![]() |
| Waziri wa Kazi na Ajira, Makongoro Mahanga akimkabidhi Nahodha wa Simba, Juma Kaseja Ngao ya Jamii juzi, Uwanja wa Taifa. |
Na Prince Akbar
SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF) litatoa vifaa vyenye
thamani ya sh. milioni 7.3 kwa Hospitali ya Temeke mkoani Dar es Salaam ambazo
ni asilimia 5 ya Sh. Milioni 146 ya fedha zilizopatikana kwenye mechi ya Simba
na Azam.
Mechi hiyo ya Ngao ya Jamii (Community Shield) kuashiria
ufunguzi wa msimu mpya wa 2012/2013 ilichezwa juzi (Septemba 11 mwaka huu)
Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na kuingiza sh. 146, 640,000. Washabiki 26,001
walikata tiketi kushuhudia mechi hiyo ambayo ilimalizika kwa Simba kushinda
mabao 3-2.
Sekretarieti ya TFF inatarajia kukutana na uongozi wa
Hospitali ya Temeke wakati wowote kuanzia leo ili kujua mahitaji halisi kabla
ya kufanya ununuzi wa vifaa husika.
Mgawanyo wa mapato ya mechi hiyo uliokuwa kama ifuatavyo;
asilimia 18 ya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) sh. 22,368,813.56, asilimia 5
ya mchango wa kusaidia jamii (Hospitali ya Temeke) sh. 7,332,000, uwanja sh.
10,148,318.64, Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) sh.
4,059,327.46, TFF sh. 10,148,318.46 na Mfuko wa Maendeleo ya Mpira wa Miguu
(FDF) sh. 5,074,159.32.
Baraza la Michezo la Taifa (BMT) sh. 1,014,831.86, kila timu
sh. 32,265,025.93, asilimia 10 ya gharama za mchezo sh. 10,148,318.64, nauli
kwa waamuzi na kamishna sh. 80,000, posho ya kujikimu kwa waamuzi na kamishna
230,000, posho ya waamuzi 400,000, tiketi sh. 4,495,800, maandalizi ya uwanja
(pitch) sh. 400,000, umeme sh. 300,000, usafi na ulinzi uwanjani sh. 2.350,000
na Wachina (Beijing Construction) sh. 2,000.000.
Mchango wa kusaidia jamii kwenye mechi ya Ngao ya Jamii
kuzindua msimu uliopita kati ya Yanga na Simba ulikuwa sh. 15,000,000 ambazo
zilikwenda Chama cha Madaktari Wanawake Tanzania (MEWATA) kusaidia uchunguzi wa
kansa ya matiti kwa akina mama.
Wakati huo huo: Kamati ya Utendaji ya TFF iliyokutana jana
(Septemba 12 mwaka huu) jijini Dar es Salaam imepitisha marekebisho ya kanuni
kwa ajili ya Ligi ya Mkoa na Ligi ya Wilaya.
Marekebisho hayo yametokana na mabadiliko ya mfumo wa
mashindano uliofuta Ligi ya Taifa. Hivi sasa kutakuwa na Ligi Kuu, Ligi Daraja
la Kwanza, Ligi ya Mkoa na Ligi ya Wilaya.
Kutokana na marekebisho hayo ya kanuni; Ligi ya Wilaya
itaendeshwa na Vyama vya Mpira wa Miguu vya Wilaya (DFAs), Ligi ya Mkoa
itaendeshwa na Vyama vya Mpira wa Miguu vya Mikoa (RFAs).
Mechi za mchujo (play offs) kutafuta timu zitakazopanda
kwenda Ligi ya Mkoa zitaendeshwa na RFAs wakati play offs za kupanda Ligi
Daraja la Kwanza zitakazohusisha mabingwa wa mikoa zitasimamiwa na TFF. Ligi za
madaraja yote zitachezwa mwaka mzima kwa mtindo wa nyumbani na ugenini.



.png)
0 comments:
Post a Comment