• HABARI MPYA

    Friday, June 14, 2013

    ABDALLAH MSAMBA ALIYEKUWA MAMBA WA FAHNBULLAH SIMBA SC...

    IMEWEKWA JUNI 14, 2013 SAA 4:00 ASUBUHI
    "MSHAMBULIAJi wa Kiliberia, William Fahnbbullar alikuwa anapenda sana krosi za Abdallah Msamba walipokuwa naye Simba SC mwishoni mwa miaka ya 1990 kwa sababu alikuwa anazitumia vizuri kufunga mabao.
    Lakini tabu moja tu, alikuwa anashindwa kutamka jina Msamba na akawa anaita ‘Mambaa’- kila alipomuita kuomba pasi.
    Msamba

    Hawa wawili walikuwa rafiki sana pale Simba SC na Msamba ndiye aliyemvutia Fahnbullah Tanzania Stars. Sijui na sina uhakika kama Willy atapata taarifa za msiba wa Abdallah. Na akipata sijui atazipokeaje.
    Kwa sauti yake laini ya upole, wakiwa mazoezini kwa kila jambo, hata akichokozwa Fahnbullah alikuwa anamshitakia Msamba. Ameondoka mtetezi wake. Ameondoka swahiba wake. Ametangulia mbele ya haki kufuatia kifo chake usiku wa kuamkia jana Dar es Salaam na anazikwa leo Makaburi ya Magomeni Makuti, Dar es Salaam.
    Nitaanzaje kumuelezea marehemu Msamba. Labda Thomas Kipese au Abubakar Kombo wangekuwa karibu yangu tungekumbushana, lakini kitu kimoja nachoweza kusema, alikuwa mtu safi, asiye na makuu na mwenye uwezo mkubwa uwanjani.
    Lakini Msamba ni kati ya wachezaji ambao hawakunufaika na maslahi makubwa enzi zao wanacheza- ila bado aliendelea kucheza kwa bidii kwa sababu aliipenda soka kutoka moyoni.
    Nilipotezana na huyu mtu kwa muda mrefu sana kwa kweli, ila nilikuwa napata taarifa zake kwamba alihama Tabata hadi Mbezi ya Kimara. 
    Mtu wa kwanza kunipigia simu kunijulisha juu ya kifo cha Msamba alikuwa Madaraka Suleiman ‘Mzee wa Kiminyio’. Ndiyo alikuwa anajua Msamba alikuwa ‘best wangu’.
    Msamba ni kati ya wachezaji walionisaidia sana kuwa Mwandishi wa aina yangu- mwenye wapenzi na mashabiki kwa sababu ya kazi hii. Alinipa ushirikiano sana. Tulipokuwa tunakutana, mimi Abubakar Kombo, Thomas Kipese na Abdallah Msamba, hapo ni zaidi ya mambo ya mpira.  
    Mwenzetu ameondoka na leo tunamzika Magomeni Makuti. 
    Tutafanya nini na tunajua ni kazi yake Mola kama alivyoimba Madee wa Tip Top Connection, haina makosa, anafanya atakalo, anafanya awezalo, kwani dunia ni yake na hakuna ashindwalo. Tangu nilipopata habari za msiba wa Msamba jana nilifadhaika sana na nimekuwa nikitumia uzoefu tu kufanya yote niliyoyafanya tangu hapo, ila siko vizuri. 
    Msiba huu umeniumiza sana. Msamba ni kati ya rafiki zangu niliopotezana nao, ambao niliamini nitakutana nao tena, kwani milima haikutani, lakini binadamu tunakutana. Basi tena. Hadi akhera. Mungu amsamehe dhambi zake za dunia na aipumzishe kwa amani roho yake. Amin,". 
    Na Mahmoud Zubeiry.   
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: ABDALLAH MSAMBA ALIYEKUWA MAMBA WA FAHNBULLAH SIMBA SC... Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top