![]() |
Ngassa |
Na Mahmoud Zubeiry
AZAM FC imeamua kusitisha mpango wa kuwataka kusitisha
kumtoa kwa mkopo kwa Mrisho Khalfan Ngassa Simba SC na kumuacha aendelee na
maisha mapya Msimbazi, lakini itaendelea kupambana kuhakikisha inapata haki
yake juu ya kiungo wake, Ramadhan Chombo ‘Redondo’.
“Huo mpango umekufa, tumegundua haiwezekani, lakini
tumejifunza sana, hatuwezi kurudia kosa,”alisema kiongozi mmoja wa Azam FC.
Azam FC tangu juzi usiku ilikuwa inafikiria kusitisha mpango
wa kumtoa kwa mkopo katika klabu ya Simba, kiungo wake huyo, Ngassa, kufuatia
kitendo cha Wekundu hao wa Msimbazi, kumsajili ‘kibabe’ kiungo wao mwingine,
Ramadhan Chombo ‘Redondo’.
“Tunapitia sheria na kanuni za usajili wa mkopo kuona kama
tunaweza kufanya hivyo, tukigundua tunaweza, tunawapokonya mchezaji wetu, si
watu waungwana hawa, na hatutahitaji tena uhusiano wa aina yoyote na wao, labda
klabu ipate viongozi wengine, si hawa wa sasa,”alisema juzi kiongozi mmoja wa
Azam, alipozungumza na BIN ZUBEIRY.
Azam walimtoa kwa mkopo Ngassa wiki iliyopita, baada ya
kukerwa na kitendo cha mchezaji huyo kubusu jezi ya timu yake ya zamani, Yanga,
katika Nusu Fainali ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame,
dhidi ya AS Vita ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
Alifanya hivyo, baada ya kufunga bao la ushindi akitokea
benchi na kuiwezesha Azam kutinga fainali ya michuano hiyo, ambako walifungwa
na Yanga 2-0, naye kwa mara nyingine akitokea benchi na kushindwa kufunga,
hivyo kutuhumiwa kucheza kinazi.
Ilielezwa kwamba Simba walitoa Sh. Milioni 25 kumnunua kwa
mkopo mchezaji huyo, ingawa baadaye Simba wakasema waliununua mkataba wa mwaka
mmoja aliobakiza mchezaji huyo Azam FC, nao wakamuongezea wa mwaka mmoja kwa
kumsainisha kwa Sh. Milioni 30, kati ya hizo Milioni 12 akipewa taslimu na 18 akipewa
gari.
Inavyoonekana, Redondo aliwadanganya Simba kwamba amemaliza
mkataba na Azam, wakaingia mkenge na kumpa Sh. Milioni 30 wakimsainisha mkataba
wa miaka miwili, wakati mkataba wake na Azam unamalizika Juni mwakani.
Hili ni kosa sawa na ambalo Simba walilifanya katika usajili
mwingine wa mchezaji wa Azam, Ibrahim Rajab ‘Jeba’, miezi mitatu iliyopita
ambaye alikuwa kwa mkopo Villa Squad wao wakaenda kumsajili bila kuwasiliana na
klabu yake kujua kuhusu mkataba wake, matokeo yake baadaye mchezaji huyo
akarejea Azam.
Simba nao wana lalamiko kama hilo, dhidi ya watani wao wa
jadi, Yanga wanaowatuhumu kumsajili beki Kevin Yondan, wakati bado ana makataba
na Wekundu hao wa Msimbazi, ingawa TFF iliweka sawa kwa kusema Yondan hakuwa na
mkataba na Simba SC.
Baadaye Simba ilitoa ufafanuzi, kwamba ilimuongezea mkataba
Yondan baada ya ule wa awali kumalizika na ikawa inasubiri muda wa usajili
ufike wauwasilishe TFF. Lakini katika kesi ya awali, Simba walipoupeleka
mkataba wao mpya na Yondan, ulionyesha mchezaji huyo anatakiwa kuanza
kuutumikia mkataba huo, Desemba mwaka huu, hivyo TFF ikasema kwa wakati ambao
yuko huru, aichezee Yanga.
Sakata la Yondan litarudi Desemba, wakati ambao atatakiwa
kuanza kuutumikia mkataba wake na Simba, wakati yupo ndani ya mkataba wa miaka
miwili na Yanga.
0 comments:
Post a Comment