• HABARI MPYA

    Tuesday, December 04, 2012

    KAMA KAWA, WACHEZAJI WOTE ERITREA WAINGIA MTAANI KAMPALA, FUFA WAHAHA KUWASAKA

    Wachezaji wa Eritrea wakiwa jukwaani Uwanja wa Mandela, Namboole mjini hapa wiki iliyopita

    Na Mahmoud Zubeiry, Kampala
    WACHEZAJI 14 wa Eritrea wametoweka kambini kwao, baada ya kutolewa kwenye Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati, CECAFA Tusker Challenge mjini hapa Jumamosi.
    Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka la Uganda (FUFA), waandaaji wa mashindano ya mwaka huu, Rogers Mulindwa ameiambia BIN ZUBEIRY leo kwamba, hawakufanikiwa kuwapata wachezaji hao wakati wanatakiwa kuondoka leo mara tu baada ya kutolewa.
    Mulindwa alisema kambini wamebaki kocha Ngash Teklit na viongozi wengine wanne tu, lakini wachezaji wote hawapo.
    “Wachezaji 14 wametoweka kambini na hatujui walipo kwa sasa. Ndege yao inatarajiwa kuondoka leo, lakini tunaendelea na jitihada za kuwasaka kwa kushirikiana na Polisi,”alisema.
    Eritrea ilikuwa kundi moja na Rwanda, Zanzibar na Malawi na wakashika mkia katika kundi hilo, wakifungwa mechi zote na kutoa sare moja tu Zanzibar katika mechi ya kwanza.
    Sasa hii inakuwa desturi sugu ya nchi hiyo kuzamia nchi za watu wanapokwenda kwenye mashindano, kwani awali wachezaji wanne walizamia walipokwenda kucheza na Tusker nchini Kenya kwenye Ligi ya Mabingwa mwaka 2006 mjini Nairobi na wengine zaidi ya 10 walizamia kwenye michuano kama hii mwaka 2007 mjini Dar es Salaam.
    Waliwahi kuzamia pia walipokwenda Angola mwaka 2007 kucheza mechi ya kuwania kufuzu Fainali za Kombe la Dunia.
    Timu hiyo ilifanya hivyo hivyo mwaka 2009 nchini Kenya na katika kambi nzima alibaki kocha na mchezaji mmoja tu. Kutokana na mfululizo wa matukio hayo, walijitoa kwenye mashindano ya kimataifa mwaka 2010 na mashindano ya mwaka huu ya Challenge ndio ya kwanza kushiriki baada ya kurudi.
    Serikali ya Eritrea ilisema ili kudhibiti tabia hiyo, kila mchezaji atatakiwa kuweka bondi fedha za nchi hiyo 100,000 kabla ya kusafiri kwenda kuiwakilisha nchi, lakini hiyo nayo inaonekana bado haijawa tiba.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: KAMA KAWA, WACHEZAJI WOTE ERITREA WAINGIA MTAANI KAMPALA, FUFA WAHAHA KUWASAKA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top