![]() |
| Stewart Hall |
Na Prince Akbar
AZAM FC, washindi wa Medali tatu za Fedha, Ligi Kuu msimu uliopita,
Kombe la Urafiki na Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame, leo
wanatarajiwa kumtambulisha kocha wao mpya kutoka Serbia, Boris Bunjak ambaye atarithi mikoba
ya Muingereza Stewart Hall aliyefukuzwa wiki iliyopita.
Habari kutoka ndani ya Azam, zimesema kwamba baada Bodi ya
Wakurugenzi na Menejimenti ya Azam, ambao pia ni mabingwa wa Kombe la Mapindzui,
kupitia wasifu wa makocha kibao, walioomba kazi katika klabu hiyo, imeridhishwa
na wasifu wa Mserbia huyo.
Mserbia huyo atapewa mkataba wa mwaka mmoja kwa kuanzia na
akifanya vizuri ataongezewa mkataba.
Kwa kuajiriwa kocha huyo, Vivek Nagul kutoka India,
aliyekuwa anakaimu nafasi ya Stewart, ambaye aliletwa na Muingereza huyo
anarejea kwenye majukumu ya kufundisha timu za vijana, wakati Kocha Msaidizi
ataendelea kuwa Kali Ongala.
Stewart kabla ya kuja Tanzania mwaka juzi, akianza
kufundisha timu ya taifa ya Zanzibar, aliwahi kufanya kazi India kwa miaka
miwili.
Akiwa India ndipo alikutana na Vivek na wakafanya naye kazi
pamoja na akaridhishwa na utendaji wake, hasa katika eneo la vijana na ndio
maana alipotua Azam FC akamleta aje kumsaidia katika eneo hilo.
Vivek amekuwa Kocha Mkuu wa Azam Academy tangu mwaka jana,
akisaidiwa na Iddi Cheche na Philipo Alando.
Stewart alifukuzwa Jumatano iliyopita kwa kosa la kukaidi
maagizo ya Bodi ya Ukurugenzi ya klabu hiyo, kumpanga Mrisho Khalfan Ngassa
katika mechi ya fainali ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la
Kagame dhidi ya Yanga.
Kikao cha Jumatano hiyo pamoja baina ya Bodi ya Ukurugenzi
ya Azam FC, Mwanasheria wa kampuni na kocha Stewart kiliafiki kuvunjwa kwa ndoa
hiyo na Azam FC ikawa chini ya Nagul, akisaidiwa na Kali Ongala.
Baada ya mechi ya Nusu Fainali ya Kagame, kati ya Azam na AS
Vita ya DRC, Stewart aliitwa na kuambiwa asimtumie tena Ngassa kwa kitendo cha
mchezaji huyo kwenda kuibusu na kuivaa jezi ya Yanga, baada ya kufunga bao la
ushindi. Ngassa ameuzwa Simba SC, baada ya sakata hilo.
Lakini Stewart katika kikao hicho, kwanza alimtetea Ngassa
kutokana na kufunga bao la ushindi na kumuelezea kama mchezaji muhimu kwake,
lakini msimamo wa bodi ulikuwa ni asipangwe tena.
Katika fainali, Stewart alimvalisha jezi Ngassa
akamuanzishia benchi, lakini kama ilivyokuwa kwenye Nusu Fainali alimuingiza
kipindi cha pili timu ikiwa nyuma kwa 1-0 na mwisho wa mchezo ikashinda 2-1
yeye akifunga la pili, dhidi ya Yanga pia alimuingiza timu ikiwa nyuma kwa 1-0.
Lakini Ngassa alishindwa kurudia kile alichofanya kwenye
mechi na AS Vita na Yanga ikashinda 2-0.
Mserbia huyo anakuwa kocha wa tano Azam, ndani ya miaka minne
tangu ianze kucheza Ligi Kuu, 2008 baada ya Stewart, Mbrazil Neider dos Santos,
Sylvester Marsh na Itamar Amorin, Mbrazil mwingine.
Lakini ni Stewart angalau anaacha kumbukumbu ya taji na
Medali Azam, baada ya kuiwezesha kutwaa Kombe la Mapinduzi Januari, kushika
nafasi ya pili katika Ligi Kuu Aprili, kabla ya kushika nafasi ya pili Kombe la
Urafiki na Kagame mwezi uliopita.
Stewart ana sifa ya kutokuwa mbinafsi na mwenye kuwaamini
watu wa chini yake, kwa mfano namna ambavyo amekuwa akimpromoti Kali Ongala.
Alimkuta Kali kama mchezaji, lakini kwa sababu ya umri kumtupa mkono,
akashauriana naye awe Kocha Msaidizi na mshambuliaji huyo wa zamani wa Yanga,
akakubali.
Chini ya Stewart, Kali alikuwa akiachiwa timu aiongoze ili
kumjengea kujiamini zaidi na mwezi uliopita aliachiwa timu kwenye Kombe la
Urafiki, akaifikisha fainali, ambako ilifungwa na Simba kwa penalti kufuatia
sare ya 2-2 ndani ya dakika 90.
Wachezaji wa Azam na makocha wapya wa klabu hiyo, pamoja na
baadhi ya maofisa wa klabu hiyo, waliangua vilio, wakati wakimuaga Stewart.
Wachezaji walioongoza kwa kilio Uwanja wa Chamazi Ijumaa
iliyopita, ni Luckson Kakolaki, Ibrahim Mwaipopo, Ramadhan Chombo ‘Redondo’,
Salum Abubakar ‘Sure Boy’, Hajji Nuhu na Erasto Nyoni, wakati kwa maofisa,
aliyeongoza ni Vivek Nagul.
Stewart mwenyewe pia alibubujikwa machozi wakati anaagana na
familia yake, aliyoishi nayo kwa zaidi ya mwaka kwa furaha, amani, upendo na
mafanikio.



.png)
0 comments:
Post a Comment