• HABARI MPYA

    Sunday, May 06, 2012

    WAZEE WA YANGA WATAHUKUMIWA KWA KAULI ZAO


    Mwenyekiti wa Yanga, Wakili lloyd Baharagu Nchunga kushoto.

    KWA sasa kuna watu ambao wako msituni, wanatumia baadhi ya wanachama wa Yanga na Waandishi wa Habari kuleta vurugu katika klabu ya Yanga, lengo lao kuuangusha uongozi uliopo madarakani.
    Watu hao wanajulikana na silaha yao ni fedha- inawapa jeuri ya kutaka kuivuruga Yanga.
    Hadi kufikia hapa, Yanga inakosa hata nafasi ya pili katika Ligi Kuu, wao wamechangia kwa kiasi kikubwa. Kujiuzulu kwa Seif Ahmad ‘Magari’ na Abdallah Bin Kleb katika Kamati ya Utendaji, inasemekana pia kumetokana na ushawishi wao.
    Hali hiyo imewakera hadi wachezaji wa Yanga, kufikia kuzungumza kwenye vyombo vya habari juzi kuamkia jana.
    Wachezaji wa Yanga walikaririwa na gazeti la Mwananchi juzi wakisema wanakerwa na mgogoro unaoendelea ndani ya klabu hiyo.
    Kwa wiki nzima sasa, uongozi wa Yanga umeelemewa na shinikizo kutoka kwa wazee wa klabu hiyo waliodhamiria kuchukua usimamizi wa timu kwa kile walichokibainisha kuwa ni uongozi mbovu uliosababisha timu kufanya vibaya.
    Wachezaji walisema pamoja na kutosimama upande wowote kuunga mkono pande zinazolumbana, bado wanaamini madhara ya mgogoro huo yanawagusa hata wao.
    Walisema pamoja na wazee wa klabu hiyo kusitisha uamuzi wao wa awali kutaka kuichukua timu, bado haimaanishi kwamba mgogoro umefika tamati na kuzitaka pande zote mbili kuafikiana haraka hasa kipindi hiki kuelekea mechi dhidi ya Simba.
    Akielezea hali hiyo ya Yanga, kipa Shaaban Kado alisema, "Mgogoro siyo mzuri ukizingatia tupo kwenye kipindi kigumu na mechi ya watani zetu, tungeomba wazee wetu, viongozi wote kwa pamoja tushirikiane, tushikamane,  tuhakikishe tunashinda mechi yetu ya Jumapili.
    "Itakuwa mbaya zaidi kama tutapoteza tena mechi yetu dhidi ya Simba, siku zote naamini kidole kimoja hakivunji chawa. Sitegemei kwenye mgogoro timu inaweza kufanya vizuri, ningependa hizi kelele za mgogoro zifike tamati," alisema Kado.
    Kado alisema, yeye na wachezaji wenzake wasingependa kuwa sehemu ya migogoro kwa sababu wameajiriwa kucheza soka na mambo ya utawala yana watu wake wa kusimamia.
    "Kelele hizo na sisi tuanazisikia na kuzipuuza kwa sababu hazituhusu na hatupaswi kuziingilia kwa sababu siyo zilizotuleta Yanga.
    "Kazi iliyotuleta Yanga ni moja tu .... kucheza soka, wanaolumbana wana mambo yao wanataka, sisi hayatuhusu," alisema mchezaji wa kiungo wa Yanga ambaye hakutaka jina lake kuandikwa gazetini.
    Alisema jambo la msingi, yeye na wachezaji wenzake hawaungi mkono upande wowote, ila wanaangalia kinachowafanya kulipwa mishahara Yanga.
    Aidha, Shamte Ally akieleza kukerwa na kinachoendelea Yanga alisema: "Sio muda muafaka kulumbana na kuwekeana bifu. Viongozi na wazee wetu wanatakiwa kujenga mshikamano tunaelekea mechi ya lawama dhidi ya Simba."
    Ally alisema baada ya kupoteza ubingwa msimu huu, wamebaki na fursa moja ya kulinda heshima yao, nayo ni kuifunga Simba kwenye mchezo wa Jumamosi wiki hii.
    Alisema kinachotakiwa sasa ni kuweka pembeni tofauti zilizopo na kujiandaa vizuri na mchezo dhidi ya Simba. "Tunapaswa kulinda heshima yetu kwa kuifunga Simba baada ya kupoteza ubingwa," alisema.
    Kwa upande wake, Hamisi Kiiza alisema kuwa pamoja na kuzingatia zaidi kilichompeleka Yanga, lakini hafurahishwi na hali ilivyo. "Huu ni mgogoro wa kiutawala, mimi sina cha kusema zaidi ya kufanya kilichoniweka Yanga," alisema Kiiza.
    "Mimi nasikia kwenye vyombo vya habari taarifa za mgogoro, nimetumia muda mwingi kuwatuliza wenzangu kutojihusisha na hali iliyopo ila tuweke mkazo kwenye mchezo wa mwisho," alisema Kiiza.
    Kwa upande wake, Rashid Gumbo alisema, "Mimi sipendi kabisa kusikia mambo hayo, kwanza hayanihusu tuwaachie wenyewe, sisi tunataka kucheza soka malumbano siyo kazi yetu."
    Kwa upande mwingine, Mwenyekiti wa Yanga, Llyod Nchunga amesema wachezaji wote wamelipwa mishahara na posho zao walizostahili baada ya kushinda mechi za Ligi Kuu.
