![]() |
Kikosi cha Yanga 2012 |
Na Prince Akbar
HATIMAYE pazia la michuano ya
Klabu Bingwa ya soka Afrika Mashariki na Kati, maarufu kama Kombe la Kagame,
linapenuliwa leo, kwa mchezo kati ya mabingwa watetezi, Yanga SC dhidi ya
Atletico ya Burundi kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam saa 10:00 jioni.
Mabingwa hao mara nne wa
michuano hiyo, wanaingia kwenye mchezo wa leo, wiki moja tu tangu wapate kocha
mpya, Mbelgiji Tom Saintfiet ambaye ni juzi tu alitaja wachezaji 20
atakaowatumia kwenye michuano hiyo.
Saintfiet aliwaacha kwenye kikosi chake wachezaji watatu
nyota na chipukizi, Omega Seme, Simon Msuva na Frank Damayo kwa sababu watakuwa
na majukumu ya kitaifa kwa muda mrefu.
Aidha, pia aliwaacha beki mkongwe na Nahodha Nsajigwa
Shadrack na kiungo Nurdin Bakari.
Saintfiet alisema kwamba Omega, Msuva na Damayo watakuwa na
timu ya taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 20, inayojiandaa na mechi ya
kuwania tiketi ya kucheza Fainali za Mataifa ya Afrika Julai 29 dhidi ya
Nigeria.
![]() |
Kocha Tom Saintfiet |
“Kwa mujibu wa kanuni
natakiwa kuwaachia wachezaji siku tano kabla ya mechi, na Jumamosi wanacheza na
Rwanda, Jumatatu wanarudiana na Rwanda, baada ya hapo watakuwa kwenye
maandalizi ya mechi na Nigeria, kwa hivyo sitakuwa nao hata kwenye Nusu
Fainali, kwa sababu hiyo nimeamua kuwaacha,”alisema.
Saintfiet alisema amemtema pia Nahodha wa klabu hiyo,
Nsajigwa Shadrack katika kikosi cha wachezaji 20, lakini amesema mchezaji huyo
ni muhimu na atakuwa naye kwenye Ligi Kuu.
Wachezaji aliowateua baada ya kushauriana na wasaidizi wake,
Freddy Felix Minziro na Mfaume Athumani kuwa ni; makipa Yaw Berko na Ally
Mustafa ‘Barthez’, mabeki Juma Abdul, David Luhende, Kelvin Yondan, Nadir
Haroub ‘Cannavaro’, Godfrey Taita, Ladislaus Mbogo, Oscar Joshua, Stefano
Mwasyika, viungo Athumani Iddi ‘Chuji’, Rashid Gumbo, Juma Seif ‘Kijiko’,
Haruna Niyonzima, Shamte Ally, Nizar Khalfan, Idrisa Assenga, Hamisi Kiiza na
washambuliaji Said Bahanuzi na Jerry Tegete.
Tangu aichukue timu, Saintfiet alicheza mechi moja ya
kirafiki dhidi ya JKT Ruvu na kushinda mabao 2-0. Katika mechi hiyo aliwasilisha
falsafa mpya ya uchezaji ya timu, ambayo ni soka ya utulivu zaidi mfano kama wa
kupaki basin a kushambulia kwa kushitukiza.
Mtakatifu Tom alisema falsafa yake ni ushindi iwe wa 1-0 au
5-0 na timu inayoshinda ni ile ambayo kwanza inajilinda vizuri.
Hivyo wana Yanga waende uwanjani na leo, wakitarajiwa
kuendelea kuona timu yao ikipaki basi na hawana budi kuuvmilia mfumo huo, kwa sababu
Tom anataka uzoeleke ili autumie kwa ufanisi baadaye kwenye michuano mikubwa ya
Afrika.
Tom alitolea mfano mafanikio ya Chelsea msimu uliopita
kutokana na mfumo huo, uliowawezesha kuving’oa vigogo wakiwemo waliokuwa
mabingwa watetezi Barcelona kabla ya kuifunga Barcelona kwenye fainali na
kubeba ndoo ya Ulaya.
Mchezo kati ya Yanga na Atlecito, utatanguliwa na mechi
baina ya mabingwa wa zamani wa michuano hiyo, APR ya Rwanda dhidi ya Waw
Salaam.
KIKOSI CHA YANGA
KAGAME;
Makipa; Yaw Berko
na Ally Mustafa ‘Barthez’
Mabeki; Juma
Abdul, David Luhende, Kelvin Yondan, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Godfrey Taita,
Ladislaus Mbogo, Oscar Joshua na Stefano Mwasyika
Viungo; Athumani
Iddi ‘Chuji’, Rashid Gumbo, Juma Seif ‘Kijiko’, Haruna Niyonzima, Shamte Ally,
Nizar Khalfan na Idrisa Assenga.
Washambuliaji;
Said Bahanuzi, Hamisi Kiiza na Jerry Tegete.
0 comments:
Post a Comment