• HABARI MPYA

    Wednesday, June 12, 2013

    VIVA TAIFA STARS, VIVA TANZANIA, ALUTA CONTINUA…

    IMEWEKWA JUNI 12, 2013 SAA 12:00 ASUBUHI
    MATUMAINI ya Tanzania kucheza Fainali za kwanza za Kombe la Dunia kidogo yamefifia, kufuatia kufungwa mabao 2-1 kwenye Uwanja wa Marakech, Morocco Jumamosi katika mchezo wa Kundi C kuwania fainali za mwakani nchini Brazil.
    Zikiwa zimebaki mechi mbili mbili kwa kila timu kuhitimisha michezo ya kundi hilo, Tembo wa Ivory Coast wanaizidi Tanzania, Taifa Stars kwa pionti nne kufuatia wao kushinda 3-0 dhidi ya Gambia, timu nyingine kwenye Kundi hilo Jumamosi. 

    Pamoja na kufungwa 2-1, Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager ilikuwa ina uwezo kabisa wa kuwafunga wenyeji kwenye Uwanja huo maridadi wenye uwezo wa kuchukua mashabiki 45, 240, lakini mambo kadhaa yaliikosesha ushindi.

    STARS ILIFUNGWA KATIKA MECHI ILIYOSTAHILI KUSHINDA
    Kwa mtazamo wa Watanzania, Morocco iliingia kwenye mchezo huo ikiwa haina cha kupoteza, iliyokata matumaini ya kusonga mbele, hivyo haikuwa na wasiwasi wowote, zaidi ya kucheza kulinda heshima yake nyumbani.
    Lakini ukweli ni kwamba, hadi sasa katika Kundi C Tanzania, Ivory Coast na Morocco yoyote inaweza kufuzu hatua ya mwisho ya kuwania Fainali za Brazil mwakani.
    Stars walijiamini kupita kiasi na kwa kumbukumbu ya ushindi wa 3-1 katika mchezo wa kwanza Dar es Salaam, matumaini ya Tanzania yalikuwa juu mno.
    Ushindi ndicho kitu pekee ambacho msafara mzima wa Stars Marakech ulikuwa unakifikiria na mipango yote ilikuwa ni juu ya namna ya kushinda mchezo huo.
    Neno “Lazima tushinde” lilitamkwa kuanzia na viongozi wa Kamati ya Ushindi, viongozi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Serikali, benchi la Ufundi, wachezaji na hata baadhi ya wananchi waliokwenda kuisapoti timu nchini humo. 
    Hakuna aliyejali timu inacheza ugenini, ambako kwa kawaida ni vigumu kushinda, hadi siku moja kabla ya mechi, baada ya wenyeji kuifanyia timu vitendo visivyo vya kuanamichezo.
    Stars ilifanyiwa vurugu na kuzimiwa taa siku moja kabla ya mechi ili ishindwe kufanya mazoezi kwenye Uwanja huo siku moja kabla ya mchezo kwa mujibu wa sheria za FIFA. 
    Sheria za FIFA zinasema timu mgeni, itapewa fursa ya kufanya mazoezi katika Uwanja utakaotumika kwa mechi dhidi ya wenyeji katika muda ambao mechi itachezwa, lakini Ijumaa msafara wa Stars ulipofika Uwanja wa Marakech ulizuiwa kuingia ndani na askari wa uwanjani hapo. 
    Juhudi za Kocha wa Stars, Kim Poulsen kuwaelewesha askari wa Uwanja huo sheria ili wairuhusu timu kuingia uwanjani hazikuzaa matunda na ikabidi viongozi wa TFF waingilie kati, nao pia wakachemsha.
    Ikawadia zamu ya viongozi wa Kamati ya Ushindi ya Stars, ambao nao walichemsha- ndipo baadhi wa Watanzania waishio huko na wachache waliosafiri kutoka Dar es Salaam walipoongeza nguvu kwa kwenda kufungua geti kwa nguvu, wakawaweka kando askari waliokuwa wanawazuia na kuiingiza timu uwanjani kufanya mazoezi. 
    Hata hivyo, Stars ilipofika uwanjani ililazimika kusubiri tena, kwani wenyeji Simba wa Atlasi walikuwa wakiendelea na mazoezi.
    Baada ya nusu saa, Morocco walimaliza awamu yao na Stars wakaanza kupasha misuli moto. Hata hivyo, baada ya dakika 34, taa za Uwanja huo zilizimwa na uwanjani kuwa giza totoro, lakini viongozi wa TFF wakaenda kuomba, zikawashwa na timu ikafanya mazoezi kwa dakika 10 zaidi na kwenda kupumzika katika hoteli ya Pullman walipofikia. 
    Njama nyingine zikafuatia katika hoteli, wenyeji walitaka kutia dawa zenye sumu ili kuwaathiri wachezaji wa Stars, lakini viongozi wakashitukia hilo na timu haikula tena katika hoteli hiyo hadi inaingia uwanjani.
    Siku ya mchezo, mapema asubuhi vijana watatu walipelekwa kwenye Uwanja wa Marakech kwenda kukagua vyumba vya kubadilishia nguo ambavyo Stars ilitakiwa kuingia na kufika huko, wakakuta vyumba vimepuliziwa dawa yenye sumu.
    Wakatoa taarifa kwa viongozi hotelini, ambao wakaagiza ufanyike usafi wa kuhuisha sumu hiyo. 
    Pamoja na kufanya hivyo, lakini wakati timu inakwenda uwanjani, harufu ile ya dawa yenye sumu ilikuwa kali kama iliyopuliziwa muda huo na uchunguzi ukabaini, inapitishiwa kwenye viyoyozi vinavyonyunya kwenye chumba hicho, hivyo ikaamriwa wachezaji wasiingie kabisa kwenye vyumba hivyo.    
    Timu iliingia uwanjani ikitokea kwenye sebule na tangu hapo ndipo sasa Watanzania wakajua Morocco wanataka ushindi katika mchezo huo na dharau ikaishia hapo 

