![]() |
Kaburu kulia akimkabidhi Mama Zainab Sh. 500,000 |
MABINGWA wa soka Tanzania Bara, Simba SC leo wamehitimisha
Wiki ya Simba na Jamii, kwa kutoa misaada yenye jumla ya thamani ya Sh. Milioni
1.5 katika kituo cha kulelea watoto yatima, Maunga Orphanage Center, kilichopo Kinondoni
Hananasif, Dar es Salaam.
Baadhi ya wachezaji wa Simba, Emanuel Okwi, Juma Nyosso,
Uhuru Suleiman, Meneja Nico Nyagawa, Daktari Cossmas Kapinga, Ofisa Habari,
Ezekiel Kamwaga, Katibu Evodius Mtawala na Makamu Mwenyekiti, Geoffrey Nyange ‘Kaburu’
walijumuika na watoto wa kituo hicho kuwafariji.
Akizungumza baada ya kukabidhi fedha taslimu Sh. 500,000
mbali na unga, mchele, sabuni na bidhaa nyingine, Kaburu alisema kwamba huo ni
mwanzo tu na watakuwa wakiendelea kusaidia kituo hicho.
“Simba SC ni taasisi kubwa, tunasema tumeguswa na kilio
chenu, nasi tunaahidi kuendelea kusaidia kadiri ambavyo tutakuwa tukipokea
maombi kutoka kwenu,”alisema Kaburu.
Akitoa shukrani baada ya kupokea misaada hiyo, Katibu wa
kituo hicho, Rashid Mpinda aliwashukuru Simba SC na kuwatakia kila heri katika
msimu ujao, kuanzia kwenye Ligi Kuu na michuano ya Afrika.
Maunga Orphanage Center kilianzishwa mwaka 2008 kikiwa na
watoto wanne, chini ya mmiliki wake, Mama Zainab Bakari na sasa kina watoto
zaidi ya 60, kati ya hao 30 wakiwa wanaishi moja kwa moja kituoni hapo na 30
wengine wanashinda kituoni na kwenda kulala kwa walezi wao.
Mama Zainab alisema kwamba changamoto zinazowakabili mbali
na kukosa eneo la kutosha kwa malazi ya watoto na hata eneo la kufanyia
michezo, lakini pia gharama za kuwasomesha watoto hao pia ni baadhi ya changamoto
nyingine zinazowakabili.
Alisema watoto wote waliofikisha umri wa kwenda shule,
wanawasomesha katika shule za Hananasif na Mkunguni na kinachowasumbua ni ada
za watoto na michango mingine ya shule.
Mama Zainab alisema kituo chao hadi sasa hakina wafadhili,
zaidi ya kutegemea michango ya wadau kama ambayo Simba SC wametoa leo na pia
misaada ya Diwani wao, Abbas Tarimba.
Alisema wanahitaji eneo lingine kubwa kwa ajili ya kujenga
kituo kikubwa kitakachopokea na kuhudumia watoto wengi zaidi, hivyo anaomba
wajitokeze wafadhili wa kuwasaidia.
Emmnauel Okwi, Uhuru na Nyosso kama ilivyokuwa kwa viongozi
wao, walionyesha kuguswa na matatizo ya watoto hao na kuahidi binafsi
kutembelea tena katika kituo hicho kuwasaidia.
Katika ratiba ya Wiki ya Simba SC na Jamii, mambo mawili tu yameshindikana
kufanyika, kutembelea shule ya Msingi Mgulani na Kiwanda cha Bia Tanzania (TBL),
ambao ni wadhamini wa klabu hiyo kupitia bia ya Kilimanjaro Premeum Lager.
Katika mfululizo wa Wiki ya Simba na Jamii, jana timu hiyo
ilicheza mechi ya kirafiki na Nairobi City Stars ya Kenya Uwanja wa Taifa, Dar
es Salaam na kufungwa mabao 3-1 katika Simba Day.
Lakini kufungwa huko kwa Simba kulitokana na kocha Milovan Cirkovick
kubadilisha karibu kikosi kizima kilichoanza na kuingiza wachezaji wapya
kipindi cha pili, ambao waliitoa City Stars ya Nairobi nyuma kwa 1-0 na kuipa
ushindi wa 3-1.
