![]() |
Mrisho Khalfan Ngassa wa Simba SC, akiruka kwanja la beki wa Coastal katika mechi hiyo ya juzi. |
Na Boniface Wambura
MECHI ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara kati ya Simba SC na Coastal Union iliyochezwa juzi Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam imeingiza sh. 36,820,000 kutoka na watazamaji 6,284.
Viingilio katika mechi hiyo namba 138 iliyomalizika kwa Simba kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 vilikuwa sh. 5,000, sh. 8,000, sh. 15,000 na sh. 20,000 huku kila klabu ikipata mgawo wa sh. 8,265,752.45 wakati Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) iliyolipwa ni sh. 5,616,610.17.
Mgawo mwingine wa mapato hayo ni asilimia 15 ya uwanja sh. 4,202,924.97, tiketi sh. 3,183,890, gharama za mechi sh. 2,521,754.98, Kamati ya Ligi sh. 2,521,754.98, Mfuko wa Maendeleo ya Mpira wa Miguu (FDF) sh. 1,260,877.49 na Chama cha Soka Dar es Salaam (DRFA) sh. 980,682.49.
Wakati huo huo; Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) kuwania ubingwa wa Tanzania Bara inaendelea Jumamosi (Machi 16, 2013) kwa mechi tatu zitakazochezwa katika miji ya Mwanza, Dar es Salaam na Manungu, Turiani mkoani Morogoro.
Toto Africans inayopigana kukwepa kurudi daraja la kwanza itakuwa mwenyeji wa Mgambo Shooting kutoka Tanga katika mechi itakayochezwa Uwanja wa CCM Kirumba.
Vinara wa ligi hiyo Yanga wataumana na Ruvu Shooting kwenye Uwanja wa Taifa wakati Uwanja wa Manungu utakuwa mwenyeji wa mechi ya Mtibwa Sugar na Coastal Union.