    STARS HAIKUSTAHILI KUIDHARAU MOROCCO HATA CHEMBE
    Kwa kweli Tanzania haikustahili kuidharau Morocco kwa aina yoyote, kwani pamoja na jeuri ya ushindi wa 3-1 katika mchezo wa kwanza Dar es Salaam, bado Simba wa Atlasi wako juu kisoka kuliko Taifa Stars.  
    Morocco wanaoshika nafasi ya 74 kwa sasa katika viwango vya soka duniani vya FIFA, wanagombea kucheza Fainali za Kombe la Dunia kwa mara ya tano, wakati Tanzania haijawahi kunusa hata mara moja.
    Walicheza kwa mara ya kwanza Fainali za Kombe la Dunia mwaka 1970 wakaishia hatua ya makundi, Fainali za pili mwaka 1986 wakatolewa hatua ya 16 Bora, za tatu 1994 na za nne 1998, zote wakitolewa hatua ya makundi.
    Ni timu ambayo inaundwa na wachezaji wengi wanaocheza Ulaya, ambao katika kipindi hiki cha majira ya joto wanakabiliwa na changamoto ya kucheza soka ya kiwango cha juu, ili kulinda au kukuza masoko yao Ulaya.
    Hiki ni kipindi cha usajili, wachezaji wa Afrika wanaocheza Ulaya wanatumia fursa hii ya mechi za kufuzu kwa Kombe la Dunia kujitafutia masoko kwenye timu mbalimbali- na hata kwa wale ambao wanacheza Afrika bado, huu ndiyo wakati wao wa kujiuza.
    Kwa hivyo, Morocco walikuwa wana kila sababu ya kucheza kwa ushindani kama timu na hata kwa mchezaji mmoja mmoja, hivyo mechi ya Jumamosi ilikuwa ngumu na si ya kudharau.  

    BENCHI LA UFUNDI LIKAHARIBU ZAIDI
    Siku moja kabla ya mechi ilipobainika kocha Kim Poulsen ataanza na washambuliaji wawili, tofauti na mfumo ambao umezoeleka amekuwa akilundika viungo wengi na kuacha mshambuliaji mmoja dhahiri Mdenmark huyo aliamua ‘kujilipua’ katika mchezo huo.
    Pamoja na matokeo mazuri katika mechi kadhaa zilizopita, timu ya Tanzania bado haijaiva kiasi cha kutosha kuweza kucheza mchezo wa kushambulia moja kwa moja dhidi ya timu kama Morocco na Ivory Coast.
    Bado mfumo bora kwa timu yetu ni ule ule wa kulundika viungo wengi katikati na kutumia mashambulizi ya kushitukiza na hilo lilidhihirika baada ya kipindi cha kwanza tu cha mchezo huo.
    Katika dakika 45 za kwanza tulizidiwa na baada ya Morocco kupata bao la kwanza na wakati huo huo beki Aggrey Morris akitolewa nje kwa kadi nyekundu dakika ya 37, dhahiri kocha Kim na benchi lake zima la ufundi walionekana kuchanganyikiwa.
    Kimtazamo, lilikuwa kosa kumuanzisha Thomas Ulimwengu pamoja na Mbwana Samatta bali, ingefaa mmoja akatokea benchi kipindi cha pili, lakini kosa la pili likafuatiwa katika mabadiliko ya dakika ya 44.
    Kim aliwatoa Ulimwengu na Mrisho Ngassa na kuwaingiza beki Nadir Haroub ‘Cannavaro’ na kiungo wa pembeni Khamis Mcha ‘Vialli’.
    Ilikuwa lazima aingie beki mwingine baada ya kutolewa kwa kadi nyekundu Morris na ilikuwa sawa kwa Ngassa kutoka, lakini lilikuwa kosa kumtoa Ulimwengu japokuwa alikosa bao la wazi dakika ya 25.
    Ulimwengu alikuwa mwiba kwa safu ya ulinzi ya Morocco na wakati wowote ilitarajiwa angefanya kitu. Kocha alipaswa kutulia kumalizia dakika 45 za kwanza ndipo atafakari mabadiliko, lakini ikiwa imebaki dakika moja tu mchezo kuwa mapumziko, akafanya mabadiliko ya ‘ovyo’.
    Timu ilidhoofika zaidi na mapema kipindi cha pili ikapachikwa bao la pili, kabla ya Amri Kiemba kufunga la kufutia machozi kwa juhudi zake binafsi kutokana na shambulizi la kushitukiza.
    Dakika nane kabla ya filimbi ya mwisho, Kim akamtoa Mcha aliyemuingiza dakika ya 44 na kuingiza mshambuliaji mwenye nguvu kama Ulimwengu, John Bocco ‘Adebayor’, maana yake alijaribu kusahihisha makosa yake, lakini ni kama alikumbuka shuka kumekucha.

