• HABARI MPYA

    Wednesday, August 08, 2012

    BAKHRESA: NITAMUUZA BEI POA TU BOCCO

    Bocco 'Adebayor'

    Na Mahmoud Zubeiry
    YUSSUF Said Bakhresa, wakala wa mshambuliaji wa Azam FC, John Raphael Bocco ambaye ameitwa na klabu ya Super Sports United ya Afrika Kusini kufanya majaribio, amesema hataweka tamaa ya fedha iwapo mchezaji huyo atafuzu.
    Akizungumza na BIN ZUBEIRY jana, Yussuf anayetambuliwa na Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA), ambaye awali miaka mitatu iliyopita alimpeleka Israel Bocco ‘Adebayor’ kwa majaribio na akafanya vizuri, alisema kwamba anachojali ni mchezaji huyo kupata timu itakayompa maslahi bora na kumuendeleza zaidi kisoka.
    “Mimi nataka klabu inayotaka kumnunua iilipe tu klabu yake, mimi sitataka hata senti moja yao, kwa sababu najua wachezaji wa Tanzania bado hawajakubalika sana katika soko la soka ya kulipwa, hivyo kufanya tamaa kunaweza kusababisha umharibie mchezaji mwenyewe wakati mwingine,”alisema Yussuf, ambaye mwaka 2009 alimpeleka Mrisho Ngassa majaribio West Ham United.
    Super Sport ilivutiwa na soka ya Bocco, katika michuano ya Klabu Bingwa ya soka Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame, mwezi uliopita, hivyo kumuita kwa majaribio, ambayo akifuzu ataweka historia ya kuwa mchezaji wa pili wa Tanzania kuchezea klabu hiyo, baada ya Suleiman Matola 2005 hadi 2007, akitokea Simba SC.
    Katika Kombe la Kagame, Bocco ambaye ataondoka Jumamosi kwenda kujaribiwa, alifunga mabao matano na kushika nafasi ya tatu katika wafungaji bora, nyuma ya Hamisi Kiiza na Said Bahanuzi wa Yanga, aliyeibuka mfungaji bora.
    Lakini Bocco pia alikuwa mfungaji bora wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara msimu uliopita, kwa mabao yake 18 akiwapiku hadi washambuliaji wa kigeni waliocheza ligi hiyo msimu huo, Emmanuel Okwi, Kenneth Asamoah, Davies Mwape na Dalington Enyiana.
    Tangu aipandishe Ligi Kuu Azam FC msimu wa 2008/2009 kwa mabao yake, akiibuka mfungaji bora wa Ligi Daraja la Kwanza, Bocco amekuwa akiingia kwenye mbio za kuwania kiatu cha dhahabu cha Ligi Kuu, msimu wa kwanza akizidiwa na Boniphace Ambani aliyekuwa Yanga, msimu wa pili Mussa Mgosi aliyekuwa Simba na msimu wa tatu na Mrisho Ngassa, kabla ya msimu uliopita kutimiza ndoto zake za kuwa mfungaji bora wa ligi hiyo.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: BAKHRESA: NITAMUUZA BEI POA TU BOCCO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top