![]() |
| Stewart Hall wa kwanza kulia, anayemfuatia ni Kali Ongala |
Na
Prince Akbar
KOCHA mpya wa Azam FC, anayerithi mikoba ya Muingereza
Stewart Hall ni Mserbia, ambaye atatambulishwa mapema kesho asubuhi, BIN
ZUBEIRY imeipata hiyo.
Habari kutoka ndani ya Azam, zimesema kwamba baada
Bodi ya Wakurugenzi na Menejimenti ya Azam kupitia wasifu wa makocha kibao,
walioomba kazi katika klabu hiyo, imeridhishwa na wasifu wa Mserbia huyo.
Mserbia huyo atapewa mkataba wa mwaka mmoja kwa
kuanzia na akifanya vizuri ataongezewa mkataba.
Kwa kuajiriwa kocha huyo, Vivek Nagul kutoka India,
aliyekuwa anakaimu nafasi ya Stewart, ambaye aliletwa na Muingereza huyo anarejea
kwenye majukumu ya kufundisha timu za vijana, wakati Kocha Msaidizi ataendelea
kuwa Kali Ongala.
Stewart kabla ya kuja Tanzania mwaka juzi, akianza
kufundisha timu ya taifa ya Zanzibar, aliwahi kufanya kazi India kwa miaka
miwili.
Akiwa India ndipo alikutana na Vivek na wakafanya
naye kazi pamoja na akaridhishwa na utendaji wake, hasa katika eneo la vijana
na ndio maana alipotua Azam FC akamleta aje kumsaidia katika eneo hilo.
Vivek amekuwa Kocha Mkuu wa Azam Academy tangu mwaka
jana, akisaidiwa na Iddi Cheche na Philipo Alando.
Stewart alifukuzwa Jumatano iliyopita kwa kosa la
kukaidi maagizo ya Bodi ya Ukurugenzi ya klabu hiyo, kumpanga Mrisho Khalfan
Ngassa katika mechi ya fainali ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe
la Kagame dhidi ya Yanga.
Kikao cha Jumatano hiyo pamoja baina ya Bodi ya
Ukurugenzi ya Azam FC, Mwanasheria wa kampuni na kocha Stewart kiliafiki
kuvunjwa kwa ndoa hiyo na Azam FC ikawa chini ya Nagul, akisaidiwa na Kali
Ongala.
Baada ya mechi ya Nusu Fainali ya Kagame, kati ya
Azam na AS Vita ya DRC, Stewart aliitwa na kuambiwa asimtumie tena Ngassa kwa
kitendo cha mchezaji huyo kwenda kuibusu na kuivaa jezi ya Yanga, baada ya
kufunga bao la ushindi. Ngassa ameuzwa Simba SC, baada ya sakata hilo.
Lakini Stewart katika kikao hicho, kwanza alimtetea
Ngassa kutokana na kufunga bao la ushindi na kumuelezea kama mchezaji muhimu
kwake, lakini msimamo wa bodi ulikuwa ni asipangwe tena.
Katika fainali, Stewart alimvalisha jezi Ngassa
akamuanzishia benchi, lakini kama ilivyokuwa kwenye Nusu Fainali alimuingiza
kipindi cha pili timu ikiwa nyuma kwa 1-0 na mwisho wa mchezo ikashinda 2-1
yeye akifunga la pili, dhidi ya Yanga pia alimuingiza timu ikiwa nyuma kwa 1-0.
Lakini Ngassa alishindwa kurudia kile alichofanya
kwenye mechi na AS Vita na Yanga ikashinda 2-0.
Mserbia huyo anakuwa kocha wa tano Azam, ndani ya
miaka minne tangu ianze kucheza Ligi Kuu, 2008 baada ya Stewart, Mbrazil Neider
dos Santos, Sylvester Marsh na Itamar Amorin, Mbrazil mwingine.
Lakini ni Stewart angalau anaacha kumbukumbu ya taji
na Medali Azam, baada ya kuiwezesha kutwaa Kombe la Mapinduzi Januari, kushika
nafasi ya pili katika Ligi Kuu Aprili, kabla ya kushika nafasi ya pili Kombe la
Urafiki na Kagame mwezi uliopita.
Stewart ana sifa ya kutokuwa mbinafsi na mwenye
kuwaamini watu wa chini yake, kwa mfano namna ambavyo amekuwa akimpromoti Kali
Ongala. Alimkuta Kali kama mchezaji, lakini kwa sababu ya umri kumtupa mkono,
akashauriana naye awe Kocha Msaidizi na mshambuliaji huyo wa zamani wa Yanga,
akakubali.
Chini ya Stewart, Kali alikuwa akiachiwa timu
aiongoze ili kumjengea kujiamini zaidi na mwezi uliopita aliachiwa timu kwenye
Kombe la Urafiki, akaifikisha fainali, ambako ilifungwa na Simba kwa penalti
kufuatia sare ya 2-2 ndani ya dakika 90.
Wachezaji wa Azam na makocha wapya wa klabu hiyo,
pamoja na baadhi ya maofisa wa klabu hiyo, waliangua vilio, wakati wakimuaga
Stewart.
Wachezaji walioongoza kwa kilio Uwanja wa Chamazi Ijumaa
iliyopita, ni Luckson Kakolaki, Ibrahim Mwaipopo, Ramadhan Chombo ‘Redondo’,
Salum Abubakar ‘Sure Boy’, Hajji Nuhu na Erasto Nyoni, wakati kwa maofisa,
aliyeongoza ni Vivek Nagul.
Stewart mwenyewe pia alibubujikwa machozi wakati
anaagana na familia yake, aliyoishi nayo kwa zaidi ya mwaka kwa furaha, amani,
upendo na mafanikio.



.png)
0 comments:
Post a Comment