![]() |
Mbuyu Tweite aka Rage |
USAJILI wa Ligi Kuu ya Bara msimu huu umekuwa na
msisimko wa aina yake, kutokana na ‘umafia’ waliofanyiana watani wa jadi, Simba
na Yanga- jambo ambalo limekumbushia baadhi ya matukio ya aina hiyo miaka
iliyopita, kama lile la Victor Costa kusaini Yanga na kujiunga nao, kisha kurejea
Simba na kuvaa jezi yenye jina la aliyempa fedha kusaini fomu Jangwani, Jamal
Malinzi, aliyekuwa Katibu wa Yanga wakati huo. Safari hii, Mbuyu Twite alipewa
dola za Kimarekani 30,000 na Ismail Aden Rage, Mwenyekiti wa Simba na kusaini,
lakini akasaini pia na kuhamia Yanga kutoka APR na alipofika Dar es Salaam
akavaa jezi yenye jina la Mtanzania huyo mwenye asili ya Kisomali. BIN
ZUBEIRY inakukumbusha baadhi ya vituko hivyo na kuamua kukipa ‘namba
moja’ kituo cha Rage.
YUSSUF
ISMAIL BANA
![]() |
Yussuf Bana kushoto akiichezea Yanga dhiai ya Simba. Kulia ni Zamoyoni Mogella na nyuma ni Muhiddin Cheupe. |
AKIWA mchezaji wa Pamba ya Mwanza mwanzoni mwa miaka
ya 1980, beki Yussuf Ismail Bana alisaini Simba katika fomu za usajili akitumia
jina la Yussuf Ismail. Lakini baadaye Yanga wakamfuata na kumrubuni asaini
kwao. Akasaini Jangwani na kutumia jina la Yussuf Bana na Chama cha Soka
Tanzania (FAT, sasa TFF) chini ya Mwenyekiti wake wa enzi hizo, Said Hamad El
Maamry wakamuidhinisha kuchezea Yanga, lilikuwa bonge la sinema.
CHARLES
BONIFACE MKWASA
Charles Boniface Mkwasa |
Akiwa mchezaji mpya kwenye kikosi cha Yanga
aliyesajiliwa kutoka Tumbaku ya Morogoro, mwanzoni mwa miaka ya 1980, Simba
ilimfuata na kumrubuni ahamie kwao. Kiungo Charles Boniface Mkwasa, akakubali
na kusaini Simba SC kwa jina la Charles Boniface alilokuwa pia akitumia Yanga
na tangu Tumbaku. Lakini Yanga wakamfuata na kumshawishi abaki, na baada ya
kukubaliana naye, akasaini kuendelea kuichezea Yanga, safari hii akitumia jina
la Charles Boniface Mkwasa. Lakini hii mbele ya FAT ya El Maamry ilidunda na
Mkwasa alifungiwa msimu mzima kabla ya kumaliza adhabu yake na kuendelea
kucheza Jangwani.
EPHRAIM
MAKOYE MAHALA:
Akiwa mchezaji mpya kwenye kikosi cha Yanga
aliyesajiliwa kutoka Kagera Stars mwaka 2000 (sasa Kagera Sugar), Simba SC
walimfuata na kumrubuni asaini kwao. Makoye, ambaye wakati huo alikuwa mwanafunzi
wa kidato cha pili katika sekondari ya Makongo, alichukua fedha za Simba
akasiani. Hata hivyo, siku hiyo hiyo Yanga walimnasa na kumchukua hadi kwa
viongozi wa Simba kurudisha fedha alizochukua aendelee kuchezea Yanga. Simba
waligoma kuchukua fedha na kwa sababu wakati huo FAT ilikuwa haitambui mikataba
ya klabu na mchezaji zaidi ya fomu za usajili, ambazo zilikuwa hazijatoka,
Makoye aliendelea kuchezea Yanga, ingawa baadaye alichezea Simba alipotemwa
Yanga.
VICTOR
COSTA
![]() |
Victor Costa aka Malinzi |
Akiwa mchezaji mpya aliyesajiliwa kutoka Mtibwa
Sugar kwenye kikosi cha Simba mwaka 2005, Yanga walimfuata beki huyo na
kumrubuni asaini kwao. Costa alisaini na kwenda kujiunga na wenzake kambini
Zanzibar ambako timu ilikuwa inacheza Kombe la Mapinduzi. Lakini aliporejea tu
Dar es Salaam, Simba wakamteka na kumpeleka mazoezini kwao, akiwa amevaa jezi
iliyoandikwa jina la Katibu Mkuu wa Yanga wakati huo, Jamal Malinzi. Costa
hakurudisha fedha za Yanga na akaidhinishwa kuendelea kuchezea timu yake.
MBUYU
TWITE:
Akiwa amekwishasaini mkataba wa kuichezea Simba SC
kutoka APR ya Rwanda, Yanga wakamzungukia na kumsainisha na beki huyo akaamua
kurudisha fedha za Simba. Tukio hilo lilimtoa machozi Mwenyekiti wa Simba SC,
Alhaj Ismail Aden Rage alipokuwa akizungumza na Waandishi wa Habari mjini
Dodoma kulaani kitendo hicho. Tukio hilo siyo tu linapanda kileleni katika
vituko vya usajili wa Ligi Kuu ya Bara kwa sababu ndilo la sasa, bali pia kwa
kitendo cha ‘mtu mzima’ Rage kumwaga machozi mbele ya kamera za Televisheni
akisikitikia changa la macho alilopigwa na mchezaji huyo.
![]() |
Rage akilia huku akiwa amekumbatiwa vizuri na kubembelezwa na Profesa Philemon Sarungi. Hapa ilikuwa kwenye msiba wa Patrick Mafisango. |
HITIMISHO:
Yapo
matukio mengine ya wachezaji kuchukua fedha timu nyingine na kubaki timu zao
kama Amri Said mwaka 2002, lakini hayana msisimko kwa sababu hawakuwahi
kujiunga na timu mpya- haya matano ndio yalikwishatengeneza picha fulani,
kwamba mchezaji fulani sasa ni wa timu fulani, lakini baadaye akageuza kibao.
0 comments:
Post a Comment