Yanga mazoezini |
Na Prince Akbar
MABINGWA wa soka Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame, Yanga
SC ya Dar es Salaam leo wanatarajiwa kuanza tena mazoezi ya kujiandaa na Ligi
Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, baada ya mapumziko ya siku mbili, yaliyotokana na
ziara yao ya Bungeni Dodoma Jumatatu.
Yanga, ambao juzi walionyesha Kombe lao ubingwa wa Kagame, katika
ukumbi wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, mjini Dodoma, walirejea Dar
es Salaam jana lakini kutokana na wachezaji wake kuchoka, hawakufanya mazoezi.
Yanga, waliotwaa Kombe hilo mara mbili mfululizo sasa, walifanya
mazoezi ya mwisho Jumapili asubuhi kabla ya safari ya Dodoma na sasa watafanya
tena mazoezi leo, saa 3:00 asubuhi katika Uwanja wa Loyola, Mabibo, Dar es
Salaam.
Yanga ilitwaa Kombe la Kagame kwa mara ya pili mfululizo
wiki iliyopita, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kwa kuifunga Azam FC mabao 2-0,
ambayo yalitiwa kimiani na Hamisi Kiiza ‘Diego Milito’ na Said Bahanuzi ‘Spider
Man’.
Hiyo kwa ujumla ilikuwa mara ya tano mfululizo, Yanga
inatwaa Kombe hilo, baada ya awali kuchukua mwaka jana, wakiifunga Simba katika
fainali bao 1-0, Uwanja wa Taifa mfungaji Kenneth Asamoah ambaye ametemwa,
ingawa siku hiyo Kiiza pia alifunga bao safi, ambalo refa alilikataa.
Yanga ilichukua kwa mara ya kwanza Kombe hilo, mwaka 1975
ikiifunga tena Simba katika fainali, mabao 2-0 wafungaji Sunday Manara
‘Computer’ na Gibson Sembuli (sasa marehemu) Uwanja wa Amaan, Zanzibar.
Ikachukua tena mwaka 1993, Uwanja wa Nakivubo, Kampala,
Uganda kwa kuifunga SC Villa mabao 2-1, yaliyotiwa kimiani na Said Nassor
Mwamba ‘Kizota’ (sasa marehemu) na Edibily Jonas Lunyamila.
Ilichukua tena mwaka 1999, ikiifunga tena SC Villa, Uwanja
wa Nakivubo, kwa penalti 5-3, kufuatia sare ya 1-1 ndani ya dakika 120, Yanga
ikisawazisha bao kupitia kwa Lunyamila, baada ya Hassan Mubiru kutangulia
kuifungia Villa, siku hiyo Manyika Peter akicheza penalti mbili za
Waganda.
0 comments:
Post a Comment