![]() |
Bunjak kulia, akiwa na Msaidizi wake Vivek Nagul |
Na Princess Asia
AZAM FC
tayari wako mjini Mwanza na asubuhi hii wanafanya mazoezi kwenye Uwanja wa Chuo
cha Ualimu (TTC), Butimba mjini humo kujiandaa na mechi yao ya pili ya Ligi Kuu
ya Vodacom Tanzania Bara dhidi ya wenyeji Toto African, Uwanja wa Kirumba mjini
humo.
Azam iliyoanza
vema ligi hiyo kwa ushindi wa 1-0 kwenye Uwanja wa Kaitaba, Bukoba, bao pekee
la Abdulhalim Humud dhidi ya wenyeji Kagera Sugar, imepania kuondoka na pointi
zote sita katika mechi zake zote mbili za Kanda ya Ziwa.
Aidha,
mabingwa hao wa Kombe la Mapinduzi kesho watafanya mazoezi kwenye Uwanja
Kirumba, ili kuuzoea kabla ya mchezo wa keshokutwa, ambao unatarajiwa kuwa
mkali na wa kusisimua.
Toto Africans
itahitaji ushindi kwenye mchezo huo, ili kurejesha imani kwa mashabiki wake
baada ya kulazimishwa sare ya 1-1 na JKT Oljoro, katika mchezo wa ufunguzi
Jumamosi.
Kuelekea mchezo
huo, Mserbia anayeinoa Azam, Boris Bunjak ameomba marefa wachezeshe kwa haki,
kwani anaamini vijana wake wanaweza kushinda pale tu sheria 17 zinapotekelezwa
uwanjani na si vinginevyo.
Kocha huyo
aliwalalamikiwa marefa waliochezesha mechi yao ya Ngao ya Jamii na Simba kwamba
waliwabeba mno wapinzani wake, hata wakatoka nyuma kwa 2-0 na kushinda 3-2.
Kwa upande
wake, Kocha wa Toto, John Tegete amesema kwamba baada ya kulazimishwa sare na
Oljoro, Jumatano watapigana kufa na kupona ili kushinda mechi ya kwanza ya Ligi
Kuu.
“Sare ya
juzi kwa kweli hatukuitarajia, tulicheza vizuri, tulipata nafasi nyingi tukapoteza,
lakini kwa siku mbili hizi tutafanyia kazi makosa yetu na Jumatano tunaomba
mashabiki waje kwa wingi kushuhudia mabadiliko, tunawaahidi ushindi,”alisema
baba huyo wa mshambuliaji wa Yanga, Jerry Tegete.
0 comments:
Post a Comment