WADADA wawili mashuhuri katika mchezo wa tennis Venus na
Serena Williams wametetea mataji yao mawili waliyoshinda katika michezo ya
Olympiki ya Beijing miaka miine iliyopita kwa ushindi wa seti 6-4 6-4 dhidi ya
Andrea Hlavackova na Lucie Hradecka wa Jamhuri ya Chek katika mshindano ya
Olympic yanayoendelea jijini London Uingereza.
Ushindi huu unamaanisha kuwa Wamarekani hawa wanakuwa ndio
wachezaji wa kwanza katika mchezo wa tennis katika historia ya michezo ya
Olympic kuwahi kushinda medali katika mashindano matatu tofauti.
Walifanikiwa kushinda medali katika michezo hiyo
ilipofanyika katika miji ya Sydney Australia, Beijing Uchina, na sasa London
nchini Uingereza.
Tiki Gelana kutoka Ethiopia ameibuka mshindi wa kwanza
katika mbio za marathon kilometa 42 wanawake kwa rekodi ya saa 2 dakika 23
sekunde 7 na kupata medali ya dhahabu.
Priscah Jeptoo kutoka Kenya amechukua nafasi ya pili katika
mbio hizo akitumia saa 2 dakika 23 nukta 12 na kujinyakulia medali ya fedha.
Naye Tatyana Petrova wa Urusi alishika nafasi ya tatu baada
ya kutumia saa 2 dakika 23 nukta 29 na kupata medali ya shaba.
Nao Mary Jepkosgei, Edna Kiplagat Ngeringwony kutoka Kenya
na Diane Nukuri wa Burundi hawakufanikiwa katika mashindano hayo.
Jepkosgei alitumia saa 2 dakika 23 sekunde 56, huku Kiplagat
akitumia saa 2 dakika 27 sekunde 52. Naye Diane alitumia saa 2 dakika 30
sekunde 13.
Naye Mo Farah wa Uingereza ameshinda medali ya dhahabu mbio
za mita 10,000 wanaume katika michezo ya London Olympics 2012.
Farah mwenye umri wa miaka 29 bingwa wa mbio za mita 5,000
alitumia dakika 27 sekunde 30 nukta 42 huku Mmarekani Galen Rupp akishika
nafasi ya pili kwa kutumia dakika 27 sekunde 30 nukta 90 na kushinda medali ya
fedha.
Tariku Bekele kutoka Ethiopia alinyakua medali ya shaba
baada ya kutumia dakika 27 sekunde 31 nukta 43.
Ushindi wa Farah umeizuia Ethiopia kushinda mara nne
mfululizo katika mbio hizo na kuzuia Kenenisa Bekele ushindi wa mara tatu
mfululizo.
Miaka minne iliyopita jijini Beijing, Farah alishindwa
kufuzu fainali za mbio za mita 5000 na toka wakati huo alikusudia kufanya
juhudi zaidi.




.png)
0 comments:
Post a Comment