![]() |
Na Bin Zubeiry |
BAADA ya ziara ya wiki mbili nchini Uturuki, Jumamosi wiki
hii Yanga watacheza mchezo wa kujipima nguvu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam
dhidi ya Black Leopard inayosuasua kwenye Ligi Kuu ya Afrika Kusini.
Black Leopard yenye maskani yake Polokwane, Limpopo nchini Afrika
Kusini kwa sasa inashika nafasi ya 12 katika Ligi Kuu ya Afrika Kusini na msimu
uliopita ilinusurika kushuka Daraja, ikishika nafasi ya 14 katika Ligi ya timu
16.
Leopards ilirejea Ligi Kuu ya Afrika Kusini mwaka juzi tangu
ishuke 2008 na huwezi kuichukulia kama timu ya ushindani kulingana na matokeo
yake.
Kwa mujibu wa Waratibu wa mechi hiyo, kampuni ya Prime Time
Promotions ya Dar es Salaam, Leopard itawasili nchini kesho tayari kwa mchezo
huo.
Yanga ilikuwa Uturuki kwa wiki mbili kwa kambi ya mazoezi na
imerejea leo Alfajiri nchini. Katika ziara yake hiyo, ilicheza mechi tatu za
kujipima nguvu na kufungwa mbili na kutoka sare moja.
Katika mchezo wake wa kwanza, ilitoka sare ya 1-1 Ariminia
Bielefeld ya Daraja la Tatu (sawa na la nne) Ujerumani kabla ya kufungwa 2-1 na
Denizlispor FC ya Daraja la Kwanza Uturuki na baadaye 2-0 na Emmen FC ya Ligi
Daraja la Kwanza Uholanzi.
Yanga iliweka kambi katika hoteli ya Fame Residence Lara
& Spa kilomita chache kutoka katika Uwanja wa Ndege wa Jiji la Antalya, iliyopo
ufukweni mwa bahari ya Mediteranian.
Kikosi cha wachezaji 27 kilikuwa kambini nchini Uturuki,
ambacho ni makipa; Ally Mustafa 'Barthez', Said Mohamed na Yussuf Abdul, mabeki
Juma Abdul, Shadrack Nsajigwa, Godfrey Taita, Stefano Mwasyika, Oscar Joshua,
Mbuyu Twite, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Ladisalus Mbogo na Kelvin Yondani.
Viungo ni Athumani Iddi ‘Chuji’, Frank Domayo, Haruna
Niyonzima, Kabange Twite, Nurdin Bakari, Omega Seme, Simon Msuva, Rehani
Kibingu, Nizar Khalfani na David Luhende wakati washambuliaji ni Didier
Kavumbagu, Said Bahanunzi, Jerry Tegete, George Banda na Hamisi Kiiza na Kocha
Mkuu Mholanzi, Ernie Brandts, Kocha Msaidizi, Freddy Felix Minziro na Kocha wa
makipa na Razak Ssiwa.
Hiyo inakuwa mara ya tatu kihistoria Yanga kufanya ziara nje
ya Afrika baada ya Brazil mwaka 1975 na Romania mwaka 1978. Yanga pia imewahi
kuweka kambi Afrika Kusini mwaka 2008.
Ikumbukwe kabla ya Yanga kwenda Uturuki, ilielezwa imesaini
Mkataba na Prime Times na kupewa Sh. Milioni 105 ili iandaliwe mechi za
kujipima nguvu pamoja na Mkutano Mkuu.
Sahau kuhusu aina ya mkataba kama unainufaisha au unainyonya
Yanga, watajua wenyewe viongozi waliopewa dhamana na wanchama, lakini
inafahamika klabu hiyo inaweza kuingiza Sh. Milioni 300 au zaidi katika mechi
moja tu.
Ni matarajio ya wengi, baada ya ziara ya Uturuki, Yanga
wangeandaliwa mechi dhidi ya timu maarufu, ya ushindani barani ili kuwapatia
burudani mashabiki wake.
