• HABARI MPYA

    Monday, December 03, 2012

    EL MERREIKH YAVAMIA ANGA ZA SIMBA, CHELEWA CHELEWA UTAKUTA MWALI SI WAKO

    Umony akiwa na ramadhan Sarpei, mmoja wa viongozi wa timu ya Sudan mjini hapa 

    Na Mahmoud Zubeiry, Kampala
    MSHAMBULIAJI wa Uganda, Brian Umony amekwishasema yuko tayari kujiunga na klabu ya Simba ya Dar es Salaam, lakini kabla Wekundu hao wa Msimbazi hawajachukua hatua yoyote, El Merreikh ya Sudan imetuma mwakilishi wake hapa azungumze na mchezaji huyo.
    Habari ambazo BIN ZUBEIRY imezipata mjini hapa zimesema kwamba, Merreikh inayosuka upya kikosi chake baada ya kukosa ubingwa wa Sudan, imetuma mwakilishi wake hapa afanye mazungumzo na Umony, aliyekoswakoswa kidogo tu na Simba mwaka 2009, alipokuwa KCC ya hapa.
    Mwandishi mmoja wa habari wa Sudan, ameiambia BIN ZUBEIRY  jana katika hoteli ya Silver Springs mjini hapa kwamba, tayari mwakilishi huyo wa Merreikh yuko hapa kwa kazi hiyo.
    Aidha, Mwandishi huyo amesema mwakilishi huyo wa Merreikh atatazama vipaji zaidi kuanzia hatua ya Robo Fainali kwa ajili ya kupendekeza wachezaji wapya wa kusajiliwa na klabu hiyo. 
    Mwandishi huyo alisema tayari Merreikh pia imekubaliana biashara na Yanga juu ya kiungo Haruna Niyonzima, Nahodha wa Rwanda katika Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati, CECAFA Tusker Challenge. 
    Mwishoni mwa wiki, akizungumza na BIN ZUBEIRY mjini hapa baada ya kuiongoza Uganda kuifunga Sudan Kusini maao 4-0 katika mechi ya mwisho ya Kundi A, Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na kati, CECAFA Tusker Challenge, Umony alisema Simba kama wanamtaka wamfuate haraka wamalizane.
    Brian amerejea nyumbani Uganda na kujiunga na Express baada ya kumaliza mkataba wake, Becamex Binh Duong F.C. ya Vietnam.
    Mwaka 2009, baada ya Simba kuzidiwa kete na SuperSport United ya Afrika Kusini, ikamsajili Emmanuel Okwi aliyekuwa SC Villa wakati huo.
    Umony aliichezea Supersport United hadi 2010 alipohamia University of Pretoria ya Afrika Kusini pia hadi mwaka 2011 alipohamia Portland Timbers ya Marekani kwa mkopo na mwaka huu akatua Becamex Binh Duong F.C. Brian anang’ara katika Kombe la Challenge, hadi sasa ana mabao matatu.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: EL MERREIKH YAVAMIA ANGA ZA SIMBA, CHELEWA CHELEWA UTAKUTA MWALI SI WAKO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top