• HABARI MPYA

    Wednesday, September 12, 2012

    SIMBA YAMTUPIA VIRAGO OBADIA AKIWA MGONJWA

    Obadia kushoto, akiwa na Mussa Mudde kulia. kama walijijua

    Na Mahmoud Zubeiry
    TIMUA timua imeendelea Simba SC na safari ni zamu ya beki Obadia Michael Mungusa. Beki huyo wa zamani wa Mtibwa Sugar akiwa anaingia katika msimu wa pili kwenye klabu hiyo, ametemwa.
    Habari kutoka ndani ya Simba SC, ni kwamba beki huyo ametemwa kwa zaidi ya mwezi mmoja, ingawa inafanywa siri kwa kile ambacho viongozi wa klabu hiyo wanaelewa.
    Lakini ajabu Simba inamtema Obadia, wakati ina uhaba wa mabeki wa kati, kwani inao watatu tu, Juma Nyosso, Paschal Ochieng na Komabil Keita, hali ambayo imefanya sasa Shomary Kapombe ahamishiwe kwenye nafasi hiyo.
    BIN ZUBEIRY ilimtafuta Obadia ambaye alisema kwamba yeye anajitambua ni mchezaji halali wa Simba SC, kwa kuwa bado ana mkataba na klabu hiyo wa mwaka mmoja zaidi, ila kwa sasa hayupo na timu kwa kuwa anaumwa.  
    “Mimi nilikuwa naumwa, viongozi wakawa hawaamini, nimecheza Kombe la Kagame naumwa, baada ya mashindano, ikabidi niende Mwanza kujitibu, wao wakasema nisiondoke hadi daktari anitazame, wakati ule daktari alikuwa hayupo, nikaamua kuondoka tu, kwa sababu hali yangu ilikuwa mbaya.
    Wakanipigia simu kunihoji mbona umeondoka bila kuongea na daktari, ikabidi nirudi Dar es Salaam, wakati huo timu inakwenda Arusha kambini, Daktari akaniambia niende kwa daktari mmoja Dar es Salaam nikapimwe.  Nilipoenda kupimwa yule, daktari akasema kuna kipimo natakiwa kufanyiwa, akawasiliana na viongozi, akawa anasubiri jibu. Ila wakawa wanamzungusha.
    Mimi nikawapigia simu viongozi kuwauliza, nikaambiwa ooh sijui sina mapenzi na timu mara wanasikia eti nasema siwezi kwenda kambini kwa sababu nadai hela, kweli kuna haki zangu nadai, lakini siwezi kugoma kufanya kazi kinyume na utaratibu, mimi ninaumwa. Basi ndio hivyo, ikawa mabishano yakaishia hapo,”alisema Oba.
    Hata hivyo, kuhusu habari za kuachwa, Obadia anasema litakuwa jambo la alabu sana, kwa kuwa awali yeye aliomba kuachwa baada ya msimu uliopita wa Ligi Kuu kumalizika, ili atafute timu nyingine, lakini viongozi wakamkatalia.
    “Nilipomaliza ligi nilipata nafasi sehemu nyingine, mimi nilipokuwa Mtibwa nilikuwa nacheza. Nimekuja Simba nikawa sichezi, nikawaambia viongozi, kama wanaona bado sina nafasi, bora waniache niende. Wakaniambia nina mkataba siwezi kuondoka na kama kuna timu inanitaka ije kuvunja mkataba.
    Nikawoamba wanipeleke sehemu hata kwa mkopo niwe nacheza, wakanihakikishia kucheza, kweli Kagame imekuja nimeanza kucheza, bahati mbaya nikaumia, ndio nimekuja kujitibu sasa yanaibuka haya tena, ila mimi bado ninajitambua ni mchezaji halali wa Simba, kuwa kuwa nina mkataba,”alisema Oba.
    Lakini kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba SC, Zacharia Hans Poppe alisema anachofahamu kuhusu mchezaji huyo aliomba mwenyewe kurudi Mtibwa na kulingana na taarifa yake ya uchezaji msimu uliopita, Kamati yake ikaafiki ombi hilo.
    “Mimi nachofahamu kutoka kwa uongozi, huyu mchezaji aliomba kurudi Mtibwa na kulingana na taarifa yake ya uchezaji msimu uliopita, tukaridhia ombi lake,”alisema Hans Poppe.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: SIMBA YAMTUPIA VIRAGO OBADIA AKIWA MGONJWA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top