    STARS BADO INA NAFASI YA KWENDA  BRAZIL
    Ivory Coast wanaoongoza kwa pointi zao 10 watamenyana na Tanzania yenye pointi zake sita katika nafasi ya pili wikiendi ijayo. Stars ikishinda itaisogelea Ivory Coast na kubakiza tofauti ya pointi moja.
    Baada ya hapo, Ivory Coast watamaliza  nyumbani na Morocco, huku Tanzania ikimaliza ugenini na Gambia. ‘Mungu akijaalia’ Stars ikaifunga Gambia na Morocco ikalazimisha japo sare kwa Ivory Coast, Taifa Stars itamaliza na pointi 12 dhidi ya 11 za Tembo.
    Na izingatiwe, Morocco yenye pointi tano sasa, ikiifunga Gambia itafikisha nane, hivyo itaingia kwenye mchezo wa mwisho wa Ivory Coast kutafuta kutimzia pointi 11.  Na kama tutaifunga Ivory Coast, itabaki na pointi 10, hivyo Morocco watajenga imani Tanzania itafungwa na Gambia ugenini na kubaki na pointi tisa, (iwapo tutashinda Jumapili), hivyo watapigana kiume kushinda waongoze Kundi.
    Nafasi ya Stars kwenda Brazil bado ipo na vizuri wahusika wakapitia kwa umakini mchezo wa Jumamosi Marakech na kujipanga vyema kutorudia makosa yaliyoigharimu timu siku hiyo. 

    KOMBE LA DUNIA 2014 SI DIRA YA KIM POULSEN
    Mapema tu baada ya kupewa mikoba ya ukocha wa Stars Mei mwaka jana, Kim alisema dira yake ni kucheza Fainali zijazo za Mataifa ya Afrika ila kama mambo yatakuwa safi, basi hata Kombe la Dunia mwakani wanaweza kwenda.
    Kim aliangalia anaichukua timu katika wakati gani ikiwa katika hali gani na akaahidi kulingana na tathmini aliyoifanya juu ya majukumu yake.
    Hata ikitokea Stars ikakosa tiketi ya Brazil mwakani, bado anastahili kupewa nafasi zaidi kuangalia uwezekano wa kutimiza ndoto zake nyingine katika timu hiyo. Watu wanajifunza kutokana na makosa na hatutarajii Mdenmark huyo anaweza kurudia makosa ya kujilipua kama Marakech.  
    Ni ukweli usiopingika mwalimu huyo wa Denmark, amefanya kazi nzuri katika kipindi kifupi alichokuwa na timu hiyo na pamoja na kustahili pongezi na heshima anastahili pia kuendelea kupewa sapoti afanye kazi yake vizuri zaidi.
    Wakati Rais Jakaya Kikwete alipoialika Ikulu Stars ikijiandaa kwenda Morocco alipongeza matokeo ya timu siku za karibuni akawataka waende kushinda, lakini akisema kabisa halitakuwa jambo jepesi kuwafunga Waarabu kwao. Ndiyo, kweli haikuwa rahisi na Stars imefungwa, lakini bado bado ina nafasi ya kwenda Brazil. Viva Taifa Stars, Viva Tanzania. Aluta Continua.  
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: VIVA TAIFA STARS, VIVA TANZANIA, ALUTA CONTINUA… Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top