• HABARI MPYA

    Monday, December 03, 2012

    KILA LA HERI STARS NA HEROES ROBO FAINALI TUSKER CHALLENGE LEO, MAANA NI SHUGHULI PEVU

    Kikosi cha Tanzania Bara

    Na Mahmoud Zubeiry, Kampala
    DUA njema za Watanzania kwa ujumla, leo zitaelekezwa mjini hapa, wakati timu mbili kutoka Jamhuri ya Muungano wetu, Bara na Zanzibar zitakapokuwa zikipigana katika Robo Fainali ya Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati, CECAFA Tusker Challenge kwenye Uwanja wa Lugogo.
    Bara, maarufu Kilimanjaro Stars watakuwa wa kwanza kutupa kete yao leo kuanzia saa 8:00 mchana kwa kumenyana na Rwanda, kwa jina la utani Amavubi, yaani Nyigu, wakati Zanzibar Heroes watasubiri hadi saa 10:00 kukipiga na Burundi, Int’hamba Murugamba, yaani Mbayuwayu.
    Robo Fainali nyingine zinatarajiwa kuchezwa kesho kwenye Uwanja wa Mandela, Namboole, Kenya ikianza na Malawi saa 10:00 jioni kabla wenyeji Uganda kumenyana na Ethiopia saa 1:00 usiku.
    Zanzibar wakiomba dua kabla ya mechi na Rwanda waliyoshinda 2-1
    Mchezo kati ya Burundi na Zanzibar unatarajiwa kuwa mkali na wa kusisimua, na zaidi Mashujaa wa Visiwani wanatakiwa kumchunga sana Nahodha wa Mbayuwayu, Suleiman Ndikumana kwa sababu ndiye amekuwa akiiongoza vema timu yake.
    Ndikumana amekuwa akihaha Uwanja wa mzima, akicheza kwa kuwahamasisha wadogo zake na hadi sasa ndiye Nahodha bora zaidi katika mashindano haya.
    Hazina ya Zanzibar ni safu nzuri ya kiungo inayoongozwa na Suleiman Kassim Selembe na Khamis Mcha ‘Vialli ’bila kusahau ukuta imara chini ya mabeki Nadir Haroub ‘Cannavaro’ na Aggrey Morris na hata kipa hodari, Mwadini Ally.
    Safu ya ushambuliaji leo hakuna shaka itaongozwa na Jaku Juma, mkali wa mabao katika Ligi Kuu ya Zanzibar na Seif Abdallah, nyota wa Ruvu Shooting ya Bara aliye mbioni kuhamia Azam FC. 
    Mambo zaidi ni Rwanda na Bara; jezi namba nane (8) leo zinatarajiwa kuwa kila kitu. Jezi hiyo kwa upande wa Rwanda anavaa Haruna Hakizimana Niyonzima na Bara Mrisho Khalfan Ngassa.
    Wawili hawa ndio wamekuwa kama roho ya timu zao katika mashindano haya na leo wanatarajiwa kuendelea kubeba jukumu hilo.
    Ngassa anacheza wingi ya kushoto kwa sasa kwenye kikosi cha Bara, wakati Niyonzima anapangwa wingi ya kulia katika kikosi cha Rwanda. Niyonzima huwa anabadilika na kuingia ndani na wakati mwingine upande wa pili na kwa ujumla huhaha Uwanja mzima, vivyo hivyo kwa Ngassa.
    Dadi Birori au Taddy Etikiama kwa jina lingine atasimama mbele bila kuongoza mashambulizi kwa Rwanda na langoni atakuwapo kipa mgumu kufungika, Jean Claude Ndoli.
    Kocha wa Bara, Mdenmark Kim Poulsen anacheza na mshambuliaji mmoja, John Bocco, lakini anatumia mawinga wenye kushambulia mno- Ngassa na Simon Msuva, wakati Micho pia hutumia washambuliaji wawili na hana viungo wenye kasi sana, ila mafundi.
    Mabeki wa pembeni wa Rwanda wanapitika kwa urahisi na leo Ngassa na Msuva washindwe wenyewe tu. Beki ya kati ya Rwanda ni ugonjwa wa moyo, maana yake John Bocco leo ni umakini wake tu.
    Kwa ujumla, Bara ina nafasi kubwa ya kuitoa Rwanda, tena kwa kuipa kipigo kitakatifu tu kama watatumia vyema nafasi zao.
    Mwinyi Kazimoto amepona na bila shaka atakuwa mmoja wa viungo watatu leo, wengine Frank Domayo na Amri Kiemba maana yake, kwenye benchi watakuwapo Athumani Iddi ‘Chuji’ na Shaaban Nditi.
    Piga, ua Juma Kaseja atasimama langoni, kulia Erasto Nyoni na kushoto uzoefu utambeba Amir Maftah ingawa Issa Rashid anakuja vizuri, wakati katikati Kevin Yondan atacheza pacha na Shomary Kapombe.
    Hii ni mara ya pili ndani ya miaka mitatu Bara kukutana na Rwanda katika hatua hii na mara ya mwisho ilikuwa Desemba 8, mwaka 2010 wakati bao pekee la mkwaju wa penalti la aliyekuwa Nahodha wa Stars, Nsajigwa Joel Shadrack Mwandemele dakika ya 61 lilipoipa Bara ushindi wa 1-0 na kutinga Nusu Fainali hadi kutwaa ubingwa Dar es Salaam.
    Lakini mwaka jana pia timu hizo zilikutana Dar es Salaam katika michuano hii, Kundi A na Rwanda iliilaza Bara 1-0 Novemba 26, katika michuano ambayo wenyeji waliboronga vibaya na kutolewa mapema.
    Tangu mwaka 2001, timu hizi zimekutana mara tisa katika Challenge na Rwanda imeshinda mechi sita, wakati Bara imeshinda mechi tatu tu. Idadi kubwa ya mabao Tanzania kuifunga Rwanda ni 3-0, wakati Amavubi wamewahi kuichapa Bara 5-1.
    Pamoja na yote, Robo Fainali za leo ni nzuri- zaidi Watanzania kwa ujumla Bara na Visiwani, wanatakiwa kuziombea dua njema timu zao zivuke hatua hii, kwani katika soka lolote hutokea.  Mungu ibariki Bara na Zanzibar, ibariki Tanzania. Amin.

