• HABARI MPYA

    Monday, December 03, 2012

    JOHN BOCCO ATABIRIWA MAISHA SUPERSPORT

    John Bocco 'Adebayor'

    Na Mahmoud Zubeiry, Kampala
    JOHN Raphael Bocco amezidi kuwa gumzo kubwa katika mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati, CECAFA Tusker Challenge yanayoendelea mjini hapa.
    Wapiga picha wa Televisheni ya SuperSport wanamsifia sana Bocco na wanasema kuna uwezekano sasa klabu ya SuperSport United ya Afrika Kusini ikamgeukia tena.
    “Amefunga katika kila mechi aliyocheza, huyu ni mfungaji wa uhakika, ni mshambuliaji mwenye nguvu, kasi na uwezo wa kumiliki mpira, anapiga sana vichwa, ana kiwango cha kucheza PSL (Ligi Kuu ya Afrika Kusini),”alisema mmoja wa wapiga picha hao jana.
    Jamaa wa SuperSport wanemuhesabia Bocco hata bao ambalo alifunga kwenye mechi dhidi ya Burundi lakini refa akakataa, ndiyo maana wanasema amefunga katika kila mechi.
    Hadi sasa, rasmi Bocco ana mabao manne, ukiondoa hilo ambalo refa ameminya. Alifunga mabao mawili katika mechi dhidi ya Sudan na akarudia kufunga idadi hiyo dhidi ya Somalia.
    Bocco anazidiwa bao moja tu na Mrisho Khalfan Ngassa, aliyefunga matano, lakini yote katika mechi moja dhidi ya Somalia.    
    Bocco maarufu kwa jina la utani ‘Adebayor’ anayechezea Azam FC ya Dar es Salaam, alifanya vizuri katika majaribio yake kwenye klabu ya SuperSport United ya Afrika Kusini Agosti mwaka huu, lakini klabu hiyo ikashindwa kufika dau la kumng’oa Chamazi.
    SuperSport ilivutiwa na soka ya Bocco, katika michuano ya Klabu Bingwa ya soka Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame, Julai mwaka huu mjini Dar es Salaam hivyo kumuita kwa majaribio, ambayo alifuzu.
    Katika Kombe la Kagame, Bocco alifunga mabao matano na kushika nafasi ya tatu katika wafungaji bora, nyuma ya Hamisi Kiiza aliyefungana na Tadi Etikiama kwa mabao sita, na Said Bahanuzi wa Yanga, aliyeibuka mfungaji bora kwa mabao yake saba.
    Lakini Bocco pia alikuwa mfungaji bora wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara msimu uliopita, kwa mabao yake 18 akiwapiku hadi washambuliaji wa kigeni waliocheza ligi hiyo msimu huo, Emmanuel Okwi, Kenneth Asamoah, Davies Mwape na Dalington Enyiana.
    Tangu aipandishe Ligi Kuu Azam FC msimu wa 2008/2009 kwa mabao yake, akiibuka mfungaji bora wa Ligi Daraja la Kwanza, Bocco amekuwa akiingia kwenye mbio za kuwania kiatu cha dhahabu cha Ligi Kuu, msimu wa kwanza akizidiwa na Boniphace Ambani aliyekuwa Yanga, msimu wa pili Mussa Mgosi aliyekuwa Simba na msimu wa tatu na Mrisho Ngassa, kabla ya msimu uliopita kutimiza ndoto zake za kuwa mfungaji bora wa ligi hiyo.
    Iwapo atanunuliwa na SuperSport, Bocco ataweka historia ya kuwa mchezaji wa pili wa Tanzania kuchezea klabu hiyo, baada ya Suleiman Matola 2005 hadi 2007, akitokea Simba SC.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: JOHN BOCCO ATABIRIWA MAISHA SUPERSPORT Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top