• HABARI MPYA

    Sunday, September 16, 2012

    PROFESA MILOVAN AFICHUA SIRI YA KUWAPIGA MKEKA KEITA, OCHIENG

    Profesa Milovan

    Na mahmoud Zubeiry
    KOCHA wa Simba SC, Milovan Cirkovick amesema kwamba kwa sasa hawatumii mabeki wake wapya, Komabil Keita kutoka Mali na Paschal Ochieng kutoka Kenya, kwa sababu anataka kwanza waone timu hiyo inavyocheza wakiwa nje, ili wajifunze.
    Akizungumza na BIN ZUBEIRY baada ya mechi ya jana, dhidi ya African Lyon, Profesa huyo wa Kiserbia alisema kwamba mabeki hao wawili wa kati wanahitaji muda kabla ya kuanza kucheza kwa mfumo wa Simba, ingawa amewasifia wote ni wazuri.
    Alisema wakati wowote wanaweza kurudi uwanjani, iwe kwa pamoja au kupangwa na wachezaji wengine na inawezekana hata kwenye mechi ijayo.
    Aidha, Milovan aliwapongeza wachezaji wake kwa ushindi huo wa jana na kusema kwamba hiyo ni zawadi kwa mashabiki wa klabu hiyo. Milo aliwapongeza Lyon pia kwa kucheza vizuri kwenye safu ya ulinzi na kiungo kidogo na kusema sasa anajipanga kwa ajili ya mechi ijayo ya ligi hiyo.
    Lakini Mserbia huyo hakusita kuelezea namna alivyokunwa na beki wa kati wa Lyon, Benedictor Mwamlangala, kwa kucheza kwake vizuri kwenye mechi hiyo.
    Simba SC jana ilianza vema kampeni za kutetea ubingwa wake wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, baada ya kuichapa mabao 3-0 African Lyon katika mchezo wa ufunguzi wa ligi hiyo, kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Milovan akiwatumia Juma Nyosso na Shomary kapombe katika beki ya kati.
    Hadi mapumziko, tayari Simba SC walikuwa mbele kwa mabao 2-0 yaliyotiwa kimiani na Emanuel Okwi dakika ya 33 baada ya kuwatoka mabeki wa Lyon na Nassor Masoud ‘Chollo’ dakika ya 36 akiunganisha krosi ya Mrisho Ngassa.
    Lyon walikosa penalti dakika ya 35, baada ya mkwaju wa Sunday Bakari kupanguliwa na Juma Kaseja, kufuatia Mwinyi Kazimoto kuunawa mpira kwenye eneo la hatari. 
    Kipindi cha pili, Lyon kidogo walirekebisha makosa yao, lakini bado Simba iliendelea kutawala mchezo na dakika ya 56, Danniel Akuffo aliifungia timu yake bao la kuhitimisha ushindi kwa mkwaju wa penalti, baada ya Emmanuel Okwi kuangushwa kwenye eneo la hatari.
    Katika mechi nyingine za ligi hiyo jana, Yanga ilianza vibaya kwa kulazimishwa sare ya bila kufungana na Prisons kwenye Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya. Kwenye Uwanja wa Mkwakwani Tanga, bao pekee la kiungo Mkenya, Jerry Santo dakika ya 41 liliipa Coastal Union ushindi wa 1-0 dhidi ya Mgambo FC.
    Uwanja wa Jamhuri, Morogoro, wenyeji Polisi wamelazimishwa sare ya bila kufungana na Mtibwa Sugar ya Turiani, Manungu. Uwanja wa CCM Kirumba mjini Mwanza, Toto Africans imelazimishwa sare ya 1-1 na JKT Oljoro, wakati Uwanja wa Chamazi, Mbagala, JKT Ruvu imeifunga Ruvu Shooting mabao 2-1.
    BENCHI LA UFUNDI; Kutoka kulia Daktari Cossmas Kapinga, Kocha wa makipa, James Kisaka, Kocha Msaidizi, Hamatre Richard (Uganda) na Kocha Mkuu, Profesa Milo kutoka Serbia katika mechi ya jana

    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: PROFESA MILOVAN AFICHUA SIRI YA KUWAPIGA MKEKA KEITA, OCHIENG Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top