• HABARI MPYA

    Monday, August 06, 2012

    MTIBWA SUGAR WAIPIGA 2-0 POLISI MOSHI

    Mtibwa Sugar 2009

    Na Prince Akbar
    MTIBWA Sugar imeanza vema michuano ya Kombe la BancABC Super 8 baada ya kuifunga Polisi, zote za Morogoro mabao 2-0 kwenye Uwanja wa Ushirika mjini Moshi, Kilimanjaro jioni ya leo.
    Mabao ya Mtibwa, inayofundishwa na mchezaji wake wa zamani, Mecky Mexime yalitiwa kimiani na Vincent Barnabas dakika ya 39 na Yussuf Bida dakika ya 49, wakati la Polisi lilifungwa na Nicholas Kabipe mapema tu dakika ya 10.   
    Mechi hiyo ilipangwa kufanyika kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid mjini Arusha jana, lakini Menejimenti ya Uwanja huo ilizizuia timu zikiwa getini na kudai hawana taarifa za mashindano hayo.
    Jana ilielezwa mechi hiyo ingechezwa leo kwenye Uwanja wa General Tyre mjini humo, badala ya Sheikh Amri Abeid, lakini imeshindikana na kuchezwa Moshi.
    Katika mechi zilizochezwa jana, mapema jioni Simba B ilitoka sare ya 1-1 na Jamhuri ya Pemba kwenye Uwanja wa Chamazi jijini Dar es Salaam katika mechi ya Kundi A. Jamhuri ndio waliotangulia kupata bao kupitia kwa Bakari Khamis dakika ya 48, akiunganisha krosi ya Abdallah Othman, kabla ya Shomary Kapombe, mchezaji pekee wa Simba A aliyecheza, kuisawazishia timu yake kwa penalti dakika ya 83, baada ya Miraj Adam kuangushwa kwenye eneo la hatari na Mfaume Shaaban.
    Mechi iliyofuatia usiku Uwanja wa Amaan, Zanzibar, Azam FC iliifunga Super Falcon mabao 2-0, wafungaji Abdi Kassim Sadallah ‘Babbi’ dakika ya 20 na Joseph Lubisha Kimwaga, wa Azam B dakika ya 60.
    Michuano hiyo ina makundi mawili, ikishirikisha timu nane, Kundi A likiwa na timu za Simba, Jamhuri, Zimamoto na Mtende FC, wakati Kundi B kuna Super Falcon, Azam FC, Mtibwa Sugar na  Polisi Moro na bingwa wa michuano hiyo inayodhaminiwa na Bank ABC ataondoka na Sh. milioni 40, mshindi wa pili Sh. milioni 20, wa tatu Sh. milioni 15 sawa na wa nne, wakati washiriki wengine wataondoka na Sh. Milioni 5 kila moja.
    Michuano itachezwa katika vituo vinne vya Dar es Salaam, Zanzibar, Arusha ambako imekataliwa na Mwanza, ambapo timu zitasafirishwa kwa ndege kwenda kucheza mechi katika vituo vyote. Kila timu itacheza mechi mechi katika vituo vituo vitatu tofauti. Simba baada ya mechi ya jana, itakwea pipa kwenda Arusha kucheza dhidi ya Mtende FC Alhamisi na itasafiri kwenda Mwanza kwa ajili ya mechi yao ya mwisho ya Kundi A dhidi ya Zimamoto Jumamosi.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: MTIBWA SUGAR WAIPIGA 2-0 POLISI MOSHI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top