Simba ilitangulia kupata bao kupitia kwa Felix Sunzu dakika
ya 15, pasi ya Mwinyi Kazimot na ilikwenda kupiumzika ikiwa mbele kwa bao hilo.
Lakini kipindi cha pili, kipa aliyempokea Juma Kaseja,
Hamadi Waziri alitunguliwa mabao matatu katika dakika 57 na Duncan Owiti,
dakika ya 64 na Bruno Okullu na dakika ya 79 na Boniphace Onyango.
Mapema katika tamasha hilo, Simba ilitoa tuzo mbalimbali kwa
wachezaji wa sasa na wa zamani kwa mchango wao kwenye klabu hiyo, pamoja na
baadhi ya wadau wake.
Waliopewa tuzo kwa wachezaji wa sasa, ni Shomary Kapombe
(Nidhamu), Emmanuel Okwi (Mchezaji bora wa msimu) na marehemu Patrick Mfisango
(Heshima).
Wa zamani ni Haidari Abeid ‘Muchacho’ (Mchezaji Bora miaka
ya 1970), Hamisi Kilomoni (Mchezaji Bora Miaka ya 1960), Ally Sykes (Heshima,
Udhamini), Profesa Philemon Sarungi (Mchango wa muda mrefu klabuni) na Gaorge
Kavishe, Meneja wa Kilimanjaro Beer, Wadhamini wa sasa wa Simba SC.
Katika mechi ya kwanza, timu na wanawake ya Simba, Simba
Queens mchana, iliifunga Ever Green ya Temeke mabao 5-3 katika mchezo wa Ligi
ya Wanawake, Dar es Salaam uliokwenda sambamba na tamasha la Simba Day, Uwanja
wa Taifa, Dar es Salaam.
Shujaa wa Simba alikuwa ni Maimuna Hamisi ‘Ronaldo’
aliyefunga mabao matatu, katika dakika za tano, 62 na 64, wakati mabao mengine
ya Malkia wa Msimbazi, walio chini ya kocha Anthony Makunja, yalifungwa na
Grace Tony dakika ya 48 na Neema Kuga dakika ya 59.
Mabao ya Ever Green yalifungwa na Sherida Boniface dakika ya
53, Vumilia Maarifa dakika ya 55 na Amina Siraj dakika ya 61.
![]() |
Viongozi, wachezaji Simba na watoto wa Maunga |
WIKI YA SIMBA NA
JAMII ILIVYOKUWA:
Agosti 5, 2012: Mkutano Mkuu wa mwaka Simba SC (Polisi
Oystrebay)
Agosti 7, 2012: Kutembelea wagonjwa Mwananyamala hospitali
Agosti 8, 2012: Simba 1-3 Nairobi City Stars (Simba Day Uwanja
wa Taifa)
Agosti 9, 2012: Kutembelea watoto yatima Maungu Orphanage
Center
![]() |
Uhuru na mmoja wa watoto wa kituo hicho |
![]() |
Nyosso na mmoja wa watoto wa kituo hicho |
![]() |
Nyagawa na mmoja wa watoto wa kituo hicho |
![]() |
Kaburu na mmoja wa watoto wa kituo hicho |
![]() |
Baadhi ya watoto wa kituo hicho |
![]() |
BIN ZUBEIRY na baadhi ya watoto wa kituo hicho |
![]() |
Mkwabi na mmoja wa watoto wa kituo hicho |
![]() |
Pamba na mmoja wa watoto wa kituo hicho |
![]() |
Nyagawa akikabidhi sembe, ngano na mchele |
![]() |
Nyosso a Uhuru tayari kuondoka baada ya zoezi |
![]() |
Kamwaga na Matari |
![]() |
Baadhi ya watoto wa kituo hicho |
![]() |
Uhuru akikabidhi sabuni |
![]() |
Okwi akikabidhi dawa za kupigia mswaki |
![]() |
Nyosso akikabidhi mafuta |
![]() |
Wachezaji wa Simba na watoto wa kituo hicho |
![]() |
Kaburu akimsikiliza Mama Zainab, mwenye kituo hicho |
![]() |
Dk Kapinga kushoto, kulia Okwi na katikati Nyosso |
![]() |
Mtawala akiwa na Katibu wa kituo hicho kulia na Mama Zainab kushoto |
0 comments:
Post a Comment