![]() |
| Simba SC |
Na Princess Asia
KIKOSI kizima cha wachezaji wa Simba SC, leo kinatarajiwa kutembelea
kituo cha watoto yatima cha Maungu Orphanage Center, kilichopo Kinondoni
Mkwajuni, Dar es Salaam katika mfululizo wa Wiki ya Simba na Jamii, kuelekea
tamasha la kuazimisha kuzaliwa kwa klabu hiyo, Simba Day, Agosti 8, mwaka huu.
Wachezaji wa Simba, wanatarajiwa kujumuika na watoto hao,
wanaoishi katika mazingira magumu na kuwafariji sambamba na kuwapa zawadi
mbalimbali.
Ratiba inaonyesha kesho Simba watatembelea wagonjwa katika
hospitali ya Mwananyamala mjini Dar es Salaam na keshokutwa ndipo litafanyika
Tamasha la Simba Day, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Katika tamasha hilo, litakalotanguliwa na burudani mbalimbali,
litafuatiwa na utambulisho wa wachezaji wote wa kikosi cha msimu ujao cha Simba
SC wakiwemo Mrisho Khalfan Ngassa aliyesajiliwa kutoka Azam FC, Mbuyu Twite
kutoka APR ya Rwanda na wengineo.
Baada ya utambulisho, Simba itacheza mechi ya kirafiki na
timu ambayo hadi sasa haijatajwa ingawa BIN ZUBEIRY inajua klabu hiyo ipo
kwenye mawasiliano na Nairobi City Stars ya Kenya.
Siku inayofuata, yaani Agosti 9, Simba watatembelea shule ya
msingi Mgulani, ambayo BIN ZUBEIRY na mastaa wengine kibao
bongo kama Rashid ‘Snake Boy’ Matumla wamesoma ili kuhamasisha michezo
mashuleni na Agosti 10, mabingwa hao wa Tanzania, watahitimisha wiki ya Simba na
Jamii, kwa kutembelea kiwanda cha Kampuni ya Bia Tanzania (TBL), kilichopo
Ilala, Dar es Salaam.
TBL ndio wadhamini wakuu wa Simba SC, kupitia bia yao ya
Kilimanjaro Premium Lager, ambayo pia ndio imedhamini Wiki nzima ya Simba na
Jamii, kuanzia kwenye Mkutano Mkuu wa mwaka wa klabu hiyo, jana Bwalo la
Maofisa wa jeshi la Polisi, Oysterbay, Dar es Salaam,
RATIBA YA
WIKI YA SIMBA NA JAMII:
Agosti 5, 2012: Mkutano
Mkuu wa mwaka Simba SC (Polisi Oystrebay)
Agosti 6, 2012: Kutembelea
watoto yatima Maungu Orphanage Center, K’ndoni Mkwajuni
Agosti 7, 2012: Kutembelea
wagonjwa Mwananyamala hospitali
Agosti 8, 2012: Simba Day (Uwanja wa Taifa, burudani na mechi)
Agosti 9, 2012: Kutembelea
shule ya msingi Mgulani kuhamasisha michezo mashuleni
Agosti 10, 2012: Kutembelea
kiwanda cha TBL Ilala



.png)
0 comments:
Post a Comment