|  | 
| Azam FC | 
Na Mahmoud Zubeiry
SIMBA SC
inashuka dimbani kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kumenyana na Azam FC
katika mechi ya kuwania Ngao ya Jamii, iliyopangwa kuanza saa 10:30 jioni.
Simba itakayotokea
katika hoteli ya Sapphire, Kariakoo itashuka dimbani ikiwa na kumbukumbu ya
kuchapwa mabao 3-0 na Sofapaka ya Kenya, katika mchezo wa kirafiki, Alhamisi
iliyopita kwenye Uwanja huo huo.
Lakini awali
ya hapo, Simba ilicheza mechi tatu za kirafiki ikiwa kambini Arusha, dhidi ya
Mathare United ya Kenya, JKT Oljoro ya Arusha ambazo kila moja ilishinda 2-1,
kabla ya kulazimishwa sare ya 1-1 na Sony Sugar ya Kenya.  
Habari njema
zaidi mshambuliaji hatari wa Simba SC, Emanuel Arnold Okwi alitua juzi kutoka
Zambia, ambako aliichezea timu yake ya taifa, Uganda, The Cranes mechi ya
kuwania tiketi ya kucheza Fainali za Mataifa ya Afrika mwakani Afrika Kusini
jana na kufungwa 1-0 kwa mbinde na leo anatarajiwa kucheza.  
Okwi
hajaichezea Simba mechi yoyote tangu msimu huu uanze, kutokana na pilika zake
za kujaribu kuhamia Ulaya, ambazo hazikufanikiwa. 
Mshambuliaji
wake mwingine, Mzambia Felix Sunzu ambaye kwa wiki nzima yuko kwao kwenye msiba
wa dada yake, alirejea jana na jioni alifanya mazoezi, tayari kwa mechi ya leo.
Lakini Simba
pia inajivunia mshambuliaji wake kutoka Ghana, Daniel Akuffo ambaye hadi sasa
katika mechi nne za kirafiki, amefunga mabao matatu, ingawa hiyo ambayo
hakufunga, dhidi ya Sofapaka hakumaliza hata nusu ya kwanza ya mchezo, baada ya
kuumia na kutoka. 
Viungo
Mrisho Khalfan Ngassa na Ramadhan Suleiman Chombo ‘Redondo’ kwa mara ya kwanza
leo watacheza dhidi ya timu yao ya zamani- wote hawa waliichezea Azam
ilipoifunga Simba 3-1 katika Robo Fainali ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na
Kati, Kagame Julai 24, mwaka huu Uwanja wa Taifa.
Azam itakayotokea
Chamazi, nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam, itaingia uwanjani ikiwa na
kumbukumbu nzuri ya kushinda mechi zake zote nne za kujipima nguvu, dhidi ya
Prisons 1-0, Transit Camp 8-0, Coastal Union 2-0 na Azam Akademi 4-0.
John Bocco
‘Adebayor’ aliyefunga mabao yote matatu Simba ilipokutana na Azam mara ya mwisho
na mwenye kawaida ya kufunga kila mechi baina ya timu hizo, leo kwa mara
nyingine atakuwa tishio kubwa kwa Wekundu wa Msimbazi, akicheza mbele ya kiungo
bora kwa sasa Afrika Mashariki, Salum Abubakar ‘Sure Boy Jr.’.
Beki wa
zamani wa Simba SC, Mganda Joseph Owino bado hajamshawishi kocha mpya wa Azam,
Boris Bunjak na hapana shaka leo Said Mourad atacheza pamoja na Aggrey Morris
katika beki ya kati, juu yao akisimama Jabir Aziz na Abdi Kassim ‘Babbi’
anaweza kuanza na Adebayor pale mbele.
Kihistoria
hiyo itakuwa mechi ya tano ya Ngao ya Jamii kuchezwa nchini na ya pili
kuishirikisha timu nje ya wapinzani wa jadi wa soka ya Tanzania, Simba na
Yanga.
Mtibwa
ilicheza na Yanga mwaka 2009, baada ya Simba kugoma na ikashinda mabao 2-1 na
kutwaa Ngao, wakati kabla ya hapo, mwaka 2001, Ligi Kuu ya Tanzania ikiwa bado
inadhaminiwa na Kampuni ya Bia Tanzania (TBL), kupitia bia ya Safari Lager,
ilichezwa mechi ya kwanza ya Ngao kihistoria.
Katika mechi
hiyo, Yanga ilishinda mabao 2-1 dhidi ya Simba na mwaka juzi Yanga iliifunga
tena Simba kwa penali 3-1 kufuatia sare ya 0-0 na mwaka jana, Simba ilitwaa
Ngao ya kwanza katika historia yake, kwa kuifunga Yanga mabao 2-0.
Ikumbukwe
mara ya mwisho Simba SC ilipokutana na Azam FC, katika Robo Fainali ya Klabu
Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame, Julai mwaka huu, Dar es
Salaam, ilifungwa mabao 3-1, yote yakifungwa na Bocco na lile la kufutia
machozi kwa wekundu hao Msimbazi liliwekwa kimiani na kiraka Shomari Kapombe.  
|  | 
| Simba SC | 
Vikosi
vya leo; 
Simba SC; Juma Kaseja, Nassor Masoud ‘Chollo’, Amir Maftah, Juma
Nyosso, Paschal Ochieng, Shomary Kapombe, Mrisho Ngassa, Mwinyi Kazimoto, Felix
Sunzu, Daniel Akuffo na Emanuel Okwi. 
Azam FC; Deo Munishi ‘Dida’, Ibrahim Shikanda, Erasto Nyoni, Said
Mourad, Aggrey Morris, Jabir Aziz, Kipre Michael Balhou, Salum Abubakar, John
Bocco, Abdi Kassim na Kipre Herman Tchetche.
REKODI
YA SIMBA NA AZAM
Julai 24, 2012
Simba 1-3 Azam (Robo Fainali Kagame) 
Julai 12, 2012
Simba 2-2 Azam (Fainali Urafiki Cup)
(Simba ilishinda kwa penalti 3-1)
Februari 11, 2012
Simba SC 2 - 0 Azam FC
Sept 11, 2011
Azam FC 0 - 0 Simba SC
Jan 23, 2011     
Simba 2-3 Azam (Dar).               
Sep 11, 2010
Azam 1-2 Simba (Tanga).
Machi 14, 2010
Azam 0-2 Simba (Dar)  
Okt 24, 2009
Simba 1-0 Azam (Dar)          
Machi 30, 2009
Azam 0-3 Simba (Dar)   
Okt 4, 2008
Simba 0-2 Azam  
MABINGWA WA MECHI ZA NGAO YA JAMII:
Mwaka          Mshindi   Matokeo 
2001               Yanga       2-1 Simba 
2009 Mtibwa 2-1 Yanga
2009 Mtibwa 2-1 Yanga
2010               Yanga       0-0 Simba (3-1penalti)
2011               Simba       2-0 Yanga
 
 
 
 
%202.png) 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 


.png)
 
0 comments:
Post a Comment