![]() |
Kala Jeremiah kinara tuzo za Kili 2013 |
WASANII Kala Jeremiah na Ommy Dimpoz usiku wa jana waling’ara kwa upande wa muziki wa kizazi kwenye tuzo za Kili Music 2013.
Tuzo hizo zilizofanyika katika ukumbi wa Mlimani City, jijini Dar es Salaam ziliwashuhudia wasanii hao wakinyakua tuzo tatu kila mmoja.
Mbali na wasanii hao wa kizazi kipya, mwimbaji wa Mashujaa Band, Chaz Baba naye aliibuka na tuzo tatu wakati bendi yake ikijizolea jumla ya tuzo tano.
Kwa tuzo hizo tano, Mashujaa Band wamefikia rekodi iliyowekwa mwaka juzi na Twenty Percent aliyezoa tuzo tano akiwa ni msanii wa kwanza kufanya hivyo katika historia ya Kili Music Awards.
Kala Jeremiah alitwaa tuzo za wimbo bora wa Hip Hop, msanii bora wa Hip Hop na mtunzi bora wa mashairi Hip Hop.
Ommy Dimpoz aliibuka kidedea katika vipengele vya Video bora ya wimbo wa mwaka ‘Baadae’, wimbo bora wa Bongo Pop (Baadae) na wimbo bora wa kushirikishwa (Me and U ft. Vanessa Mdee).
Wakati Mashujaa Band ikipewa tuzo ya bendi bora, Chaz Baba alitwaa tuzo za Mwimbaji bora wa kiume – Bendi, mtunzi bora – Bendi na Wimbo bora wa bendi (Risasi Kidole) huku Ferguson akitwaa tuzo ya rapa bora wa bendi na hivyo kukamilisha tuzo tano zilizokwenda Mashujaa Band.
Kwa tuzo hizo, Chaz Baba anajiwekea rekodi ya nyimbo zake kupata tuzo kwa miaka mitatu mfululizo, mwaka jana (Dunia Daraja) na mwaka juzi (Mwana Dar es Salaam) zilichukua tuzo za nyimbo bora za dansi.
Watu wanaweza kuhoji tuzo ya bendi bora kwenda kwa Mashujaa lakini jibu lake liko wazi kabisa, unainyimaje hadhi hiyo bendi yenye tuzo 4 mkononi?
Kwa upande wa taarab ushindani ulikuwa ni mkubwa ambapo Jahazi Modern Taraab wameibuka na tuzo mbili sambamba na Mashauzi Classic huku Khadija Kopa akishinda tuzo ya Wimbo bora wa mwaka (Mjini Chuo Kikuu).
Jahazi wameibuka na tuzo ya Kundi bora la taarab na Msanii bora wa kiume wa taarab (Mzee Yussuf) wakati Mashauzi Classic wamepata Mtunzi bora wa mashairi ya taarab (Thabit Abdul) na Msanii bora wa kike wa taarab (Isha Mashauzi).
Luiza Mbutu aliitoa kimasomaso Twanga Pepeta kwa kupata tuzo ya Mwimbaji bora wa kike wa bendi, alistahili sana hakuna ubishi.
Baadhi ya wasanii waliobuka na tuzo moja moja ni pamoja na Ben Pol, Amin, Recho, Mrisho Mpoto, Ali Nipishe Amorosso, Man Water na Lady Jay Dee.
Jay Dee aliyepata tuzo ya Msanii bora wa kike, aliulipua ukumbi kwa makelele tangu jina lake lilipotajwa pamoja na washindani wanzake, shangwe zikazizima zaidi pale alipotajwa kuwa mshindi.
Gardner Habash (Mumewe Jay Dee) alipanda jukwaani kupokea tuzo hizo kwa vile mshindi yuko nje ya Dar es Salaam).
Tuzo ya heshima (iliyotukuka) kwa upande wa taasisi ilikwenda kwa The Kilimanjaro Band ‘Wana Njenje’ na kwa msanii ilikwenda kwa marehemu Salum Abdallah.
HABARI HII NI KWA HISANI YA SALUTI5