![]() |
Hans Poppe katikati akijadiliana namna ya kuiwezesha Stars kushinda kesho na Magori kulia na DK Dau kushoto katika hoteli ya Pullman mjini Marakech. |
MWENYEKITI wa Kamati ya Usajili ya Simba SC, Zacharia Hans Poppe amesema kwamba amekuja Morocco kuongeza nguvu kuhakikisha timu ya soka ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars inafanya vizuri kesho katika mchezo dhidi ya Morocco kuwania tiketi ya kucheza Fainali za Kombe la Dunia.
Akizungumza na BIN ZUBEIRY mjini hapa, Hans Poppe mmoja kati ya wafanyabiashara wakubwa nchini, amesema kwamba yeye ni mwanamichezo na mzalendo halisi, hivyo amekuja hapa kwa kujitolea kuunganisha nguvu zake.
“Mimi ni mzalendo nah ii si mara ya kwanza kuongeza nguvu katika kampeni ya timu ya taifa, natambua na kuheshimu mchango mkubwa wa TBL wadhamini wakuu wa timu na hata Kamati iliyoundwa ya kusaidia timu. Lakini bado kila Mtanzania ana wajibu wa kuisaidia timu yake ya taifa. Ndiyo maana niko hapa,”alisema Poppe.
Kwa upande wake, Nahodha wa Taifa Stars, Juma Kaseja amesema kwamba wachezaji wote imara na tayari kwa mchezo wa kesho dhidi wa Simba wa Atlasi kuwania tiketi ya kucheza Fainali za Kombe la Dunia, Uwanja wa Marakech mjini hapa.
Akizungumza na Waandishi wa Habari mjini hapa, Kaseja ambaye pia ni Nahodha wa klabu ya Simba, amesema kwamba maandalizi kwa ujumla hadi sasa ni mazuri na wako tayari kabisa kukabiliana na wenyeji wao hao.
Kaseja alisema ana uwezo mkubwa na Morocco hivi sasa hii ikiwa ni mara ya nne kuja kucheza hapa, hivyo binafsi hana wasiwasi kabisa na mchezo wa kesho.
“Ushindi ndiyo lengo letu kubwa na tunaomba Watanzania watuombee dua ili tuweze kutimiza malengo yetu. Sisi tuki imara na tuko tayari kabisa, Morocco tunawajua na wala hatuna wasiwasi nao, ila tunawaheshimu kama timu kubwa na yenye uzoefu zaidi yetu,”alisema.
Kwa upande wake, Kaimu Mwenyekiti wa Kamati ya Ushindi ya Stars, Dk Ramadhani Dau amesema kwamba wanatekeleza vyema majumumu yao yaliyowaleta Morocco na mengine yatafuata baadaye,”alisema Dau.
Mkuu wa Msafara wa Stars, Cresscentius John Magori naye amesema mambo yanaendelea vizuri na matumaini kesho ni na hadi sasa mambo yanakwenda vizuri.
“Lengo letu ni kushinda kesho, lazima tupigane kushinda, ushindi.
Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Zuberi Kabwe naye yupo hapa kuiunga mkono Stars pamoja na Mwenyekiti wa Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania (TASWA), Juma Abbas Pinto.
![]() |
Nahodha Kaseja |
Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager, inashika nafasi ya pili katika Kundi C, ikiwa na pointi sita nyuma ya Ivory Coast yenye pointi saba, ambayo kesho itakuwa ugenini ikimenyana na Gambia katika mchezo mwingine wa kundi hilo.
Kabla ya kuja hapa, Stars iliweka kambi ya wiki moja katika hoteli ya Tansoma, Dar es Salaam ikijifua Uwanja wa Karume na siku chache kabla ya kuondoka ilialikwa Ikulu na Rais Jakaya Kikwete, aliyewapa hamasa kwa hotuba nzuri.