![]() |
Wachezaji wa Azam |
Na Mahmoud Zubeiry
MECHI ya kwanza ya Raundi ya Pili ya Kombe la Shirikisho la Soka Afrika, kati ya wenyeji Barack Young Contollers na Azam FC ya Dar es Salaam, itachezwa Jumapili saa 10:00 za Liberia kwenye Uwanja wa Antonette Tubman mjini Monrovia na si kesho kama ilivyopangwa awali.
Ratiba ya mashindano ya Shirikisho awali ilikuwa inaonyesha mechi hiyo itachezwa kesho, lakini kocha Muingereza wa Azam, Stewart Hall ameiambia BIN ZUBEIRY leo kwamba, mechi hiyo itachezwa Jumapili kuanzia saa 10:00 za huko, ambayo ni sawa na saa 1:00 usiku kwa Afrika Mashariki.
Stewart amesema timu yake inaendelea vizuri nchini humo na vijana wake wanampa matumaini ya kushinda mchezo huo keshokutwa, licha ya kucheza ugenini.
Wawakilishi hao wa Tanzania katika Kombe la Shirikisho Afrika, jana walilazimika kujilipia wenyewe hoteli mjini Monrovia kwa siku zote watakazokuwa nchini Liberia kwa ajili ya mchezo huo kufuatia kutoridhishwa na mazingira na hadhi ya hoteli kwa ujumla waliyopewa na wenyeji wao kuelekea mchezo huo wa kesho.
Hall alisema kwamba wenyeji waliwapangia hoteli iitwayo Crystal lakini kwa bahati mbaya baada ya kuikagua hawakuridhika nayo.
“Ulikuwa mgogoro mkubwa ikabidi twende hadi FA (chama chao cha soka), lakini B.Y.C. wakasistiza hoteli ile imepaasishwa na CAF (Shirikisho la Soka Afrika) na hawataibadili,”alisema Hall.
Kutokana na hali hiyo, Hall alisema uongozi uliamua kuingia gharama za kujipangia hoteli na hivyo wakahamia katika hoteli iitwayo Golden Key. “Hapa sasa safi, panaridhisha,”alisema.
Hall alisema jana walifanya mazoezi katika Uwanja wa mazoezi wa wenyeji wao hao na leo wanatarajiwa kufanya mazoezi kwenye Uwanja wa Antonette Tubman, ambao utatumika kwa mechi hiyo.
Azam FC iliyoondoka nchini Jumatano na kufika juzi hiyo hiyo, imetua nchini humo na kikosi cha wachezaji 22, ambao ni makipa; Mwadini Ally na Aishi Manula, mabeki; Joackins Atudo (Kenya), David Mwantika, Himid Mao, Malika Ndeule, Waziri Salum na Luckson Kakolaki.
Kwa upende wa viungo ni Abdulhalim Humud, Kipre Balou (Ivory Coast), Jabir Aziz, Ibrahim Mwaipopo, Salum Abubakar, Humphrey Mieno (Kenya), Abdi Kassim ‘Babbi’, Uhuru Suleiman na Khamis Mcha ‘Vialli’ wakati washambuliaji ni John Bocco ‘Adebayor’, Kipre Tchetche (Ivory Coast), Seif Abdallah, Brian Umony (Uganda) na Gaudence Mwaikimba.
Barrack Young Controllers inayomilikiwa na jeshi la nchini humo, iliyoanzishwa mwaka 1997, inatumia Uwanja wa Antonette Tubman uliopo mjini Monrovia kwa mechi zake na haina tofauti sana na Azam kihistoria.
Wakati Azam ilianzishwa mwaka 2004 na kucheza Ligi Kuu ya nchi kwa mara ya kwanza mwaka 2008, hadi sasa ina mataji mawili ya Kombe la Mapinduzi na moja la Kombe la Hisani ya nchini DRC, wapinzani wao wana mataji mawili ya Kombe la Liberia na moja la Super Cup ya nchini humo.
Azam ni timu pekee ya Tanzania iliyobaki kwenye michuano ya Afrika baada ya Simba na Jamhuri ya Pemba kutolewa katika Raundi ya Kwanza tu ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Azam inayomilikiwa na Alhaj Said Salim Awadh Bakhresa na faimili yakle, ilifuzu kuingia Raundi ya Pili ya michuano hiyo, baada ya kuichapa jumla ya mabao 8-1 Al Nasir Juba ya Sudan.