Mfano tu huko Afrika Kusini, kuna timu maarufu kama Kaizer
Chiefs, Orlando Pirates, Santos, SuperSport United na nyingine ambazo zina
rekodi ya kucheza michuano ya Afrika na Watanzania wanazifahamu.
Lakini ajabu inaletwa timu ambayo kwa msimu wa pili mfululizo
sasa inapigania kuepuka balaa la kushuka daraja.
Kama ni mechi tu bora mechi ni sawa, lakini kwa maana ya
mechi bora haiwezi kuwa kwa Yanga dhidi ya vibonde hao wa Ligi Kuu ya Afrika
Kusini.
Yanga imewekeza fedha nyingi katika ziara yake ya Uturuki na
baada ya hapo, ilitakiwa kupata mechi ya kusisimua ili mashabiki wake wapime
uwezo wa wachezaji wao na waweze kujua wamevuna nini kwenye ziara hiyo ya Ulaya.
Lakini badala yake wanaletewa katimu ambako Watanzania
wamekasikia kwa mara ya kwanza kama nako kapo katika dunia ya soka.
Au kama timu zilikosekana Afrika Kusini, kwanini hao Waratibu
wasihamishie mawindo yao nchi nyingine, ili kupata timu bora, kuliko
kulazimisha halafu kanaletwa katimu, ambako hakawezi kuvuta hisia za mashabiki?
Yanga wanatakiwa kucheza mechi ambayo itavuta hata hisia za
mashabiki wengi wa wapinzani wao, Simba SC na hiyo itawasaidia kupata mapato
mengi kwenye mchezo huo.
Lakini kwa haka katimu kanakoletwa, sana watakwenda wale
‘Yanga oyee oyee’, ila wana Yanga wenye kujua na kufuatilia vema soka na
wapenzi wa Simba wataipuuza tu mechi hiyo.
Mapema nilisema Yanga wana fursa nzuri ya kuiandaa timu yao
kabla ya kurejea kwenye michuano ya Afrika mwakani, ili watengeneze timu bora
ya ushindani na waweze kufika mbali.
Yanga lazima wajipime na timu zinazowazidi uwezo ili wajue
ubora halisi wa timu yao kulingana na changamoto ambazo watakutana nazo katika
michuano ya Afrika.
Lakini Black Leopard, Yanga itashinda 5-0 na magazeti
yatasifia, mwakani inatoka ratiba wanapangwa Zamalek, majanga! Umefika wakati
sasa viongozi wa klabu zetu watumie hata uzoefu wa historia katika kuamua na
kupanga mambo kwa manufaa ya klabu.
Sasa hebu tujiulize, hiki ni kitimu gani ambacho kinacheza na
Yanga Jumamosi? Kwa kitimu kama hiki, ni bora Yanga wangecheza hata Coastal
Union au Mtibwa Sugar zingewapa changamoto nzuri.
Yanga watambue wako nyuma sana kimafanikio katika michuano ya
Afrika na wanaachwa mbali sana na wapinzani wao wa jadi Simba SC.
Mafanikio makubwa ya Yanga katika soka ya Afrika ni kucheza
Robo Fainali, wakati wenzao Simba SC wana rekodi ya kucheza hadi fainali ya
michuano ya Afrika.
Hata ukienda kwenye ushindani wa wenyewe kwa wenyewe hapa
nyumbani, Simba SC wana rekodi ya kuifunga Yanga SC mabao mengi katika mechi
moja, 6-0 jambo ambalo linatokana na ubora wa timu.
Kwa staili hii wanayotaka kwenda nayo Yanga, wasitarajie japo
kulipa 5-0 za mwaka jana walizopigwa na Simba SC. Lazima Yanga wabadilike na
wakubali kucheza mechi ngumu, ili kupima uwezo halisi wa timu yao. Kwa leo.