![]() |
Athumani Kilambo, enzi za uhai wake |
Na Boniface Wambura
SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF) limepokea kwa masikitiko kifo cha mchezaji wa zamani wa timu ya Yanga, Pan Africans na Taifa Stars, Athuman Kilambo 'Baba Watoto' kilichotokea jana (Machi 10 mwaka huu) jijini Dar es Salaam.
Msiba huo ni mkubwa kwa wadau wa mpira wa miguu kwani kwa nyakati tofauti Kilambo akiwa mchezaji, na baadaye kocha alitoa mchango mkubwa kwa timu mbalimbali alizochezea na kufundisha zikiwemo Pan Africans na Cargo, hivyo mchango wake tutaukumbuka daima.
TFF inatoa pole kwa familia ya marehemu Kilambo, Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) na klabu ya Pan Africans na kuwataka kuwa na subira na uvumilivu katika kipindi hiki kigumu cha msiba huo mzito.
Mazishi yanatarajiwa kufanyika leo (Machi 11 mwaka huu) katika makaburi ya Kisutu mkoani Dar es Salaam ambapo TFF imetoa ubani wa sh. 100,000. Mungu aiweke roho ya marehemu Kilambo mahali pema peponi. Amina.
Rais Jakaya Mrisho Kikwete akiweka udongo kwenye kaburi la mchezaji mkongwe wa Yanga na baadaye Kocha wa Pan Africa Marehemu Athumani Kilambo leo Machi 11, 2013 katika makaburi ya Kisutu jijini Dar es salaam. Marehemu Kilambo, ambaye alifariki jana usiku baada ya kuugua saratani ya koo kwa takriban miaka miwili,atakumbukwa kama beki imara wa Yanga na Kocha stadi wa Pan Africa ambaye aliiwezesha Klabu hiyo kutwaa ubingwa wa taifa mwaka 1982. Pia amefundisha nyota wengi wa
kandanda nchini wakiwemo kina Kassim Manara, Adolf Richard, Mohamed Mkweche, Juma Pondamali na wengineo wengi ambao walichezea Taifa Stars kutokea Yanga na Pan.
Rais Jakaya Mrisho Kikwete akiondoka baada ya kuongoza maelfu ya waombolezaji katika mazishi ya mchezaji mkongwe wa Yanga na baadaye Kocha wa Pan Africa Marehemu Athumani Kilambo leo Machi 11, 2013 katika makaburi ya Kisutu jijini Dar es salaam.
Rais Jakaya Mrisho Kikwete akisalimiana na Katibu Mkuu wa Yanga Lawrence Mwalusako katika mazishi ya mchezaji mkongwe wa Yanga na baadaye Kocha wa Pan Africa Marehemu Athumani Kilambo
leo Machi 11, 2013 katika makaburi ya Kisutu jijini Dar es salaam. wengine toka kushoto ni Naibu Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika. Ndugu Adam Malima, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Dar es salaam Mhe Ranmadhani Madabida na kulia ni Mwenyekiti wa Yanga Bw. Yusuf Manji.
PICHA NA IKULU