• HABARI MPYA

    Tuesday, June 11, 2013

    BREAKING NEWS; AMRI KIEMBA ASAINI MIAKA MIWILI SIMBA SC MCHANA HUU

    Hadi 2015  Msimbazi; Amri Kiemba amesaini miaka miwili leo Simba SC
    Na Mahmoud Zubeiry, IMEWEKWA JUNI 11, 2013 SAA 9:30 ALASIRI
    HATIMAYE kiungo Amri Ramadhani Kiemba amesaini Mkataba mpya na Simba SC mchana wa leo kuendelea kuichezea klabu hiyo kwa miaka miwili, hivyo kuzima tetesi kwamba alikuwa mbioni kurejea klabu yake ya zamani Yanga SC.
    Akizungumza na BIN ZUBEIRY mchana huu, Kiemba amesema amesaini mbele ya Kaimu Mwenyekiti wa Simba SC, Joseph Itang’are ‘Kinesi’ mchana huu.
    “Unajua mimi si muongeaji, wakati magazeti yanaandika mimi nimesaini Yanga nilikuwa nashangaa sana. Ila sikutaka kujibu, sasa ukweli ni huu nakupa Bin Zubeiry, nimesaini Simba kwa miaka miwili zaidi,”alisema.
    Amesema kwa sasa anaelekeza nguvu zake katika kambi ya timu ya taifa, Taifa Stars na anaamini mjadala wa Kiemba umekwisha salama, sasa ni zamu ya wengine.
    Kiemba amesaini SImba SC leo ikiwa ni siku moja tu tangu arejee nchini kutoka Morocco alipokuwa na timu ya taifa, Taifa Stars.
    Kiemba yuko juu kwa sasa kisoka na alikuwa lulu Morocco kutokana na kuifungia Tanzania, Taifa Stars bao la kufutia machozi ikilala 2-1 mbele ya wenyeji, Simba wa Atlasi Jumamosi Uwanja wa Marakech, Morocco.  
    Baada ya mchezo huo, mashabiki wa soka Morocco walianza kumfuatafuata Kiemba wakiomba kupiga naye picha na walimtambua rahisi kwa sababu ya rasta zake.
    Kiemba aliendelea kusumbuliwa na Wamorocco hadi hotelini Pullman Stars ilipifikia na hadi wakati Stars inaondoka Marakech, madereva teksi wa hotelini hapo, walimuomba kupiga naye picha.
    Hali hiyo iliendelea hadi Stars ilipotua Casablanca kwa ajili ya kupanda ndege kurejea Dar es Salaam na Kiemba hakuwafanyia hiana aliwapa ushirikiano na kwa ujumla Waarabu walimfuruhia mno kiungo huyo. 
    Kabla ya mchezo, mchezaji ambaye Waarabu walikuwa wanamtaja na kumuulizia sana alikuwa Mbwana Ally Samatta aliyewafunga mabao mawili katika ushindi wa Stars wa 3-1 Dar es Salaam.
    Pamoja na Kiemba na Samatta, Waarabu wa Morocco wameiheshimu timu nzima ya Tanzania kwa mchezo uwezo wake kisoka na kusema ina vipaji vingi, Thomas Ulimwengu, Frank Domayo, Salum Abubakar na Shomary Kapombe wakiwa wachezaji wengine waliowachengua zaidi.   
    Stars ilifungwa 2-1 na wenyeji Jumamosi katika mchezo wa Kundi C kuwania tiketi ya kucheza Fainali za Kombe la Dunia Brazil mwakani. 
    Hadi mapumziko, Morocco walikuwa mbele kwa bao 1-0 lililotiwa kimiani na Abderazak Hemed Allah dakika ya 37, baada ya yeye mwenyewe kujiangusha kwenye eneo la hatari baada ya kugongana na Aggrey Morris.
    Morris alitolewa kwa kadi nyekundu baada ya hapo na Stars wakabaki pungufu.
    Dakika ya 25 Thomas Ulimwengu alifanya kazi nzuri ya kumtoka beki, lakini shuti lake likadakwa na kipa.   
    Kocha Kim Poulsen aliwapumzisha kwa mpigo washambuliaji Mrisho Ngassa na Ulimwengu dakika ya 44 na kuwaingiza beki Nadir Haroub ‘Cannavaro’ na kiungo Khamis Mcha ‘Vialli’. 
    Kipindi cha pili Morocco walirejea na moto tena, wakiishambulia zaidi Stars iliyoonekana kudhoofika na katika dakika ya 50 Youssef El Arabi  akafunga  bao la pili kiulaini baada ya kuwatoka mabeki wa Tanzania na kubaki na kipa Juma Kaseja.  
    Hata hivyo, shambulizi la kushitukiza liliipatia Stars bao la kwanza dakika ya 61 lililofungwa na Amri Kiemba kwa shuti la mbali kutoka wingi ya kushoto.
    Dakika ya 82 Kim alimpumzisha Vialli na kumuingiza John Bocco ‘Adebayor’ ambaye aliongeza nguvu katika safu ya ushambuliaji.    
    Kwa matokeo hayo, Stars inabaki na pointi zake sita baada ya kucheza mechi nne, kushinda mbili nyumbani na kufungwa mbili zote ugenini, nyingine ikiwa dhidi ya Ivory Coast.
    Lakini Stars inabaki nafasi ya pili mbele ya Morocco yene pointi tano sasa, wakati Ivory Coast wanaongoza kwa pointi zao 10. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: BREAKING NEWS; AMRI KIEMBA ASAINI MIAKA MIWILI SIMBA SC MCHANA HUU Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top