• HABARI MPYA

    Thursday, May 16, 2013

    MAMILIONEA SIMBA SC WAPELEKA MZIGO ZANZIBAR KUIMALIZA YANGA KESHOKUTWA

    Simba wakijifua Mao Dze Tung

    Na Prince Akbar, IMEWEKWA MEI 16, 2013 SAA 12:01 ASUBUHI
    UONGOZI na wadau kadhaa wa klabu ya Simba SC ya Dar es Salaam, likiwemo kundi la Friends of Simba leo unatarajiwa kutembelea kambi ya timu yao, iliyopo Zanzibar ikijiandaa na mchezo dhidi ya mahasimu wao wa jadi, Yanga SC keshokutwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
    Habari za ndani ambazo BIN ZUBEIRY imezipata kutoka Simba SC, zimesema kwamba uongozi na matajiri wa Friends Of Simba watatua kisiwani Unguja leo kufanya mazungumzo na wachezaji wao.
    Katika ziara hiyo, pamoja na wachezaji kupewa motisha ili kuwajenga kisaikolojia kuelekea mechi hiyo, pia watatangaziwa na ahadi nono iwapo watashinda Jumamosi.
    Jana uongozi wa Simba SC ulikuwa na kikao cha dharula kupeana taarifa muhimu na kupanga mikakati ya mwisho kuelekea mchezo huo.  
    Kikao hicho pia, kilitarajiwa kujadili suala la kubadilishwa kwa refa wa mchezo huo, ghafla kutoka Israel Nkongo hadi Martin Saanya.
    Simba SC imeweka kambi maeneo ya Mbweni, Zanzibar ikifanya mazoezi yake kwenye Uwanja wa Mao Dze Tung katikati ya mjini huo wa kitalii. 
    Juzi, Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba inayosimamia ushiriki wa timu katika mashindano pia, Zacharia Hans Poppe aliiambia BIN ZUBEIRY kwamba uongozi utakutana haraka kujadili mabadiliko hayo.
    Kapteni huyo wa zamani wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), alisema taarifa rasmi waliyokuwa nayo awali refa aliyepangwa kuchezesha mechi hiyo ni Israel Nkongo, lakini ajabu Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) juzi likamtaja refa tofauti, Martin Saanya.
    “Haiwezekani mabadiliko yafanyike ghafla, lazima kutakuwa kuna namna hapa. Tunakutana mara moja kujadili na kuchukua hatua, ikiwezekana tunaweza kugomea hiyo mechi, iwapo tutagundua kuna mchezo mchafu umeandaliwa dhidi yetu,”alisema Hans Poppe.
    Saanya kutoka Morogoro ndiye ameteuliwa kuchezesha pambano la watani wa jadi, Simba na Yanga SC la kufunga pazia la Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara Jumamosi kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
    Katika mchezo huo, unaosubiriwa kwa hamu na wapenzi wa soka nchini ili kujionea nani zaidi baina ya miamba hiyo, Saanya atasaidiwa na Samuel Mpenzu wa Arusha na Jesse Erasmo kutoka Morogoro, wakati refa akiba atakuwa ni Hashim Abdallah wa Dar es Salaam.
    Kamisaa wa mechi hiyo atakuwa Emmanuel Kavenga kutoka Mbeya wakati mtathmini wa waamuzi atakuwa ni Leslie Liunda wa Dar es Salaam.
    Mashabiki watakaotaka kwenda kushuhudia mpambano huo wa mahasimu wa jadi katika soka ya Tanzania, watalazimika kulipa Sh. 5,000, hicho kikiwa kiingilio cha chini zaidi katika sehemu ya viti vya Rangi ya Bluu. 
    Aidha, katika mchezo huo utakaoanza saa 10:00 jioni, viingilio vingine ‘nafuu kidogo’ vitakuwa ni Sh 7,000 kwa viti ya Rangi ya Kijani na Sh. 10,000 kwa viti vya Rangi ya Chungwa.
    Upande wa ‘wakubwa’, viingilio vitakuwa ni Sh. 15,000 kwa VIP C, Sh. 20,000 kwa VIP B na Sh. 30,000 kwa VIP A na tiketi zitaanza kuuzwa kesho.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: MAMILIONEA SIMBA SC WAPELEKA MZIGO ZANZIBAR KUIMALIZA YANGA KESHOKUTWA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top