• HABARI MPYA

    Sunday, September 16, 2012

    MUARGENTINA WA LYON ALALAMIKA MAREFA WALIIBEBA SIMBA JANA

    Kocha Muargentina wa African Lyon, Pablo Ignacio Velez akiwa na Charles Otieno, Mkurugenzi wa Ufundi wa klabu hiyo katika mechi ya jana dhidi ya Simba.
    Na Prince Akbar
    KOCHA Mkuu wa African Lyon, Muargentina Pablo Ignacio Velez amewalaumu marefa waliochezesha mechi yao ya ufunguzi ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara dhidi ya Simba SC jana Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, kwamba waliwapendelea wapinzani wao hao.
    Akizungumza na BIN ZUBEIRY jana baada ya mechi hiyo, ambayo walichapwa mabao 3-0, Velez alisema kwamba timu yake ilicheza vizuri na ilipoteza nafasi ikiwemo penalti, lakini pia marefa walichangia kuiangusha.
    Marefa waliochezesha mechi hiyo jana ni Orden Mbaga, aliyesaidiwa na Hamisi Chang’walu na Shafii Mohamed, wakati refa wa akiba alikuwa Hashim Abdallah, wote wa Dar es Salaam.
    “Nimekuja hapa kufanya kazi ya muda mrefu, na kila siku napambana kuweka mambo sawa, yote yaliyotokea uwanjani leo, nayachukua mimi, mimi ndiye kocha wa African Lyon,”alisema Muargentina huyo.
    “Tumecheza na timu nzuri na makosa tuliyofanya ndio yametugharimu, kwanza Simba wakiwa wanaongoza 1-0, tukapata penalti, lakini beki wetu wa pembeni, Sunday akapoteza. Lakini pale Chollo alicheza rafu mbaya, na alistahili kupewa kadi nyekundu ya moja kwa moja na sisi tukapewa faulo.
    Na pale nje nilimuona mshika kibendera kama anataka kunyoosha, lakini akasita. Mimi nimecheza mpira, na napenda niseme, kama refa angepiga filimbi ya faulo ya Chollo, tusingefungwa bao la pili. Kipindi cha pili, ile penalti ya Simba, refa alikuwa umbali wa mita 40 na mpira ulikuwa miguuni mwa mchezaji wangu Jacob Masawe, alipulizaje ile filimbi?”alihoji Velez.
    Simba SC jana ilianza vema kutetea ubingwa wake wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, baada ya kuichapa mabao 3-0 African Lyon katika mchezo wa ufunguzi wa ligi hiyo, kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Milovan akiwatumia Juma Nyosso na Shomary kapombe katika beki ya kati.
    Hadi mapumziko, tayari Simba SC walikuwa mbele kwa mabao 2-0 yaliyotiwa kimiani na Emanuel Okwi dakika ya 33 baada ya kuwatoka mabeki wa Lyon na Nassor Masoud ‘Chollo’ dakika ya 36 akiunganisha krosi ya Mrisho Ngassa.
    Lyon walikosa penalti dakika ya 35, baada ya mkwaju wa Sunday Bakari kupanguliwa na Juma Kaseja, kufuatia Mwinyi Kazimoto kuunawa mpira kwenye eneo la hatari. 
    Kipindi cha pili, Lyon kidogo walirekebisha makosa yao, lakini bado Simba iliendelea kutawala mchezo na dakika ya 56, Danniel Akuffo aliifungia timu yake bao la kuhitimisha ushindi kwa mkwaju wa penalti, baada ya Emmanuel Okwi kuangushwa kwenye eneo la hatari.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: MUARGENTINA WA LYON ALALAMIKA MAREFA WALIIBEBA SIMBA JANA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top