• HABARI MPYA

    Tuesday, December 11, 2012

    KAMATI YA MGONGOLWA YAKETI KESHO KUMJADILI NGASSA

    Wakili Mgongolwa

    Na Mahmoud Zubeiry
    KAMATI ya Sheria, Maadili na Hadhi za Wachezaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), chini ya Mwenyekiti wake, Wakili Alex Mgongolwa, inatarajiwa kukutana kesho mjini Dar es Salaam kujadili uhalali wa kuuzwa kwa mchezaji Mrisho Ngassa.
    Ofisa Habari wa TFF, Boniphace Wambura Mgoyo amesema mchana wa leo katika Mkutano na Waandishi wa Habari kwamba, Kamati hiyo inakutana kufuatia malalamiko yaliyowasilishwa na klabu ya Simba iliyokuwa inamtumia mchezaji huyo kwa mkopo kutoka Azam FC.
    Hata hivyo, Kamati hiyo itakutana huku kukiwa kuna taarifa kwamba, Simba SC na Azam FC zimefikia makubaliano ya kumuuza kwa pamoja mshambuliaji huyo kwenda El Merreikh ya Sudan.
    Habari za ndani ambazo BIN ZUBEIRY imezipata kutoka kwenye kikao cha pamoja kati ya Simba na Azam jana, zimesema kwamba Merreikh imeongeza dau la kumnunua Ngassa kutoka dola za Kimarekani 70,000 hadi 100,000, zaidi ya Sh. Milioni 150 za Tanzania.
    Baada ya kuongeza dau hilo, Azam ilikutana na Simba kujadili pamoja ofa hiyo mpya na kukubaliana kumuuza na kugawana nusu kwa nusu.
    Upande wa Azam uliwakilishwa na mmoja wa Wakurugenzi wa bodi ya klabu hiyo, wakati kwa Simba waliwakilishwa na Makamu wao Mwenyekiti, Geoffrey Nyange ‘Kaburu’.
    Upande wa maslahi ya mchezaji umeboreshwa pia, Ngassa sasa atapewa dola za Kimarekani 75,000 zaidi ya Sh. Milioni 120,000 kwa kusaini mkataba wa miaka miwili na mshahara utabaki kuwa dola 4,000 (Sh. Milioni 6).
    Habari zinasema kwamba, baada ya makubaliano hayo, leo Simba na Azam watasaini mkataba na Azam na kumuuza rasmi mchezaji huyo.
    Hata hivyo, tangu wakati kikao hicho kinaendelea jioni ya jana, Ngassa alikuwa akitafutwa ili kuhusishwa, lakini hakupatikana kwenye simu.
    Wasiwasi umeibuka kwamba huenda Ngassa anaweza akawa ameghairi mpango wa kwenda Merreikh kutokana na ushauri mbaya wa watu wake wa karibu. Mchezaji mmoja wa timu ya taifa, aliiambia BIN ZUBEIRY jana kwamba Ngassa anafikiria kuachana na mpango wa kucheza Sudan, kwa sababu anasikia ni nchi ya Kiislamu na haina starehe.
    Wapembuzi wa mambo wanasema kwamba, ilipofikia Ngassa anahitaji ushauri nasaha, kwani nafasi aliyopata ni adimu na ni muhimu kwa taifa na hata kwa maslahi yake binafsi.
    Achilia mbali maslahi mazuri, lakini anakwenda kucheza timu ya ushindani ambayo itakuza kiwango chake aweze kuisaidia timu ya taifa pia. Merreikh ni timu ambayo karibu kila mwaka inashiriki Ligi ya Mabingwa.
    Dili la Ngassa kwenda Merreikh awali liliingia katika mgogoro, baada ya Azam kumuuza bila kuishirikisha Simba.
    Ikumbukwe, Azam walimtoa kwa mkopo Ngassa mwanzoni mwa Agosti, mwaka huu baada ya kukerwa na kitendo cha mchezaji huyo kubusu jezi ya timu yake ya zamani, Yanga, katika Nusu Fainali ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame, dhidi ya AS Vita ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
    Alifanya hivyo, baada ya kufunga bao la ushindi akitokea benchi na kuiwezesha Azam kutinga fainali ya michuano hiyo, ambako walifungwa na Yanga 2-0, naye kwa mara nyingine akitokea benchi na kushindwa kufunga, hivyo kutuhumiwa kucheza kinazi.
    Ilielezwa kwamba Simba walitoa Sh. Milioni 25 kumnunua kwa mkopo mchezaji huyo, ingawa baadaye Simba wakasema waliununua mkataba wa mwaka mmoja aliobakiza mchezaji huyo Azam FC, nao wakamuongezea wa mwaka mmoja kwa kumsainisha kwa Sh. Milioni 30, kati ya hizo Milioni 12 akipewa taslimu na 18 akipewa gari.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: KAMATI YA MGONGOLWA YAKETI KESHO KUMJADILI NGASSA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top