    REKODI YA TANZANIA NA RWANDA CHALLENGE:
    Desemba 17, 2001; Nusu Fainali Rwanda
    Tanzania 1-2 Rwanda B
    Desemba 11, 2002; Nusu Fainali Mwanza
    Tanzania 3-0 Rwanda
    Desemba 19, 2004; Kundi A Ethiopia
    Tanzania 1-5 Rwanda
    Desemba 6, 2005; Kundi A Rwanda
    Tanzania 1-3 Rwanda
    Desemba 5, 2006; Robo Fainali Ethiopia
    Tanzania 1-2 Rwanda
    Januari 7, 2009; Kundi A Uganda
    Tanzania 2-0 Rwanda
    Desemba 10, 2009: Nusu Fainali Kenya
    Tanzania 1-2 Rwanda
    Desemba 8, 2010; Robo Fainali Dar es Salaam
    Tanzania 1– 0 Rwanda
    Novemba 26, 2011; Kundi A, Dar es Salaam
    Tanzania 0 – 1 Rwanda

    WAFUNGAJI CECAFA TUSKER CHALLENGE 2012
    Mrisho Ngassa               Tanzania  5
    John Bocco                    Tanzania  4
    Suleiman Ndikumana     Burundi    3 (1 penalti)
    Brian Umony                  Uganda    3
    Chris Nduwarugira         Burundi    3
    Khamis Mcha                 Zanzibar   2
    David Ochieng               Kenya       2
    Clifton Miheso                Kenya       2
    Dadi Birori                      Rwanda    2
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: KILA LA HERI STARS NA HEROES ROBO FAINALI TUSKER CHALLENGE LEO, MAANA NI SHUGHULI PEVU Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top