Sunzu msimu uliopita dhidi ya mabeki wa Yanga, Nadir Haroub na Oscar Joshu nyuma |
Na mahmoud Zubeiry
KOCHA Mkuu wa
Simba SC, Profesa Milovan Cirkovick amesema kwamba anamuhitaji mchezaji ghali
katika timu yake, Mzambia Felix Sunzu kwenye kikosi chake cha kwanza, lakini
anaweza kucheza bila yeye.
Akizungumza juzi
mjini Dar es Salaam, Milo alisema kwamba Sunzu hakumtumia kwenye mechi ya
kwanza ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara dhidi ya African Lyon kwa sababu
alichelewa kurudi Dar es Salaam kutoka kwao Zambia. “Ilikuwa kila siku anasema
atakuja kesho, kesho, haji,”alisema.
Sunzu aliyetua
Dar es Salaam siku moja kabla ya mechi na Lyon, katika kipindi cha takriban
wiki tatu hakuwa na timu, kwanza akienda kwenye msiba wa dada yake Lubumbashi,
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) na aliporejea akaomba ruhusu ya kwenda
kwao Zambia.
Alipoulizwa kama
mchezaji huyo anayelipwa mshahara mkubwa zaidi kuliko wachezaji wote wa klabu
hiyo, dola 3,500 kwa mwezi, zaidi ya Sh. Milioni 5 za Tanzania, ni muhimu kwa
sasa kwenye kikosi chake, Mserbia huyo alisema; “Ndiyo, ni muhimu, namuhitaji,
lakini naweza kucheza bila yeye,”alisema.
Inaonekana sasa
Milo anatiwa jeuri na washambuliaji wake wapya, Mghana Daniel Akuffo, Abdallah
Juma, Salim Kinje, Mrisho Ngassa na wengine ambao yupo nao tangu msimu uliopita
akina Emmanuel Okwi, pamoja na viungo wenye uwezo wa kufunga kama Mwinyi
Kazimoto, Haruna Moshi na wengineo.
Awali ya
hapo, Milo kwa sasa hawatumii mabeki wake wapya, Komabil Keita kutoka Mali na
Paschal Ochieng kutoka Kenya, kwa sababu anataka kwanza waone timu hiyo
inavyocheza wakiwa nje, ili wajifunze.
Profesa huyo
wa Kiserbia alisema kwamba mabeki hao wawili wa kati wanahitaji muda kabla ya
kuanza kucheza kwa mfumo wa Simba, ingawa amewasifia wote ni wazuri.
Alisema
wakati wowote wanaweza kurudi uwanjani, iwe kwa pamoja au kupangwa na wachezaji
wengine na inawezekana hata kwenye mechi ijayo, Jumatano dhidi ya JKT Ruvu,
Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Aidha,
Milovan aliwapongeza wachezaji wake kwa ushindi huo wa juzi na kusema kwamba
hiyo ni zawadi kwa mashabiki wa klabu hiyo. Milo aliwapongeza Lyon pia kwa
kucheza vizuri kwenye safu ya ulinzi na kiungo kidogo na kusema sasa anajipanga
kwa ajili ya mechi ijayo ya ligi hiyo.
Lakini
Mserbia huyo hakusita kuelezea namna alivyokunwa na beki wa kati wa Lyon,
Benedictor Mwamlangala, kwa kucheza kwake vizuri kwenye mechi hiyo.
Simba SC juzi
ilianza vema kampeni za kutetea ubingwa wake wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania
Bara, baada ya kuichapa mabao 3-0 African Lyon katika mchezo wa ufunguzi wa
ligi hiyo, kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Milovan akiwatumia Juma
Nyosso na Shomary kapombe katika beki ya kati.
Hadi
mapumziko, tayari Simba SC walikuwa mbele kwa mabao 2-0 yaliyotiwa kimiani na
Emanuel Okwi dakika ya 33 baada ya kuwatoka mabeki wa Lyon na Nassor Masoud
‘Chollo’ dakika ya 36 akiunganisha krosi ya Mrisho Ngassa.
Lyon
walikosa penalti dakika ya 35, baada ya mkwaju wa Sunday Bakari kupanguliwa na
Juma Kaseja, kufuatia Mwinyi Kazimoto kuunawa mpira kwenye eneo la hatari.
Kipindi cha
pili, Lyon kidogo walirekebisha makosa yao, lakini bado Simba iliendelea
kutawala mchezo na dakika ya 56, Danniel Akuffo aliifungia timu yake bao la
kuhitimisha ushindi kwa mkwaju wa penalti, baada ya Emmanuel Okwi kuangushwa
kwenye eneo la hatari.
0 comments:
Post a Comment