![]() |
| Malkia wa Nyuki; Mpira Pesa wampokea kwa mikono miwili |
Na Mahmoud Zubeiry
MWENYEKITI wa Kamati Maalum ya Kuinusuru Simba SC katika wakati huu mgumu, Rahma Al Kharoos au Malkia wa Nyuki kwa jina la utani, jana alikuwa na kikao na Tawi la Mpira Pesa Magomeni, Dar es Salaam.
Akizungumza na BIN ZUBEIRY jana usiku baada ya kikao hicho, Malkia wa Nyuki alisema kikao kilienda vizuri na Mpira Pesa wameahidi kumpa ushirikiano katika jitihada za kuinusuru Simba SC.
“Kwa kweli kikao kilikuwa kizuri sana, tumezungumza na tumekubaliana wote kuwa kitu kimoja katika kipindi hiki kigumu, kuhakikisha tunaokoa jahazi la Simba SC,”alisema Malkia wa Nyuki.
Alhamisi wiki hii, Wajumbe wa Baraza la Wazee na la Wadhamini ndani ya Simba SC, waliunda Kamati maalum ya kuinusuru timu katika wakati huu mgumu chini ya Mwenyekiti, Rahma Al Kharoos.
Na Ijumaa Makamu Mwenyekiti wa klabu hiyo, Geoffrey Nyange ‘Kaburu’ na Mjumbe wa Kamati ya Utendaji, Zacharia Hans Poppe aliyekuwa pia Mwenyekiti wa Kamati nyeti ya Usajili, walijiuzulu.
Sasa mtihani wa kwanza wa Malkia wa Nyuki ni mechi ya kesho ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara dhidi ya Coastal Union ya Tanga kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Mechi hiyo itachezeshwa na refa Martin Saanya atakayesaidiwa na Jesse Erasmo na Vincent Mlabu wote kutoka mkoani Morogoro.
Simba SC kwa sasa haifanyi vizuri katika Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara na tayari imekwishatolewa katika Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kufungwa jumla ya mabao 5-0 na Recreativo de Libolo ya Angola katika raundi ya kwanza tu.
Ubingwa wa Ligi Kuu ni kama umekwishaota mbawa, kwani hadi sasa Wekundu hao wa Msimbazi wanashika nafasi ya tatu wakiwa na pointi 31, sawa na Coastal Union ya Tanga na Mtibwa Sugar ya Morogoro, nyuma ya Azam FC yenye pointi 36 na Yanga inayoongoza kwa pointi zake 42, zote za Dar es Salaam.
Wakati Kaburu na Hans Poppe wanajiuzulu, Mwenyekiti wa Simba SC, Alhaj Ismail Aden Rage yuko India kwa matibabu ya mgongo. Rage anasumbuliwa na maradhi ya mgongo na sasa ni takriban mara ya tatu anakwenda nchini humo kwa tiba tangu mwishoni mwa mwaka jana.
Habari zaidi zinasema, hata Rage yuko tayari kujiuzulu ili uitishwe uchaguzi mpya, lakini alipanga kufanya hivyo katika Mkutano Mkuu ambao alipanga kuuitisha wakati wowote tangu wiki iliyopita.



.png)