• HABARI MPYA

    Thursday, May 03, 2012

    ROBBEN AJITIA KITANZI BAYERN HADI JAKAYA AACHIE NCHI


    FC Bayern München, Arjen Robben
    Getty Images
    KLABU ya Bayern Munich ya Ujerumani, imetangaza kwamba Arjen Robben amesaini mkataba mpya ambao utamuweka Allianz Arena hadi mwishoni mwa msimu wa 2015, wakati Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete atakapomaliza muda wake wa kuiongoza nchi.

    Mwanasoka huyo wa kimataifa wa Uholanzi, mkataba wake wa awali unatarajiwa kumalizika Juni 2013 na winga huyo amekuwa akihusishwa na mpango wa kuhamia klabu kadhaa kubwa Ulaya katika miezi ya karibuni.

    Baada ya habari kwamba kumekuwa na mazungumzo ya mkataba mpya, hatimaye Robben amejitia kitanzi The Bavarian kwa miaka miwili zaidi.

    "Wakati wote nimekuwa nikisema kwamba nina furaha Munich nikiwa na FC Bayern," alisema Mholanzi huyo katika tovuti ya klabu yake. "Kwa msimu huu, nilipenda wazo la kusaini mkataba mpya mapema. Bayern ni kama familia kwangu. Watoto wangu wawili kati ya watatu wamezaliwa Munich na mimi na familia yangu tunajisikia tupo nyumbani hapa

    "Pia, katika akili ya kimichezo, kurefushwa huku kwa mkataba ni uamuzi sahihi kwangu. Tuna timu nzuri na nina uhakika kwamba tutafurahia mafanikio zaidi katika miaka ijayo."

    Ofisa Mtendaji Mkuu wa Bayern, Karl-Heinz Rummenigge amesema amefurahia kwa Robben kujitia kitanzi kwa vigogo hao wa Bundesliga.

    "Tuna furaha sana kumtia kitanzi Arjen Robben hadi 2015," alisema mwanasoka huyo wa zamani wa kimataifa wa Ujerumani Magharibi.

    "Arjen ni muhimu sana kwa Bayern na anatuhakikishia mafanikio katika mustakabali wa klabu."

    Robben, ambaye alifunga bao la penalti muhimu kwa The Bavarians katika Nusu Fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, wakiitoa Real Madrid, alijiunga na Bayern akitokea Los Blancos (Real Madrid) mwaka 2009.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: ROBBEN AJITIA KITANZI BAYERN HADI JAKAYA AACHIE NCHI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top