• HABARI MPYA

    Tuesday, December 04, 2012

    KAMA SI MWADINI, NILIKUWA NIMEKWISHA, ASEMA CANNAVARO

    Cannavaro baada ya kukosa penalti jana

    Na Mahmoud Zubeiry, Kampala
    NAHODHA wa Zanzibar, Nadir Haroub ‘Cannavaro’ amesema kwamba anamshukuru sana kipa wao, Mwadini Ally kwa kucheza penalti ya Abdul Fiston wa Burundi jana, kwani vinginevyo walikuwa wamekwishatolewa kwenye Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati, CECAFA Tusker Challenge.
    “Mimi nilipokosa tu penalti kwa kweli mwili ulikufa ganzi na kuamini sasa safari ya kurudi Zanzibar imeiva na mimi ndiye nimewaangusha wenzangu. Sikuwa na raha tena, lakini nguvu ziliniijia baada ya Mwadini kucheza penalti,”alisema Cannavaro alipozungumza na BIN ZUBEIRY jana Uwanja wa Lugogo.
    Nahodha huyo wa Yanga SC ya Dar es Salaam, alisema kwamba baada ya kuitoa Burundi sasa anaamini Kombe la Challenge litakwenda Zanzibar, kwani haoni timu nyingine ya kuwasumbua wao katika mashindano haya.
    Zanzibar jana ilikata tiketi ya kutinga Nusu Fainali baada ya kuichapa Burundi kwa penalti 6-5 kufuatia sare ya bila kufungana ndani ya dakika 90 na sasa itacheza na mshindi kati ya Kenya na Malawi katika Nusu Fainali.
    Shujaa wa Zanzibar jana alikuwa ni Abdallah Othman aliyefunga penalti ya mwisho, baada ya kipa Mwadini Ally kupangua penalti ya Abdul Fiston wa Burundi.
    Manahodha wa timu zote, Nadir Haroub ‘Cannavaro’ wa Zanzibar na Suleiman Ndikumana wa Burundi walipoteza penalti zao jana.
    Ndikumana alikuwa wa kwanza kwenda kupiga na mkwaju wake ukaota mbawa na kupaa juu ya lango, wakati wenzake waliofunga mbali na Fiston kupoteza ni Steve Nzigamasabo, Amisi Tambwe, Chris Nduwarugira, Leopold Nkurinkiye na Gael Duhatindavyi.
    Upande wa Zanzibar Heroes, Khamis Mcha ‘Vialli’ alikwenda kufunga penalti ya kwanza ya Zanzibar, Adeyom Saleh Mohamed akafunga ya pili, Jaku Juma akafunga ya tatu, kabla ya Cannavaro kumpelekea mikononi mkwaju wake kipa Arthur Arakaza wa Burundi, Samir Hajji Nuhu akafunga ya tano, Aggrey Morris akafunga ya sita na Othman kutumbukiza nyavuni ya ushindi.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: KAMA SI MWADINI, NILIKUWA NIMEKWISHA, ASEMA CANNAVARO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top