• HABARI MPYA

    Saturday, August 11, 2012

    MTAKATIFU TOM AAHIDI UBINGWA WA AFRIKA YANGA

    Kocha Tom kushoto, siku aliposaini mkataba Yanga

    Na Prince Akbar
    KOCHA wa klabu ya Yanga ya Dar es Salaam, Mbelgiji Tom Saintfiet amesema kwamba nia yake ni kuleta mataji zaidi katika klabu hiyo, likiwemo taji la ubingwa wa Afrika, ambalo hakuna timu katika ukanda huu wa Afrika Mashariki na Kati, imewahi kulitwaa.
    Akizungumza na BIN ZUBEIRY katika mahojiano maalum jana, Mtakatifu Tom alisema kwamba akipewa muda na ushirikiano wa kutosha anaweza kutimiza ndoto zake hizo.
    “Mimi ni mshindi na nimekuja Yanga kushinda mataji, na nitaleta mataji mengi zaidi na makubwa kuliko hili, nitaleta hadi Kombe la Afrika,”alisema kocha huyo, ambaye kutokana na kazi yake nzuri alipokuwa Ethiopia, alipachikwa jina Mtakatifu Tom.
    Akiwa anaingia mwezi wa pili tangu aanze kazi Yanga, tayari Tom amekwishaweka Kombe moja kwenye kabati la mataji la Yanga, ambalo ni la Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame.
    Yanga ilitwaa Kombe la Kagame kwa mara ya pili mfululizo wiki mbili zilizopita, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kwa kuifunga Azam FC mabao 2-0, ambayo yalitiwa kimiani na Hamisi Kiiza ‘Diego Milito’ na Said Bahanuzi ‘Spider Man’.
    Hiyo kwa ujumla ilikuwa mara ya tano mfululizo, Yanga inatwaa Kombe hilo, baada ya awali kuchukua mwaka jana, wakiifunga Simba katika fainali bao 1-0, Uwanja wa Taifa mfungaji Kenneth Asamoah ambaye ametemwa, ingawa siku hiyo Kiiza pia alifunga bao safi, ambalo refa alilikataa.
    Yanga ilichukua kwa mara ya kwanza Kombe hilo, mwaka 1975 ikiifunga tena Simba katika fainali, mabao 2-0 wafungaji Sunday Manara ‘Computer’ na Gibson Sembuli (sasa marehemu) Uwanja wa Amaan, Zanzibar.
    Ikachukua tena mwaka 1993, Uwanja wa Nakivubo, Kampala, Uganda kwa kuifunga SC Villa mabao 2-1, yaliyotiwa kimiani na Said Nassor Mwamba ‘Kizota’ (sasa marehemu) na Edibily Jonas Lunyamila.
    Ilichukua tena mwaka 1999, ikiifunga tena SC Villa, Uwanja wa Nakivubo, kwa penalti 5-3, kufuatia sare ya 1-1 ndani ya dakika 120, Yanga ikisawazisha bao kupitia kwa Lunyamila, baada ya Hassan Mubiru kutangulia kuifungia Villa, siku hiyo Manyika Peter akicheza penalti mbili za Waganda.   
    Aidha, kwa kutwaa Kombe hilo chini ya Mbelgiji huyo, Yanga imeendeleza rekodi yake ya kutwaa mataji ya michuano hiyo, chini ya makocha wa kigeni baada ya mwaka 1975 kuchukua chini ya Tambwe Leya aliyekuwa raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) kabla ya kuchukua uraia wa Tanzania, (sasa marehemu), 1993 chini ya Nzoyisaba Tauzany aliyekuwa raia wa Burundi kabla ya kuchukua uraia wa Tanzania, mwaka 1999 chini ya Raoul Shungu wa DRC na mwaka jana chini ya Mganda, Sam Timbe.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: MTAKATIFU TOM AAHIDI UBINGWA WA AFRIKA YANGA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top