakuna anayeweza kuona kama kuna tatizo kwenye timu, ingawa lipo hilo la ubutu wa safu ya ushambuliaji.
Tutasubiri Yanga iingie kwenye michuano ya Afrika icheze na timu ngumu ishindwe kufunga mabao, ndipo watu waanze kusema timu haina washambuliaji. Hiyo ndio kawaida yetu Watanzania.
Kuna tatizo kwa washambuliaji wa Yanga. Kuna kitu wanakosa katika mazoezi yao na mafundisho yao ya kila siku, mbinu za kufunga. Utaona Yanga inacheza kwa mpangilio mzuri kuanzia nyuma, lakini wanapofika kwenye eneo la hatari la wapinzani ndio mushkeli.
Jumamosi Hamisi Kiiza aliingia yeye nyavuni mpira ukimpita wakati akijaribu kuunganisha krosi ya Haruna Niyonzima. Nilicheka sana. Nilijiuliza, alikuwa amefumba macho? Kweli, unaweza kujiuliza wanakosaje mabao ya wazi wachezaji wa Yanga, huwa wanafumba macho wanapotaka kufunga?
Yote kwa yote, kuna kitu washambuliaji wa Yanga wanakosa katika mafundisho yao, mbinu za kufunga mabao na hilo litawapa tabu siku zijazo, iwapo halitatafutiwa ufumbuzi mapema.
Naikumbuka APR ya Rwanda ilipokuwa chini ya Brandts katika Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame ilikuwa inacheza vizuri kuanzia nyuma, lakini kwenye kufunga lilikuwa tatizo na haikuwa ajabu walipofungwa mechi zote mbili na Yanga, wakati huo ikifundishwa na Mbelgiji, Tom Saintfiet.
Naona tatizo hilo limehamia Yanga na sishangai sana, kwa sababu Brandts ni kocha ambaye enzi zake alikuwa beki hodari na huwezi kustaajabu Yanga ina ukuta imara. Mbaya zadi, Msaidizi wake pia Freddy Felix Minziro pia alikuwa beki na makocha wengi wanaotokea uwanjani, zaidi wanafundisha kwa uzoefu wa kucheza.
Brandts ni kocha mzuri, ametengeneza Yanga imara, inayocheza soka ya kuvutia, tena ikishambulia mno- lakini kuna hilo tatizo la washambuliaji kufilisika mbinu za kufunga. Nini kifanyike hapa?
Wamepita washambuliaji wengi bora Yanga na wengi wao wamesomea ukocha. Vema klabu ikamchukua mmojawao, impe jukumu la kuwanoa washambuliaji wa timu hiyo, maana haiyumkiniki timu iachane na kocha mzuri kama Brandts kwa sababu tu ameshindwa kupika washambuliaji, japokuwa ametengeneza timu imara.
Yanga wanatakiwa kuzingatia usemi wa wahenga kwamba, wasipoziba ufa, watajenga ukuta. Wasalam.