    "Hakuna malimbikizo ya mishahara, tumeshawalipa posho ya michezo yote walioshinda kasoro ile mitatu tu ambayo walipoteza, sasa hivi tunawajenga wachezaji wetu kisaikolojia wajue wao ni mabingwa wa Kombe la Kagame, wasisikitike kupoteza nafasi ya kutetea ubingwa," alisema Nchunga.
    Akizungumzia maandalizi ya pambano hilo, Kocha Fred Minziro alisema, "Wachezaji wote wako fiti, nachokifanya hivi sasa ni kuwajenga kisaikolojia na nimeshawambia kuwa mgogoro wa viongozi hautuhusu, sisi ni waajiriwa tu Yanga, viongozi watajua wenyewe watamalizaje mgogoro wao.
    Kuhusu mchezo huo, Minziro alisema,"Simba wanaingia uwanjani kusaka ubingwa, sisi tutacheza kulinda heshima yetu."
    Wakati kambini Yanga Bagamoyo hali na msimamo ukiwa ni huo, Dar es Salaam pilika zimeendelea- na jana wanachama wakiongozwa na mwanachama maarufu wa migogoro, Bakili Makele walikuwa kwenye vyombo vya habari.
    Nashangaa kuona bado kuna vyombo vya habari Tanzania vinatoa nafasi vyombo vyao kuwa uwanja wa malumbano na migogoro- sitaki kuamini kama huu ndio wajibu wa vyombo vya habari.
    Bakili Makele tangu namjua Yanga- umaarufu wake umetokana na migogoro na siku zote huibuka wakati wa migogoro.
    Zaidi ya hapo, unaweza kujiuliza huyu mtu yupo kweli? Wengine niliowaona, ni watu ambao tangu kwenye uchaguzi hawamuungi mkono Nchunga- sasa unategemea nini kutoka kwa hao watu?
    Hii sasa inafanya watu tuamini kwamba, Nchunga anahujumiwa, anasalitiwa ili Yanga ifanye vibaya, iyumbe naye haonekani hafai.
    Nasikitika watu hawa ni wageni sana Yanga na hawaijui historia ya klabu hiyo. Wana Yanga ni wazito kuamua, kwa sababu wana subira, ila yakiwafika kooni huwa ni wati tofauti sana.
    Huwa hawaangalii sura wala hadhi ya mtu.
    Mungu amrehemu, Abbas Gulamali, alimwaga fedha nyingi Yanga na akakarabati hadi jengo, kwa ujumla alifanya makubwa na ya kihistoria- lakini alipotofautiana kimisimamo na wenye Yanga yao, yalimgeukia.
    Huwezi kuuzungumzia ubingwa wa Yanga Afrika Mashariki na Kati 1993 na 1999 mjini Kampala, Uganda bila kumtaja Gulamali, ambaye alifikia kuimbwa na marehemu Pepe Kalle, kama rais wa Yanga na wenye timu yao walikaa kimya tu.
    Hakuwa rais wa Yanga, alikuwa mfadhili tu- na wakati huo Katiba ilikuwa haina cheo cha urais, ila watu walisema kwa anayowafanyia klabuni, ajiite vyovyote atakavyo wao wanataka furaha.
    Ila, mwisho wa siku ilikuwaje? Wenye kuijua Yanga watakuwa wanakumbuka.
    Reginald Mengi alikuwa ana heshima kubwa Yanga na akajitolea kusuluhisha mgogoro wa Yanga Asili na Yanga Kampuni.
    Awali, walimsikiliza na kwenda naye sawa, lakini alipotofautiana na wenye Yanga yao, yalimgeukia pale Star Light Cinema na hadi leo hajakanyaga tena kwenye shughuli ya Yanga.
    Nani asiyejua Mengi ni Yanga mzuri na milionea ambaye leo hii akiangukiwa klabu itakuwa baab kubwa? Tunakubali udhaifu wa uongozi ndani ya klabu, lakini suluhisho lake si kuleta vurugu klabuni.
    Kama watu wana vita binafsi, wapambane wao kwa wao bila kuiumiza Yanga. Lloyd Nchunga ni mwana Yanga mmoja tu kati ya mamilioni. Haiwezekani mtu apambane na Mwenyekiti wa Yanga kwa kuinyima Yanga ubingwa- hata nafasi ya pili na bado anataka timu ifungwe na Simba. Huyu si mwana Yanga- ni mnafiki. Ni mbinafsi- na maana yake anataka hata kuwapo Yanga kwa maslahi yake binfasi.
    Yanga wa kisasa wanataka umoja, mshikamano na mafanikio ya uwanjani. Yanga wa kupewa noti nyekundu walete malumbano na migogoro isiyo na tija klabuni, hao ni wa kuwaangalia mara  mbili. 
    Wewe una umgovi na Nchunga au Yanga, hebu jiulize? Kwa nini uwanyime raha wana Yanga mamilioni kwa mamilioni kwa fedha zako?
    Namalizia kwa kuwaambia Wazee wa Yanga, watumie fursa yao kuweka mambo sawa klabu ni si kuparaganyisha.
    Mzee wa Yanga anaposema hata Yanga ikiifunga Simba, Nchunga ataondoka tu, huyu anamaanisha nini? Maana yake wana Yanga wajiandae kuugulia maumivu ya kipigo cha Simba leo- ili azma ya kumng’oa Nchunga itimie?

    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: WAZEE WA YANGA WATAHUKUMIWA KWA KAULI ZAO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top