![]() |
Wachezaji wa Ngorongoro |
Na Princess Asia
NGORONGORO Heroes, timu ya taifa ya vijana wenye umri chini
ya miaka 20 imewasili asubuhi hii (Agosti 10 mwaka huu) kwa ndege ya Overland
Airways kwenye mji wa Ilorin, Jimbo la Kwara lililo Kusini mwa Nigeria tayari
kwa mechi ya marudiano dhidi ya wenyeji Flying Eagles itakayochezwa Jumapili.
Mechi hiyo ya raundi ya pili ya michuano ya U20 ya Afrika
itachezwa kwenye Uwanja wa Township kuanzia saa 10 kamili jioni kwa saa hapa
ambapo Tanzania itakuwa ni saa 12 kamili jioni. Ngorongoro Heroes ilitua jana
(Agosti 9 mwaka huu) jijini Lagos ambapo ililala kabla ya kuja hapa.
Msafara wa Ngorongoro Heroes wenye watu 27 ukiongozwa na
mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)
ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Mtwara (MTWAREFA)
ulipokea na Ofisa Ubalozi wa Tanzania nchini Nigeria, Jones Mndeme na viongozi
wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Nigeria (NFF) umefikia hoteli ya Kingstone
Grand Suites.
Kwa mujibu wa Kocha wa Ngorongoro Heroes, Jakob Michelsen,
timu itafanya mazoezi leo jioni (Agosti 10 mwaka huu) wakati mazoezi ya mwisho
yatakuwa kesho jioni (Agosti 11 mwaka huu) kwenye uwanja ambao utatumika kwa
mechi ya Jumapili.
Wachezaji wote wako katika hali nzuri isipokuwa Issa Rashid
na Aishi Manula ambao walikuwa wakisumbuliwa na tumbo baada ya timu kufika jana
(Agosti 9 mwaka huu) jijini Nairobi, Kenya ambapo ilibadili ndege kuja Nigeria.
Hata hivyo, hali zao zinaendelea vizuri na huenda wakawa sehemu ya kikosi cha
kwanza kitakachoivaa Flying Eagles.
Mbali ya Rashid na Manula, wachezaji wengine walioko hapa
kwenye kikosi cha Ngorongoro Heroes ni Barwany Khomeiny, Samir Ruhava, Dizana
Yarouk, Leonard Muyinga, Hassan Ramadhan, Jamal Mroki, Omari Kheri, Frank
Domayo, nahodha Omega Seme, Abdallah Kilala, Hassan Dilunga, Ramadhan Singano,
Simon Msuva, Said Zege, Atupele Gren na Ramadhan Salum.
Mbali ya Michelsen, Benchi la Ufundi linaundwa na Mohamed
Rishad 'Adolf' (Kocha Msaidizi), Peter Manyika (Kocha wa makipa), Nassoro
Matuzya (Daktari), Joakim Mshanga (Physio), Juma Kizwezwe (Mtunza vifaa) na
Meneja wa timu John Lyimo.
Flying Eagles ambayo ilishinda mechi ya kwanza mabao 2-1
nayo tayari imeshaingia hapa Ilorin ikitokea Lagos kwa mechi hiyo ambayo
matokeo yake yataamua timu ipi itaingia raundi ya tatu ambayo ni ya mwisho
kabla ya fainali za Afrika kwa vijana wenye umri chini ya miaka 20
zitakazofanyika mwakani nchini Algeria. Timu itakayovuka itacheza raundi hiyo
na mshindi kati ya Congo Brazzavile na Afrika Kusini.Katika mchezo huo utakaochezwa Jumapili, Ngorongoro inahitaji kushinda 2-0 ili kusonga mbele, baada ya awali kufungwa na Nigeria mabao 2-1, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam wiki iliyopita, mabao ya mshambuliaji wa Enugu Rangers, Achaji Gero katika dakika ya pili na 44.
Bao la Ngorongoro lililofungwa na mshambuliaji mpya wa Coastal Union ya Tanga, Atupele Green aliyesajiliwa kutoka Yanga B, dakika ya 50, akimalizia krosi ya Ramadhani Singano ‘Messi’.
Ngorongoro wangeweza kupata mabao zaidi kwenye mechi hiyo, kama wangecheza soka ya chini, lakini kutia krosi za juu kwenye lango la Nigeria ilikuwa ni kuwatesa washambuliaji wao wafupi, Atupele na Simon Msuva.
Baada ya mchezo huo, kocha wa Ngorongoro Heroes, Mdenmark Jakob Michelsen alisema kwamba ataongeza nguvu katika kikosi chake kwa kuwaita wachezaji wawili wanaocheza nje, kiungo Adam Nditi wa Chelsea na Thomas Ulimwengu wa Tout Puissant Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), sambamba na nyota wengine waliokwenda Ujerumani n TSU kwenye michuano ya Fallerhof.
Bahati mbaya kwake, siyo tu Chelsea haijamruhusu Nditi, bali hata Mazembe, safari hii imegoma kumpandisha ndege Ulimwengu.
Katika mchezo wa kwanza, vikosi vilikuwa; Ngorongoro; Barwany Khomein, Omega Seme, Jamal Mroki, Issa Rashid, Ruhana Samir, Yarouk Ramadhan, Kheri Salum/Jerome Lambele, Frank Damayo, Simon Msuva, Atupele Green na Ramadhan Singano.
Flying Eagles; Samuel Okani, Hassan Abubakar, Ahiyu Mohamed, Ikechukwu Okine, Chizoba Amaefule, Agboyi Oubokha, Moses Orkuma, Chidi Osochukwu, Yahaya Adam/Harrison Egbune, Achaji Gero na Aminu Omar/Uchw Agbo.
0 comments:
Post a Comment