• HABARI MPYA

    Monday, August 06, 2012

    MTIBWA NA POLISI MORO SASA LEO BANC ABC SUPER 8


    Shaaban Kado, kipa wa Mtibwa
    Na Prince Akbar
    MECHI ya kuwania Kombe la BancABC Super 8 iliyoshindikana kufanyika jana, kati ya Mtibwa Sugar na Polisi, zote za Morogoro baada ya Menejimenti ya Uwanja wa Sheikh Amri Abeid kudai kutokuwa na taarifa za mashindano hayo, sasa itachezwa leo.
    Lakini mechi hiyo inawezekana ikachezwa kwenye Uwanja mwingine wa General Tyre mjini humo, badala ya Sheikh Amri Abeid.
    Katika mechi zilizochezwa jana, mapema jioni Simba B ilitoka sare ya 1-1 na Jamhuri ya Pemba kwenye Uwanja wa Chamazi jijini Dar es Salaam katika mechi ya Kundi A. Jamhuri ndio waliotangulia kupata bao kupitia kwa Bakari Khamis dakika ya 48, akiunganisha krosi ya Abdallah Othman, kabla ya Shomary Kapombe, mchezaji pekee wa Simba A aliyecheza, kuisawazishia timu yake kwa penalti dakika ya 83, baada ya Miraj Adam kuangushwa kwenye eneo la hatari na Mfaume Shaaban.
    Mechi iliyofuatia usiku Uwanja wa Amaan, Zanzibar, Azam FC iliifunga Super Falcon mabao 2-0, wafungaji Abdi Kassim Sadallah ‘Babbi’ dakika ya 20 na Joseph Lubisha Kimwaga, wa Azam B dakika ya 60.
    Michuano hiyo ina makundi mawili, ikishirikisha timu nane, Kundi A likiwa na timu za Simba, Jamhuri, Zimamoto na Mtende FC, wakati Kundi B kuna Super Falcon, Azam FC, Mtibwa Sugar na  Polisi Moro na bingwa wa michuano hiyo inayodhaminiwa na Bank ABC ataondoka na Sh. milioni 40, mshindi wa pili Sh. milioni 20, wa tatu Sh. milioni 15 sawa na wa nne, wakati washiriki wengine wataondoka na Sh. Milioni 5 kila moja.
    Michuano itachezwa katika vituo vinne vya Dar es Salaam, Zanzibar, Arusha na Mwanza, ambapo timu zitasafirishwa kwa ndege kwenda kucheza mechi katika vituo vyote. Kila timu itacheza mechi mechi katika vituo vituo vitatu tofauti. Simba baada ya mechi ya leo, itakwea pipa kwenda Arusha kucheza dhidi ya Mtende FC Alhamisi na itasafiri kwenda Mwanza kwa ajili ya mechi yao ya mwisho ya Kundi A dhidi ya Zimamoto Jumamosi.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: MTIBWA NA POLISI MORO SASA LEO BANC ABC SUPER 8 Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top