![]() |
| Mtakatifu Tom |
KOCHA wa Yanga, Mbelgiji Tom Saintfiet amesema kwamba wapinzani wake katika mchezo wa kwanza wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara jana, Prisons ya Mbeya walicheza soka ya kuudhi tangu mwanzo, ndiyo maana wakapata sare ya bila kufungana kwenye Uwanja wa nyumbani kwao, Sokoine mjini Mbeya.
Hata hivyo, Saintfiet alisema amejifunza jambo na anayakubali matokeo hayo na sasa anajipanga kwa ajili ya mchezo ujao.
“Ilikuwa mechi ngumu, Prisons walicheza soka ya kuudhi, wakipoteza muda tangu sekunde ya kwanza,”alisema kocha huyo, ambaye hiyo inakuwa sare yake ya kwanza tangu aanze kufundisha Yanga Julai mwaka huu, akiwa ameshinda mechi 11 na kufungwa moja.
Mtakatifu Tom alisema kwamba pamoja na ugumu huo, lakini kipindi cha pili walipata nafasi za kufunga mabao, ila bahati mbaya walishindwa kuzitumia vema na hana cha kulamu kwa sababu katika soka wakati mwingine mambo huwa hivyo.
“Kipindi cha pili tulistahili pointi tatu, Hamisi Kiiza alipiga mashuti matatu mazuri na Simon Msuva pia moja, lakini kipa wa Prisons akaokoa vizuri sana, hatukucheza kwa ubora wetu, lakini siwezi kuwalaumu wachezaji wangu, walipambana, nimesononeka sana,”alisema Mtakatifu alipozungumza na BIN ZUBEIRY kwa simu kutoka Mbeya jana.
Yanga jana ilianza vibaya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, baada ya kulazimishwa sare ya bila kufungana na Prisons kwenye Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya, huku wapinzani wao wakubwa katika mbio za taji, Simba na Azam wakiibuka na ushindi.
Simba iliichapa African Lyon mabao 3-0 Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam wafungaji Emanuel Okwi, Nassor Masoud ‘Chollo’ na Daniel Akuffo, wakati Azam iliichapa Kagera Sugar 1-0 kwenye Uwanja wa Kaitaba, mfungaji Abdulhalim Humud.
Katika mechi nyinginre za ligi hiyo, kwenye Uwanja wa Mkwakwani Tanga, bao pekee la kiungo Mkenya, Jerry Santo dakika ya 41 liliipa Coastal Union ushindi wa 1-0 dhidi ya Mgambo FC.
Uwanja wa Jamhuri, Morogoro, wenyeji Polisi wamelazimishwa sare ya bila kufungana na Mtibwa Sugar ya Turiani, Manungu.
Uwanja wa CCM Kirumba mjini Mwanza, Toto Africans imelazimishwa sare ya 1-1 na JKT Oljoro, wakati Uwanja wa Chamazi, Mbagala, JKT Ruvu imeifunga Ruvu Shooting mabao 2-1.



.png)
0 comments:
Post a Comment