• HABARI MPYA

    Thursday, August 16, 2012

    BIN KLEB AMTUNUKIA TUZO YA UONGO 'ALHAJ' RAGE

    Bin Kleb

    Na Prince Akbar
    MJUMBE wa Kamati ya Utendaji ya klabu ya Yanga, Abdallah Ahmad Bin Kleb, amerejea Dar es Salaam na kusema kwamba Mwenyekiti wa Simba SC, Alhaj Ismail Aden Rage anastahili tuzo ya kutunga uongo kwa kitendo chake cha kuwadanganya wanachama wa Simba eti kuna mtoto wa kigogo aliingilia usajili wa Mbuyu Twite.
    “Rage anastahili tuzo ya muongo, ile vita ilikuwa kati yangu mimi na yeye, nadhani yeye alikuja Kigali kupiga picha na yule mchezaji, baada ya kushindwa kufanya hivyo alipokuwa Dar es Salaam, maana yake alikuja haraka haraka akazungumza na kiongozi mmoja wa FERWAFA (Shirikisho la Soka Rwanda), akapiga picha na Twite akaondoka.
    Karudi Dar es Salaam kwenye Mkutano Mkuu anasema amemsajili Twite, baada ya mimi kuonyesha vielelezo vya kumsajili huyo mchezaji kama mikataba na picha akiwa anasaini na kukabidhiwa jezi, akaanza kusema kuna mtoto wa kigogo, huyo mzee vipi? Mbona anakuwa muongo namna hii.
    Yeye aseme kweli tu, hana uzoefu na mambo haya, yeye ni mtu wa kuropoka tu, hawezi kazi,”alisema Bin Kleb.
    Rage, alilalamika hadi kutoa machozi mjini Dodoma, wakati akizungumzia sakata la Mbuyu Twite akidai kuna mtoto wa kigogo aliingilia kati na ndio maana mchezaji huyo akabadilisha uamuzi wake na kwenda Yanga.
    Rage alidai kumsaini kwanza Twite, huku akinywa kahawa mjini Kigali na akadai wakati anamsaini na kumpa dola za Kimarekani 30,000 Yanga wakapiga simu na mchezaji huyo akawajibu amekwishamalizana na watu wa Simba.
    Lakini baadaye Twite akaibuka akisaini Yanga na kurudisha fedha za Wekundu hao wa  Msimbazi.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: BIN KLEB AMTUNUKIA TUZO YA UONGO 'ALHAJ' RAGE Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top