KLABU ya West Brom imejipatia ushindi wake wa kwanza kwenye Uwanja wa Anfield tangu mwaka 1967 wakati ilipowalaza wenyeji Liverpool 1-0.
Wekundu wa Anfiled leo hawakuwa na bahati, kwani waliikosa mabao ya wazi huwezi kuamini, Jordan Henderson na Dirk Kuyt wakikosa mabao ya wazi zaidi, tena wazi sana.
Hiyo iliwagharimu kipindi cha pili baada ya makosa ya Glen Johnson kutumiwa vizuri na Peter Odemwingie aliyemtungua kipa Pepe Reina dakika ya 75.
Liverpool sasa imeshinda mechi tano tu nyumbani katika mechi zao 17 zilizopita za ligi msimu huu.
Kwa ujumla, leo Wekundu hao walipiga mashuti 28 langoni kwa wapinzani wao waliopiga tisa tu, na walipiga kona 15 dhidi ya tatu za The Baggies.
Ushindi huo unaipandisha Albion hadi nafasi ya 10 kwenye msimamo wa Ligi Kuu, nafasi mbili na pointi moja juu ya Liverpool, ambayo imevuna pointi saba tu katika mechi zao 10 zilizopita.